Didier Deschamps amemjumuisha N’Golo Kante kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa kitakachocheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Uholanzi na Urusi mwezi huu.
Hii ni mara ya kwanza kwa kiungo huyo wa Leicester City kuitwa kwenye timu ya taifa. Huenda kesho Ijumaa atapata nafasi ya kucheza mchezo wake wa kwanza ya kimataifa dhidi ya Uholanzi.
Kiwango anachokionesha Kante kwenye kikosi cha Leicester City chini ya mwalimu Claudio Ranieri kinatosha kabisa kumshawishi Deschamps kumjumuisha kwenye timu ya taifa.
Nafikiri nyota huyo atafanya vizuri kwenye michezo ya kirafiki na hatimaye kupata nafasi ya kuwawakilisha Ufaransa ambao watakuwa wenyeji kwenye michuano ya Euro itakayoanza mwezi Juni.
Swali la kujiuliza ni kwamba je Kante anaweza kupata nafasi kwenye kikosi cha Deschamps? Takwimu za kiungo huyo kwenye msimu huu wa EPL zinatoa jibu la ‘ndio’ kwenye swali hilo.
Uwepo wa Lassana Diarra wa Marseille, Yohan Cabaye wa Crystal Palace, Blaise Matuidi wa PSG na Paul Pogba wa Juventus na wengine hauwezi kumnyima nafasi Kante kwenye kikosi cha Ufaransa.
Hainishangazi pia kuona Morgan Schneiderlin ameachwa nje na Didier Deschamps. Kiuhalisia hana nafasi kwenye kikosi kwa sasa.
Takwimu za EPL msimu huu zinaonesha N’Golo Kante ndiye kinara wa kunyang’anya mipira. Ana uwezo mkubwa pia wa kuziingilia pasi za maadui.
Deschamps anayafahamu haya vizuri. Amesema kuwa uwezo wa kiungo huyo wa kuirejeshea timu mpira unapokuwa mikononi mwa wapinzani na pia uwezo wake wa kupiga pasi ndivyo vilivyomshawishi amwite kikosini.
Amesema pia si kwamba hamuamini Schneiderlin ila tu ameamua kumpatia nafasi Kante ili aonyeshe alicho nacho kwenye michezo ya kirafiki kabla hajafanya uamuzi wa mwisho kuelekea michuano ya Euro.
Kwenye mfumo wa 4-3-3 ambao mwalimu Deschamps amekuwa akiutumia mara kadhaa kwenye michezo ya Ufaransa Kante anayo nafasi yake.
Nafasi yake ni ile ya kiungo mkabaji. Lassana Diarra hawezi kumyima nafasi N’Golo Kante iwapo kwa Didier Deschamps takwimu zina maana ziaidi ya majina ya wachezaji.
Pogba, Cabaye, Sissoko, Matuidi na viungo wengine watashindania nafasi za viungo wengie wawili kwenye 4-3-3.
Mafanikio ya Leicester msimu huu yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na N’Golo Kante. Amekuwa akiwakinga vizuri walinzi wa Leicester City.
Licha ya kazi nzuri ya Robert Huth, Wes Morgan na walinzi wengine wa Leicester lakini bila ya kiwango anachokionesha Kante kwenye upande wa ulinzi Leicester wasingekuwa na rekodi nzuri ya ulinzi walio nayo.
Vijana hao wa Ranieri ni mingoni mwa timu nne zilizoruhusu mabao machache zaidi msimu huu wa EPL wakiungana na Tottenham, Manchester United na Arsenal.
Mchango wa Kante kwenye hili si mdogo. Uwezo wake wa kunyang’anya mipira na kuziingilia pasi za wapinzani umekuwa ukiwarahisishia kazi walinzi wa Leicester msimu huu.
Deschamps anatakiwa kumpa nafasi Kante ili arahisishe kazi ya Laurent Koscielny na wenzie kwenye kikosi cha Ufaransa. Hili linaweza kumpa Deschamps mafanikio makubwa kwenye michuano ya Euro.
Ingawa Kante si mzuri sana kwenye mashambulizi anapolinganishwa na Pogba, Cabaye au Matuidi lakini ikumbukwe timu yoyote inahitaji kuwa na uzania ili iweze kupata mafanikio uwanjani.
Kante anahitajika kwenye eneo la kiungo mkabaji. Anastahili nafasi ya uhakika kwenye kikosi cha Ufaransa. Ila tusubiri kuona kiwango atakachoonyesha kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Uholanzi na dhidi ya Urusi wiki ijayo.