in , , ,

KINA “HARRY KANE” WAMEFIKA SEHEMU WALIYOSHINDWA KINA “DAVID BECKHAM”

London imepambwa na tabasamu pana, tabasamu ambalo lilikosekana kwa muda mrefu. Miaka 28 imepita bila furaha kubwa ndani ya mioyo ya wapenda kandanda hapa England.

Pengine historia kubwa iliandikwa mwaka 1966, lakini historia hiyo haiwezi kuondoa ukweli wa historia iliyoandikwa mwaka 1990 kule Italy kwenye fainali za kombe la dunia zilizofanyika mwaka huo.

England ilifanikiwa kufika katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya kombe la dunia. Hatua ambayo ni kubwa baada ya ile hatua ya fainali za mwaka 1966 ambapo England alifanikiwa kubeba kombe la dunia.

Kufika nusu fainali ya kombe la dunia ni hatua kubwa sana, ndiyo maana kombe la dunia la mwaka 1990 litabaki kwenye kumbukumbu za vitabu vya nchi ya England kwa sababu lilizalisha heshima kubwa katika ardhi hii ya Malkia.

Heshima ambayo ilibebwa na nyota kama kina Garry Lineker, Peter Shilton, Bryan Robson. Nyota ambao walikuwa na vipaji vikubwa. Haikuchukua muda mrefu kwa England kupata vipaji vingine vikubwa.

Baada ya kizazi cha Garry Lineker kilikuja kizazi cha kina Beckham. Kizazi ambacho kilikuwa kimesheheni majina yenye vipaji vikubwa dunia.

Kizazi ambacho tuliamini kinaweza kikafika mbali katika mashindano ya kombe la dunia lakini kiliishia katika hatua ya robo fainali.

England ya leo

Wengi waliumia na kuona hakuna mipango dhabiti katika nchi ya England kwa sababu kizazi hiki kilibeba matumaini makubwa sana kutokana na aina ya wachezaji nyota waliokuwa ndani ya kikosi. Kikosi kilichokuwa na viungo mahiri watatu wa daraja la dunia kama Paul Schoes, Frank Lampard na Steven Gerrald. Nyuma kukiwa na mabeki visiki kama John Terry, Rio Ferdinand, Sol Campell, Ashley Cole. Ukuta ambao ulikuwa na safu ya ushambuliaji yenye majina kama David Beckham, Wayne Rooney, Joe Cole, Michel Owen.

Majina haya yalikuwa yamebeba matumaini makubwa sana tofauti na majina yaliyopo katika kikosi cha sasa kilichopo Russia.
Vyombo vingi vya habari safari hii havikuimulika timu ya taifa ya England katika jicho la ushindani. Wengi waliiona kama timu ambayo inaenda kusindikiza watu.

Haikubeba matumaini makubwa kipindi ilipokuwa inaenda Russia kwa ajili ya kombe la dunia. Wengi walitabiri haitofika mbali kulingana na aina ya kikosi ambacho walienda nacho pamoja na kocha Gareth Southgate ambaye alionekana hana uzoefu mkubwa.

Kuzifundisha timu za taifa za vijana za England ndiyo ilikuwa kazi kubwa kwakw kabla hajapewa mikoba ya kuionoa timu ya taifa ya England.

Mikononi mwake alibeba wachezaji ambao walionekana wa kawaida hata umri wao ulionekana kutowapa nafasi ya uzoefu.

Hii hali iliwafanya watu wengi kutowapa nafasi, vinywa vya wengi vilitawala timu kama Brazil na Ujerumani kama timu ambazo zitafika mbali.

Lakini leo hii imekuwa tofauti na matazamio ya wengi, England imesimama sehemu ambayo Brazil na Ujerumani walitakiwa kusimama kulingana na matumaini makubwa waliyokuwa wameyabeba awali kabla ya fainali hizi za kombe la dunia.

Hakuna anayekumbuka kwa sasa kuwa England haikupewa nafasi kubwa kutokana na aina ya wachezaji pamoja na kocha kukosa uzoefu. Umoja na upiganaji umewafikisha hapo, tofauti ya kikosi hiki na kikosi cha kina David Beckham ni moja tu, kikosi hiki hakikuwa kinaongelewa sana katika mlengo chanya.

Wengi waliamini kuwa hakitofanya vizuri, hivo presha kubwa haikuwa ndani ya wachezaji.Wachezaji wamejituma bila kuwa na presha kubwa kama presha ambayo walikuwa nayo kina David Beckham.

Inawezekana tunaweza kuwakumbuka kina Frank Lampard, Steven Gerrald, David Beckham, Wayne Rooney na Paul Scholes kwa sababu ya vipaji vyao vikubwa katika kipindi chao cha kucheza mpira, ila ukweli unabaki pale pale kuwa tutawakumbuka kina Harry Kane, Jesse Lingard, Harry Maguire kwa kuifikisha timu ya taifa ya England sehemu ambayo wao hawakuifikisha.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

72 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

TULIIACHA MIGUU YA MWANJALI TUMEAMINI ILIYOKUWA MIGUU YA WAWA

Tanzania Sports

TUNATEMBEA KWENYE GIZA AMBALO FEISAL “FEI” MTOTO LIMEMTIA UPOFU