Dunia yake ilijengwa na udongo wa kutokata tamaa, udongo ambao ulichanganywa na maji ya kupambana kwa nguvu.
Mchanganyiko huu ndiyo ulioumba kiumbe kimoja kifupi. Kiumbe kipambanaji kweli, na kiumbe ambacho kilitoka katika maeneo ya kimasikini kweli.
Hii siyo hadithi ya kushangaza kusikia shujaa kuwa alizaliwa katika mji wa kimasikini. Hili halijawahi kuwa jambo la kushangaza kabisa.
Mashujaa wengi wametoka huko na wanazidi kutoka huko. Ni wachache sana ambao walitoka kwenye nchi ya asali na maziwa.
Lakini wengi wao hutoka kwenye nchi ya jua na vumbi. Ndiyo mazingira ambayo huwafanya kupigana kabisa ili kuifikia nchi ya maziwa na asali.
Chembechembe hizi ziliwekwa kwenye damu ya Alexie Sanchez. Zikawa zinazunguka mwilini mwake kadri ambavyo damu ilivyokuwa inazunguka mwilini.
Ndiyo maana maisha yake yametawaliwa na kukataliwa ila bila kukata tamaa. Alikatawaliwa sana tangu akiwa nchini Chile lakini hakukuribisha neno kukata tamaa kwenye moyo wake.
Karibu na moyo wake kulikuwepo na mshale wa ushujaa. Mshale ambao ulikuwa na sumu ya upambanaji haswaa. Sumu ambayo aliishi nayo sana.
Ndiyo maana hata alipotoka ligi kuu ya Italy nakwenda katika ligi kuu ya Hispania (Seria A) katika klabu ya Barcelona huko nako alikataliwa.
Pep Guardiola hakuwahi kumkubali. Hakuwahi kumuona kama chaguo namba moja katika kikosi chake cha Barcelona.
Aliishi maisha hayo kwa muda mrefu. Maisha ya kuonekana yeye siyo chaguo la kwanza la Barcelona, lakini hakujali hilo.
Ndani yake alifikiria kupambana tu. Hata alipouzwa kwenda Arsenal ya ligi kuu ya England hakukata tamaa. Alitulia na kuendelea kupambana.
Kitu kizuri alienda sehemu ambayo ilimsaidia kukua zaidi. Sehemu ambayo alipewa nafasi kubwa zaidi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
Sehemu ambayo ilimwamini sana na kumuona kama jemedari mkuu wa kikosi cha Arsenal kwa kipindi hicho chini ya Arsene Wenger.
Nani ambaye hakumjua Alexies Sanchez wakati yuko Arsenal?. Yule mshambuliaji ambaye alikuwa anacheza kama false 9 huku akifunga magoli kuanzia 20 kwa msimu mmoja ?
Hapa ndipo upambanaji wake ulizidi kuonekana. Hakukata tamaa baada ya kukataliwa na Barcelona. Hakujali kuhusiana na hilo.
Alipuuza sana baada ya kukataliwa na Pep Guardiola , kocha ambaye anasadikika kuwa kocha bora kuwahi kutokea hapa duniani.
Unajisikiaje unapokataliwa na kocha mkubwa na bora duniani kama Pep Guardiola?. Hapana shaka inauma na inaweza kukufanya ukate tamaa.
Lakini kitu hiki Alexies Sanchez hakukiruhusu kabisa. Hakukipa nafasi ya kutosha katika maisha yake. Kitu pekee kilichokuwa kinatawala katika maisha yake ni mafanikio makubwa kupitia mpira wa miguu.
Ndiyo maana alipon’gara kupitia Arsenal , Pep Guardiola alimtaka aje katika kikosi cha Manchester City. Muda huu Pep Guardiola hakukumbuka kuhusu kumkataa akiwa Barcelona.
Alimuona kwa wakati huu kuwa ni mchezaji ambaye ni bora sana. Mchezaji ambaye anaweza kumsaidia Manchester City kutwaa makombe.
Lakini mwisho wa siku Alexies Sanchez aliichagua Manchester United. Wapinzani wakubwa wa Manchester City.
Inawezekana hili lilikuwa tusi kubwa kwa Pep Guardiola kutoka kwa Alexies Sanchez. Na inawezekana uhamisho huu ulitengeneza huzuni kubwa kwa Pep Guardiola.
Hiki kitu kilikuwa tofauti kwa Manchester United na mashabiki wake. Huu ushajili ulitengeneza furaha kubwa sana ndani ya Manchester United.
Nani ambaye hakumbuki mbwembwe kubwa ambazo zilitawala katika usajili huu wa Alexies Sanchez?. Hapana shaka hakuna.
Nani hakumbuki video iliyotazamwa na watu wengi duniani kupitia ukurasa wa twitter wa Manchester United ?
Video ambayo ilikuwa imebeba dhima ya utambulisho wa Alexies Sanchez pale Manchester United ?
Video ambayo ilikuwa inamuonesha Alexies Sanchez akipiga kinanda huku akiwa na jezi namba saba (7)?
Jezi ambayo inaheshimika sana katika kikosi cha Manchester United. Jezi ambayo imevaliwa na magwiji wakubwa wa mpira wa miguu.
Eric Cantona aliwahi kuvaa hiyo jezi. David Beckham aliwahi kuvaa hiyo jezi, George Best aliwahi kuvaa hiyo jezi , hata ngozi ya Cristiano Ronaldo iliwahi kufunikwa na hiyo jezi.
Bila shaka umeona ukubwa wa jezi hiyo. Lakini kwa wakati huo ilikuwa katika ngozi ya kijana kutoka ardhi ta kimasikini kutoka Chile.
Kijana mpambanaji, kijana mpiganaji haswaa, kijana asiye kata tamaa, kijana ambaye anapenda kucheza mpira kuliko kufanya mapenzi.
Sifa zote hizi ziliwapa jeuri ya kuwa Alexies Sanchez atafanya vizuri sana katika kikosi cha Manchester United.
Mashabiki wa Manchester United hawakuona aibu kabisa kusema kwa kujitapa kuwa walimpata mtu sahihi wa kuvaa jezi namba saba (7)
Jezi ya magwiji, jezi ya watu wenye vipaji maalumu, watu ambao waliwahi kufanya vizuri na Manchester United kipindi cha nyuma.
Lakini mategemeo yao yalikuwa tofauti kabisa na uhalisia. Walitegemea makubwa lakini uhalisia ulikuja kuonekana Alexies Sanchez akiwapa kidogo.
Bado mpaka sasa hivi wanatamani kumuona Alexies Sanchez akifanya vizuri ndani ya jezi ya Manchester United.
Bado wanatamani kuirudisha furaha yao iliyoishia katikati na haikufanikiwa kufika mwisho, lakini cha ajabu kinachoonekana mwisho watapata huzuni kuliko furaha waliyokuwa wanaitegemea.