SOTE tunakubaliana kuwa bingwa mtetezi wa Ligi Kuu hapa England amepepesuka msimu huu. Manchester City imekumbana na vipigo vingi msimu huu kiasi kwamba hawana matumaini ya kuanyakua kombe lolote. Pep Guardiola anaonekana kukubaliana na matokeo na hali ya klabu yake. Uchambuzi wa TANZANIASPORTS unaonesha klabu hiyo imekumbana na majeruhi wengi msimu huu, pamoja na makosa mengi ya wachezaji katika mechi mbalimbali.
Safu ua ulinzi na viungo kumekuwa na makosa yanayowagharimu na imefika wakati makocha wa timu pinzani wanacheza na timu hiyo wakiwa na mbinu ya kushambulia zaidi bila kuhofia chochote. Sababu kubwa ni kuelewa kuwa Man City wana msimu mbaya ambao hawawezi kurudisha makali yao haraka. Aidha, bingwa huyu mtetezi amekuwa na wachezaji ambao wanachoka sana, kiasi kwamba wanapopambana na timu imara kimwili wanajikuta wanaanguka ovyo.
Katika mechi kadhaa unaona wazi Man City wana shida ya utimamu wa miili, umakini na kutojiunganisha. Hata hivyo Pep Guardiola hakutaka msimu wake uende vibaya bila kuwa na suluhisho. Miongoni mwa suluhisho hilo ni usajili wa Abdukodir Khusanov. Beki huyu ni kijana mdogo mwenye umri wa miaka 20 lakini anakuonesha thamani na sababu ya Pep Guardiola kuwashawishi mabosi wake kumsajili kinda huyo.
Je Khusanov ni beki wa aina gani?
Kiasili huyu ni beki wa kati. Anaweza kupishana nafasi na Ruben Dias, John Stones na Manuel Akanji. Pia anaweza kucheza beki wa kulia ama kushoto kulingana na mahitaji ya kocha wake. Khusanov hajafanya mambo makubwa ya kuinusuru timu hiyo lakini ni mchezaji ambaye anaonesha suluhisho katika safu ya ulinzi. Kwa umri mdogo anaweza kuhimili mikikimikiki na kuzima mashambulizi hatari ya wapinzani wao. Sifa yake kubwa ni kusoma mbinu na mwelekeo wa wapinzani kusaka goli.
Kucheza mtu na mtu na kuziba nafasi pia. Ana kasi na nguvu za mwili. Uwezo wake wa kiakili na kuingia kwenye mfumo wa Pep Guardiola umeonekana wazi. Katika michezo ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Real Madrid, kwa mechi zote mbili huyu ndiye alionekana nyota wa mchezo kwani hakuna wakati ambao alishindwa kudhibiti nyendo za washambuliaji wa Real Madrid. Katika mchezo wao dhidi ya Liverpool alikuwa na wakati mzuri lakini ugeni wa EPL ulimfanya aonekane kama hana makali. Ni aina ya beki ambaye anasafisha makosa ya wenzake, mlinzi wa kati mwenye nguvu, mbabe na anayweza kuchuana na mshambuliaji yeyote.
Je Pep Guardiola anamzungumziaje beki wake?
Khusanov alisajiliwa mwezi januari akitokea Ligi Kuu Ufaransa. Akizungumzia tabia binafsi za mchezaji huyo Pep Guardiola aliiambia tovuti ya Manchester City, kuwa ni mchezaji mwenye tabia za aina yake kila wanapokwenda kucheza mechi kwenye viwanja vya ugenini. “Khusanov hapendi upuuzi puuzi, anaweza kusafiri na timu yetu akiwa hana begi la kuhifadhi vitu vyake, mfano vya usafi. Hana muda wa kuchukua vitu vingi. Anakuja kwenye maandalizi ya mechi, atacheza mpira na muda ukiisha tunaondoka, hana muda wa mambo mengi.” Akizungumzia suala la ufundi, Guardiola alisema “zingatia maneno yangu, mchezaji huyu amekuja kucheza mpira haswa, ana nguvu, mwepesi na kasi. Tuna bahati tulikuwa Kyle Walker mwenye kasi kubwa, lakini Khusanov naye ana kasi vile vile. Anajua mipambano ya kimwili na washambuliaji,”
Sura ya kitoto, roho ya kikatili
Hii ni sifa ambayo baadhi ya wachezaji wenye sura za kitoto lakini wanakuwa na roho za kikatili uwanjani. Mtazame Mesut Ozil alikuwa mahiri kwenye kiungo na aliwageuza wapinzani wake kama chapatti kadiri alivyojisikia. Ni aina ya wachezaji ambao unaweza kuwapuuza kwa mwonekano wake wa kitoto lakini kila anapopambana na washambuliaji na kulinda lango la Manchester City unabaini sababu nyingi zilizowafanya kumnunua nyota huyo.
Man City wanaelekea kujenga timu mpya baada ya kuboronga msimu huu. Khusanov ni miongoni mwa wachezaji waliowasili klabuni hapo katika dirisha dogo la usajili pamoja na Nico na Marmoush. Baadhi ya wachambuzi hawampi sana sifa zake kwa vile wanakumbuka kosa alilofanya kwenye mchezo wa klabu yake dhidi ya Chelsea. Lakini ukweli ni kwamba Khusanov ni atakuja kuwaumbua kwa umahiri wake. ni mchezaji ambaye kila klabu ingetamani kuwa naye. Miezi mitano atakayokuwa kwenye Ligi ya England itakuwa imempa uzoefu mkubwa msimu ujao. Msimu huo ataingia uwanjani akiwa anaelewa jinsi Ligi hiyo ilivyo na namna anavyotakiwa kuendana nayo.
EPL ni ligi inayotumia nguvu nyingi sana na inahitaji mchezaji mwenye mapafu ya mbwa, yaani yule ambaye anacheza dakika zote 90 bila kuchoka na mtumiaji mkubwa wa nguvu au ubabe dhidi ya wapinzani wao. Khusanov anaweza kufanya zaidi ya anachokifanya sasa.
Comments
Loading…