Watuhumiwa zaidi kushitakiwa
Sakata la rushwa, wizi wa fedha na utakatishaji fedha huenda likatanuliwa zaidi miongoni mwa viongozi na taasisi wanaohusishwa na Shirikisho la Soka la Kimataia (Fifa).
Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Loretta Lynch amesema wanafkiria hatua zaidi kulingana na upelelezi unavtoendelea kuhusu kashfa kubwa zaidi kupata kuikumba Fifa.
Lynch amesema wanaendelea kupata mafanikio kwenye kazi yao na kwamba kwa kiasi kikubwa ushahidi umepatikana. Katika hatua nyingine inayochukuliwa na vyombo vya dola ya Uswisi, mali kadhaa zimenaswa zikihusishwa na fedha hizo chafu.
Mamlaka za Marekani zinafanya kazi kwa karibu na zile za Uswisi kwenye uchunguzi huo, ambapo Mei mwaka huu viongozi saba wa Fifa walikamatwa jijini Zurich na kuunganishwa na wengine saba katika mashitaka.
“Upelelezi hauna uzio na tunafuata kokote ushahidi utakakoongoza. Nashukuru kwamba kuna ushirikiano wa hali ya juu na kwa kiasi kikubwa tumekusanya ushahidi juu ya suala hili,” anasema Lynch.
Mei 14 mwaka huu, maofisa wa Fifa na watendaji wa masuala ya masoko na michezo walihusishwa na kadhia inayoonesha zaidi ya pauni milioni 97 zimetumiwa visivyo na wahusika.
Mwanasheria Mkuu wa Uswisi, Michael Lauber amesema kwamba taarifa mbalimbali muhimu zimenaswa, pamoja na kuanzishwa uchunguzi dhidi ya akaunti 121 kwenye benki tofauti.
Mwanasheria huyo amethibitisha pia kwamba wapelelezi wa Uswisi wanaendelea na uchunguzi juu ya kandarasi za haki za vyombo vya habari kwa fainali zilizopita za 2010 na 2014. Amesema kwamba upelelezi huo bado unaelekea utachukua muda mwingi.
Juni mwaka huu, Rais wa Fifa, Sepp Blatter alitangaza kwamba atajiuzulu nafasi hiyo, ikiwa ni siku nne tu tangu aliposhinda kwenye uchaguzi, akitetea nafasi yake akiwa na umri wa miaka 79.
Hata hivyo bado anaendelea kukalia kiti hicho, akidaiwa kwamba anaandaa rasimu za mageuzi makubwa kwenye chombo hicho kilichojikuta kwenye matata ya mlungula kuhusiana na fainali za Kombe la Dunia 2018 na 2022 nchini Urusi na Qatar.