*Mizengwe yatumika kuacha mgombea mmoja
*Waziri wa Michezo ahusika, watu waandamana
Mchezaji maarufu wa soka wa zamani wa Sierra Leone, Mohammed Kallon ametupwa nje ya kinyang’anyiro cha kuwania uongozi wa Chama cha Soka (SLFA).
Kallon amekasirishwa na hatua hiyo, na kusema kuanzia sasa hataki kushiriki kwa namna yoyote kitu chochote kinachohusiana na soka.
Mizengwe hiyo imewakumba pia wagombea wengine wawili wa nafasi ya urais, Rodney Michael na Foday Turay.
Kwa msingi huo, amebakishwa mgombea mmoja, Isha Johansen, ambaye itakuwa kama kumsukuma mlevi tu, kwa sababu kitakachofanyika ni kumpitisha kwani hana mpinzani.
Kwa mara nyingine soka ya Afrika imetumbukia gizani, ikiwa ni si muda mrefu tangu Shirikisho la Soka Afrika litupe mbali wagombea wengine na kumpitisha bila kupingwa Issa Hayatou ambaye amekuwa kama rais wa maisha.
Mizengwe pia ilifanyika kwenye uchaguzi wa Tanzania, kwa wagombea wenye sifa, kama inavyoelezwa hawa wa Sierra Leone, kutupwa mbali, lakini uchaguzi huo unarudiwa baada ya Fifa kuingilia kutokana na mzozo uliotokea wa serikali na mahakama.
Kallon (33) ni mchezaji wa zamani wa Inter Milan ya Italia na AS Monaco ya Ufaransa, akiwa mpachika mabao mzuri.
Kifungu kilichomwondoa kwenye kushiriki ni kile kinachotaka mgombea awe ameishi nchini Sierra Leone kwa miaka mitano mfululizo kabla ya kugombea, na kiliwekwa ikijulikana kuna nyota kama huyo aliyekuwa ng’ambo akisakata soka na ana uelewa mkubwa wa masuala hayo.
Mwaka 2010, Kallon alisaini mkataba wa mwaka mmoja na klabu ya Shaanxii Chanba FC ya China, ambapo wakuu wa FA wanasema mwaka 2001 na 2008 pia alipata hati za kuishi nchi nyingine, hivyo hangeweza kuwa Sierra Leone kwa miaka mitano mfululizo kabla ya mwaka huu.
Kallon anasema: “Nimefadhaishwa sana na uamuzi huu ninaoamini ni wa kisiasa, kwa sababu Waziri wa Michezo, Paul Kamara anamuunga mkono Isha waziwazi.
“Najua ninazo sifa, nimejitolea miaka 19 ya maisha yangu kuchezea Sierra Leone, nimetoa fedha nyingi kwa ajili ya Kallon FC na kusaidia kuendeleza vijana walio ya miaka 15…wengi wanacheza ng’ambo na asilimia 80 ya wanaochezea timu ya taifa ni matunda yangu, bado hivi ndivyo wanavyonilipa.
“Sasa najua kwamba sitakiwi wala sipendwi Sierra Leone, si serikali tu bali kwa ujumla na kwa msingi huu klabu yangu ya Kallon FC imekufa, sitaki tena chochote kinachoihusu soka ya Sierra Leone!”
Wagombea wengine, Michael na Turay waliondolewa kwa madai ya kukiuka Ibara ya 25 ya Fifa inayozuia kushughulika na kamari, bahati nasibu na mambo kama hayo kwenye soka.
Wote wamekanusha na kusema ni mizengwe tu, ambapo mamia ya wafuasi wa Kallon na Michael walijaribu kwenda Freetown kuonana na Rais Ernest Boi Koroma, lakini walizuiwa.
Walibeba mabango yaliyoandikwa: ‘Bila Rodney, bila Kallon hakuna soka’. Uchaguzi huo ulitakiwa kufanyika zaidi ya mwaka mmoja uliopita, lakini uliahirishwa mara kadhaa, baada ya kutokea kutoelewana juu ya nani ana sifa za kugombea urais.
Comments
Loading…