Ujio wa Man City umefifisha nguvu ya Chelsea..Man Utd wanatumia gharama kubwa kusajili wachezaji pamoja na kubadilisha makocha bila kupata mafanikio yoyote…
KAMA hakueleweka basi sasa mashabiki na wapenda michezo wanalazimika kumwelewa aliyekuwa kocha wa Arsenal, Arsene Wenger kupitia viongozi wa sasa wa klabu hiyo. Watazame Edu Gaspar na Mikel Arteta wanavyoongoza Arsenal katika falsafa ya kocha wao wa zamani Arsene Wenger. Falsafa ya Wenger ingali inafanya kazi Arsenal.
TANZANIASPORTS imefuatilia mwenendo na taarifa zote muhimu za Arsenal pamoja na wapinzani wao, na kubaini kuwa Arsene Wenger ndiye kivuli kinachoongoza klabu hiyo. Ndiye mpishi wa falsafa ya Arsenal ikiwa chini ya wachezaji wake, wale aliowafundisha kandanda. Tathmini hii imejikita katika maeneo yafuatayo; mikataba ya wachezaji imeboreshwa, usajili wa wachezaji wenye viwango na vipaji,kuuza wachezaji katika muda sahihi kwa klabu na mchezaji.
Arsène Wenger ni alama ya falsafa ya Arsenal, kocha ambaye alichukua madaraka mwaka 1996 na kuipandisha thamani ya klabu hiyo.
Katika kipindi chake alitwaa mataji ya Ligi Kuu, FA na kushiriki UEFA kila msimu. Ilikuwa vigumu Arsenal kukosekana katika timu 4 za juu za kuwakilisha England hata akikosa ubingwa.
Kipindi hicho Wenger aliifanya Arsenal iweze kushindana na utawala wa Man United huku mapato yakiwa madogo takribani Pauni Milioni 70 kipindi hicho. Vilevile akachuana na vigogo kama Barcelona, Real Madrid, Juventus, AC Milan,. Inter Milan na nyinginezo.
Wenger pia alishuhudia ujio wa matajiri wanaomiliki timu kama Manchester United na Chelsea ambazo uwezo wao kifedha ulikuwa tishio sokoni, lakini Wenger alifanikiwa kuwadhibiti ndani ya uwanja kiufundi.
Pia, Wenger aligundua kuwa njia ya kupambana na timu zenye misuli mikubwa sokoni ni lazima Arsenal iondoke kwenye uwanja wa Highbury. Wenger aliona umuhimu wa uwanja mkubwa na mzuri ambao utakuwa kivutio kwa wengi. Ili kukamilika mkakati huo ilibidi Wenger azikatae ofa za timu zenye pesa kama Real Madrid, PSG ,Timu ya Taifa ya Ufaransa,Man United ,Chelsea na nyinginezo na akakubali kusaini mkataba wa miaka mitano kubaki Arsenal.
Alianza kuwasajili wachezaji chipukizi na wale ambao walikuwa na vipaji vizuri lakini vilikosa nafasi. Wenger aliwapa nafasi wachezaji ambao walionekana kana kwamba hawana cha maana uwanjani.
Alilazimika kuwauza baadhi ya Nyota wake kupata pauni Milioni 30 za kulipia deni katika mpango wa ujenzi wa uwanja mpya (wanaotumia sasa). Samir Nasri, Cesc Fabregas, Thierry Henry , Patrick Vieira, Ashley Cole waliuzwa kwa bei mwafaka ambayo ilisaidia Arsenal.
Wenger aliunda kikosi kwa shida lakini akawafanya wachezaji wake wawe na maarifa makubwa. Katika kipindi hicho ilishuhudiwa kikosi chake kikiwa na beki wa kushoto Mathieu Flamini (ambaye kimsingi ni kiungo mkabaji) na akaibua vipaji kama Kieran Gibbs na Alex Iwobi, Chamberlain na wengineo.
Ujio wa Man City umefifisha nguvu ya Chelsea. Man Utd wanatumia gharama kubwa kusajili wachezaji pamoja na kubadilisha makocha bila kupata mafanikio yoyote.
Liverpool wanahaha kumuunga mkono kocha wao Jurgen Klopp. Lakini hadi sasa kivuli cha Wenger kimesimama imara Arsenal. Siku chache kabla ya kuondoka Arsenal, wengi waliamini ingekuwa rahisi kufutilia mbali nyayo zake. Lakini walisahau kuwa Wenger aliunda kikosi chake kwa gharama nafuu, akatengeneza na kupandikiza maarifa kwao, ndiyo maana tunawaona Edu Gaspar na Mikel Arteta.
Wanafunzi wa Wenger hawa kwa kutumia kikosi kilichojaa vijana wasio na uzoefu katika mbio za ubingwa kilitetemesha EPL. Vijana wengi wenye vipaji Smith-Rowe, Odegaard, Sambi, Zinchenko, Ramsdale, William Saliba, Gabriel, Nketiah, Nelson na kadhalika. Kikosi Cha namna hiyo kilichojaa vijana ni ishara kuwa Wenger aliacha maarifa makubwa Arsenal na kwa wachezaji wake ambao walielewa falsafa ya uongozi wake.
Kwanini kivuli cha Wenger kipo Arsenal?
Tuanzie kwa Mkurugenzi wa Michezo, Edu Gaspar. Huyu alikuwa mchezaji wa Wenger. Mbrazil mwenye sifa zake Arsenal. Kwa Sasa anahitaji wachezaji vijana wenye vipaji na viwango vya juu. Ameongoza Arsenal hadi nafasi ya pili EPL pamoja na kurudi kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kukosekana kwa miaka 12. Edu anatumia mbinu na ujuzi aliochota kwa Wenger.
Arteta, ndiye kocha mkuu. Alicheza pamoja na Edu wakati ww Arsene Wenger. Naye anao ujuzi wa Wenger na maarifa yake.
Arteta anaamini vipaji na ufundi wa benchi lake. Ni muumini wa soka la kuvutia kama ilivyokuwa kwa Wenger.
Na Sasa kibarua cha kuirudisha Arsenal Kwenye michuano ya Ulaya amefaulu. Anahitaji ubingwa, na tayari ameanza kusuka kikosi chake kwa ajili ya UEFA. Kai Havertz toka Chelsea, Declan Rice toka West Ham ni miongoni mwa nyota ambao watakipiga Arsenal msimu ujao. Hivyo hatua ya kujenga kikosi cha vijana imepita, sasa wanaongezewa nguvu kwa wachezaji wa daraja la juu. Ni kivuli cha Wenger.
Comments
Loading…