Mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu, Simba jumamosi iliungana na miamba mingine ya Yanga na Azam kuibuka na ushindi katika mechi za ugenini. Simba wakiwa nchini Botswana waliibuka na ushindi wa 1-0 na kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Kwa upande wa Yanga walitangulia kuibuka na ushindi katika mchezo wa kwanza, huku Azam wakicharaza Al Merreikh 2-0. TANZANIASPORTS inachambua kwa kina kuhusiana na mwenendo wa vilabu vya Tanzania katika mashindano ya Afrika.
Wapinzani wazipa ukubwa
Wapinzani wa Yanga walikuwa wa kwanza kuzungumzia ukubwa wa klabu hiyo. Bila shaka wapinzani hao wanatambua kuwa Yanga ni timu iliyotikisa frika kwa misimu ya karibuni ikiwemo kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho. Pia ni timu ambayo imekuwa gumzo kutokana na aina ya makocha wanaofundisha klabu hiyo. Hali kahdhalika Simba ambao wametoka kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho, wamekuwa timu ambayo imefaya vyema kwenye mashindano ya CAF na kuwa miongoni mwa vilabu gumzo.
Katika mazingira hayo, Simba na Yanga zinatajwa mara nyingi na wapinzani wao kuwa timu kubwa na dhahiri wanaogopa kukabiliana nazo. Simba na Yanga zimetetemesha ufalme wa vilabu vya Kiarabu na Afrika kusini ambako sasa Ligi Kuu Tanzania inatupiwa macho zaidi kutokana na mafanikio yao. ingawaje vilabu hivi havijachukua makombe lakini vinatajwa kuwa vigogo wa soka Afrika ambao wanapaswa kuogopwa. Hali hii inatokana na ushiriki wao kwenye mashindano ya CAF mara kwa mara.
Majirani waanza kujifunza
Hivi karibuni katika mjadala wa kituo kimoja cha Televisheni nchini Kenya, mada kubwa ilikuwa namna timu za Tanzania zinavyopiga hatua kwenye mashindano ya CAF. Wachangiaji wengi wanakubaliana kuwa Ligi Kuu Tanzaniua imepiga hatua kwa sbaabu ya uwepo wa wachezaji wa kigeni ambao idadi yao ni 12. Kwa mujibu wa taratibu za TFF zinaruhusu wachezaji 12 wa kigeni katika klabu zao. Hali hiyo imeongeza chachu kwa timu za Tanzania zinaposhiriki mashindano ya CAF kwani zimekaribisha vipaji vya uhakika. Kenya ni miongoni mwa nchi ambazo zinajaribu kusuka upya Ligi yao huku awakiwa tayari kujifunza kutoka Ligi Kuu Tanzania. Hatua hiyo imechukuliwa pia na majirani kama klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Je, Azam na Singida Black Stars kufuata nyayo za Yanga na Simba?
Hili ndilo swali ambalo linaulizwa na wadau wengi nchini. Lakini katika anga za Kimataifa tayari Simba na Yanga zimeandika majina yao kwa wino wa dhahabu kiasi kwamba zimekuwa za kuogopwa. Wakati Yanga na Simba zimekuwa timu za kuogopwa, upande mwingine vilabu vya Azam na Singida Black Stars vina kibarua kigumu kujipenyeza katika soka la Afrika. Wakati vilabu viwili vya Tanzania vinaogopwa, ni dhahiri Ligi Kuu inatakiwa kuingiza timu nyingine ambazo zitakuwa tishio Afrika. Azam na Singida Black Stars ni miongoni mwa timu za Ligi Kuu ambazo zimeingia kwenye mashindano ya CAF.
Vipaji kutoka nje
Wakati Simba na Yanga zinatajwa kuwa kumbwa na wapinzani wao, ni dhahiri viongozi wake wanapaswa kulinda thamani na hadhi yao. Njia ya kuhakikisha Simba na Yanga zinabaki kuwa juu ni lazima ziendelee kusajili wachezaji mahiri na wenye vipaji vikubwa. Kadiri vipaji vizuri vinapotua Ligi Kuu Tanzania ndivyo thamani yake inavyozidi kupanda. Vipaji kutoka nje ya nchi vinatakiwa kuwa vile vyenye hadhi ya Kimataifa na ambavyo vitalenda matunda Ligi Kuu. Wakati Yanga na Simba zinapokuwa na wachezaji mahiri maana yake vigogo wengine Afrika wanazitazama kama sehemu ya mavuno. Kwamba wachezaji wanaong’ara wakiwa Simba na Yanga wana nafasi kubwa ya kusajiliwa katika vilabu vya Al Ahly, Raja Casablanca, Kaizer Chiefs, Esperance, Wydad, RS Berkane na kadhalika. Ubora wa vipaji ni ubora wa Ligi Kuu. Hivyo usajili wa vilabu hivi unatakiwa kuwa bora.

