Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Ufaransa vimebainisha kuwa ndani ya barua hiyo Mbappe amesisitiza kuwa hakuna uwezekano wa yeye kuongeza mkataba klabuni hapo hivyo anatarajia mambo mawili…
HEKAHEKA za usajili wa wachezaji wapya zinaelekea kushika kasi huku mshambuliaji wa Paris St. Germain (PSG) Kylian Mbappe akiwa ameibua zogo kubwa katika viunga vya jiji la Paris baada ya kuonesha nia ya kuwahama mabingwa hao wa Ligue 1. Kylian Mbappe ameripotiwa kuwaambia mabosi wa PSG kuwa hana mpango wa kuongeza mkataba wa kuichezea timu hiyo mara baada yaw a sasa kumalizika Juni mwaka 2024.
Uamuzi wa Mbappe umewalazimisha PSG kufikiria mpango wa kumpiga bei nyota huyo katika dirisha la sasa usajili kuliko kumpoteza bure Juni 2024. Mbappe amewaandikia barua mabosi wa PSG kuwajulisha msimamo wake, lakini imedaiwa kuwa amefichua mpango huo kwa vyombo vya habari ambavyo vimeripoti kuona barua hiyo.
Kylian Mbappe ameujulisha uongozi wa PSG ili ufanye uamuzi wa kumuuza sasa kuliko kumwacha aondoke bure msimu ujao. Wakati Mbappe akichukua uamuzi huo, upande wa pili Rais wa Rais Madrid, Florentino Perez amewaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa ana uhakika wa kumsajili nyota huyo lakini wanapswa kuwa na subira kwanza. Kumekuwa na mgogoro wa chinichini kati ya PSG na Mbappe hali ambayo inalifanya suala la mkataba wake kuwa katika mazingira magumu.
Mwanzoni mwa wiki hii, magazeti ya michezo yaliripoti habari ya kipekee kuhusu sakata la Mbappe, yakisema kuwa barua aliyoandika nyota huyo kwenda kwa uongozi wa PSG wameiona na waliwahakikishia wasomaji wao kuwa ni barua sahihi ambayo hata mabosi wa klabu hiyo wameshtushwa na hatua hiyo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Ufaransa vimebainisha kuwa ndani ya barua hiyo Mbappe amesisitiza kuwa hakuna uwezekano wa yeye kuongeza mkataba klabuni hapo hivyo anatarajia mambo mawili; kuuzwa katika dirisha hili la usajili au kuachwa amalize mkataba wake kisha PSG kuambulia patupu kwani ataondoka bure Juni 2024. Mkataba wake wa sasa unafika tamati Juni 2024 lakini kulikuwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja tena kadiri watakavyokubaliana.
Aidha, magazeti ya Ufaransa yametoa taarifa za kushtua juu ya malengo ya Mbappe na kushangaza uongozi wa PSG huku wakihoji ni wapi walikoipata barua hiyo. Hata hivyo PSG wanaamini kuwa barua hiyo imefichuliwa na kambi ya Mbappe mwenyewe makusudi kwa nia ya kuuambia umma kuwa hana mpango wa kubaki na kuweka wazi kuwa ni yeye ndiye ametoa taarifa kuliko klabu ikabaki na taarifa hiyo ndani kisha ikajigamba kuamua kumpiga bei. Barua hiyo imewachochea mabosi wa PSG waamue kumuuza Mbappe katika dirisha hili la usajili.
Barua hiyo haijawashtua mabosi wa PSG peke yao, badala yake imewakasirisha wamiliki wa timu hiyo serikali ya Qatar. Wamiliki wa timu hiyo toka Qatar wanaamini kuwa watafanya kila jitihada kuhakikisha Mbappe anabaki PSG zaidi ya mwaka 2024. Kwamba wanaamini watamshawishi kuongeza mkataba mpya ambao utamfanya abakie PSG kwa muda mrefu zaidi, lakini kuvuja kwa barua aliyoandika kwenda kwa uongozi wa klabu yake hakupokelewa vizuri na wamiliki hao, hasa baada ya msuguano mkali wa kusaini mkataba mpya msimu uliopita.
Sasa kumekuwa na hisia kwamba bodi ya klabu ya PSG huenda ikawa tayari kumuuza nyota huyo kwakuwa angali na thamani nzuri sokoni. “PSG imeshangazwa na uamuzi wa mchezaji wake, imeamua kw akauli moja safari hii itasimama katika msimamo thabiti, Mbappe anatakiwa kusaini mkataba mpya au kuuzwa kabla ya dirisha la usajili kufungwa,” vimeeleza vyombo vya habari vya Ufaransa.
Mbappe hataruhusiwa kuondoka bure klabuni hapo, kwa hali yake na namna inavyowatendea wachezaji wake PSG inaonekana kukosa ari ya kumshawishi nyota huyo abakie klabuni hadi mwishoni mwa mkataba wake wa sasa. “Mbappe hataondoka bure kwa namna yoyote ile,” ni baadhi ya maneno waliyokaririwa viongozi wa PSG na vyombo vya habari vya Ufaransa.
Mazingira yaliyotumika na hali ilivyokuwa wakati wa kusaini mkataba mpya mwaka 2022 yalionesha kuwa haukuwa rahisi kwa pande hizo mbili kufanya kazi pamoja. Kukubaliana na mkataba wa miaka miwili na mchezaji huyo pamoja na kuweka kipengle cha kuongeza mwaka mmoja kulionesha bayana juu ya kusitasita na klabu kukosa mipango madhubuti ya maendeleo yao.
Kama ilivyo kawaida yao, Real Madrid walikuwa katikati yay a mtafaruku wa Mbappe na PSG katika majadiliano ya kusaini mkataba mpya. Real Madrid walikuwa tayari na waliamini watamsajili nyota huyo, na inafahamika kuwa ni mchezaji kipenzi cha Florentino Perez. Akiwa amejaribu kumsajili mara kadhaa bila mafanikio, sasa kuna upenyo ambao unaonesha kuwa iwapo Mbappe ataondoka PSG basi timu inayofuata itakuwa ni Real Madrid. Kuondoka kwa nahodha wa Real Madrid, Karim Benzema kumeacha pengo katika safu ya ushambuliaji, hivyo Mbappe anabaki kuwa mchezaji wanayemtolea udenda kumsajili kuziba pengo lililoachwa wazi na Karim Benzema.
Comments
Loading…