KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania – Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amesema kikosi chake kimeiva na kipo tayari kukabiliana na timu ya taifa lolote kwenye Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) yaliyopangwa kuanza Jumamosi hii.
Morocco amesema wamejifua na kujiandaa vilivyo kila idara na kwamba baada ya maandalizi ya muda mrefu, haoni timu ya kuwadhibu, huku akieleza kuwa amekuwa akifuatilia mfumo wa uchezaji wa Burkina Faso na kuwa na imani ya kupata ushindi katika mechi ya Jumamosi hii.
Mashindano ya CHAN yanatarajiwa kuanza kwa hafla kisha kufuatiwa na mechi baina ya Taifa Stars na Burkina Faso kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 2:00 usiku.
Tanzania ni mwenyeji mwenza wa mashindano haya kwa mara ya kwanza katika historia, kwa kushirikiana na Kenya na Uganda katika michuano hiyo mikubwa barani.

Ni wazi kwamba mechi hiyo itakuwa ya ushindani mkali, huku makocha wa timu zote mbili wakieleza matarajio yao ya kuanza mashindano kwa ushindi.
“Tupo tayari kukutana na timu yoyote katika mashindano haya kutokana na aina ya kikosi nilicho nacho. Tumefanya maandalizi ya kutosha na wachezaji wote wako fiti,” akasema Morocco.
Kocha huyo ameongeza kuwa michezo ya kirafiki waliyocheza kabla ya mashindano imesaidia kupunguza presha kwa wachezaji, hasa chipukizi waliopo kwenye kikosi hicho.
“Wachezaji chipukizi wameonyesha kiwango kizuri na kushirikiana vyema na wazoefu. Tunaamini tunaweza kufanya vizuri na kuacha kombe nyumbani,” amesisitiza.
Kwa upande wa afya ya wachezaji, Morocco amesema hakuna majeruhi mkubwa isipokuwa Clement Mzize, ambaye ana majeraha ya kawaida yanayomruhusu kuendelea na mazoezi huku akisubiri tathmini ya mwisho kutoka kwa daktari wa timu.
Morocco alawataka mashabiki wa soka nchini kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono Taifa Stars ili wachezaji wapate morali ya kucheza kwa jasho na damu kutetea heshima ya Taifa Tanzania.
Kipa Aishi Manula, akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, akasema lengo kuu ni kukusanya pointi nyingi katika hatua za mwanzo ili kujiweka vizuri katika kundi lao, akisisitiza kwamba wanaona Fahari kucheza kwenye ardhi ya nyumbani.
“Tunajivunia kucheza kwenye ardhi ya nyumbani. Tutapambana kuhakikisha tunashinda michezo yetu ya mwanzo,” amesema Manula.
Aliongeza kwamba uwanja watakaotumia ni jukwaa muhimu kwa wachezaji chipukizi kujitangaza mbele ya mawakala na mashabiki kutoka sehemu mbalimbali za Afrika.
Kocha Mkuu wa Burkina Faso, Issa Balbone, naye alitamba kuwa kikosi chake kimejiandaa ipasavyo na kwmaba wachezaji wapo tayari kwa mchezo huo muhimu, licha ya kwamba Taifa Stars wamo wachezaji wazuri.
Alisema wamekuja Tanzania kwa nia moja tu – kushinda mechi zao, moja baada ya nyinginena kuiheshimisha Burkina Faso na watu wake.