*Arsenal, Man U wachapwa
*Leicester wapotea njia
Ligi Kuu ya England imeendelea na maajabu yake, ambapo Arsenal ambao
wangeweza kushika usukani wamepata kichapo cha aina yake, Manchester
United nao wakalala huku pia vinara Leicester wakifungwa.
Arsenal walifungwa 4-0 na Southampton, kichapo kikubwa zaidi msimu
huu, kilichokuja katika siku ambayo ikiwa wangeshinda wangeongoza
ligi. Mabao ya wenyeji yalifungwa na mlinzi Cuco Martina, Shane Long
mawili na Jose Fonte.
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger anasema walipoteza changamoto nyingi,
lakini hakutaka kuwalaumu wachezaji wake, akiongeza kwamba bao la
kwanza lilifungwa huku Southampton wakiwa wameotea, la pili baada ya
kucheza madhambi na la pili mpira ulikuwa umeshatoka, akionesha kuwa
yote hayakustahili.
Kocha wa Saints, Ronald Koeman alionesha kushangazwa na ushindi huo
akisema si kitu cha kawaida kwa Arsenal kufungwa idadi hiyo ya mabao.
Olivier Giroud na Theo Walcott walikosa mabao kadhaa ambayo wangefunga
kwa kichwa.
Jumatatu hii Arsenal wanawakaribisha Bournemouth wakati Saints
watasafiri kwenda kucheza na West Ham.
Katika mechi nyingine, Manchester United walichapwa 2-0 wakiwa ugenini
kwa Stoke, ikiwa ni mara ya kwanza kufungwa mechi nne mfululizo katika
msimu tangu 1961 na kocha Louis van Gaal amesema angeweza kuamua
kuachia ngazi.
Van Gaal aliulizwa na wanahabari ikiwa anaona kibarua chake kipo
shakani na kuwa angefukuzwa, akajibu kwamba hilo si suala la kujadili
na mwanahabari bali na Ed Woodward, makamu mwenyekiti mtendaji wa
klabu hiyo, ila akasema wakati mwingine anaweza kuondoka mwenyewe
badala ya kusubiri kufukuzwa kazi.
Mabao ya Stoke yalifungwa na Bojan Krkic na Marko Arnautovic na katika
kujaribu kuokoa jahazi, Van Gaal alimwingiza nahodha wake, Wayne
Rooney mwanzoni mwa kipindi cha pili lakini hakusaidia chochote kupata
mabao.
Katika mechi nyingine, Aston Villa walikwenda sare ya 1-1 na West Ham,
Bournemouth wakaenda suluhu na Crystal Palace, Chelsea wakabanwa na
Watford na kumaliza mechi kwa 2-2 huku Liverpool wakiangusha mbuyu kwa
kuwafunga Leicester 1-0.
Manchester City waliwakandika Sunderland 4-1, Tottenham wakawakomelea
Norwich 3-0 na Newcastle wakalala nyumbani kwa 1-0 mbele ya Everton.
Leicester bado wanaongoza ligi kwa pointi 38 wakifuatiwa na Arsenal
wenye 36, Man City 35 na Spurs 32. Tatu wa mkiani ni Newcastle wenye
pointi 17, Sunderland 12 na Villa nane. Mabingwa watetezi Chelsea
wamebaki kwenye nafasi yao ya 15 wakiwa na pointi 19 mbili kutoka eneo
la hatari ya kushuka daraja.