in

JURGEN KLOPP ANAHITAJIKA ANFIELD

 

Baadhi ya vyombo vya habari vya Ulaya vinaripoti kuwa siku za Brendan Rodgers Anfield zinahesabika. Meneja huyo ambaye alijiunga na Liverpool mwaka 2012 akitokea Swansea ameshindwa kuipatia Liverpool mafanikio wanayoyahitaji.

Ingawa kwenye msimu wake wa pili aliiwezesha timu hiyo kumaliza kwenye nafasi ya pili nyuma ya Manchester City waliotwaa ubingwa lakini msimu uliopita alishindwa kuiwezesha kumaliza angalau kwenye nafasi nne za juu.

Mbaya zaidi msimu huu timu hiyo inaonekana kuyumba. Mbaka sasa ikiwa imeshacheza michezo sita imeshinda michezo miwili tu na kujikuta kwenye nafasi ya 13. Ni mapema mno kuwakatia tamaa kwa sasa. Lakini kiuhalisia Liverpool haionyeshi matumaini ya kumaliza angalau kwenye nafasi nne za juu mwishoni mwa msimu.

Hata hivyo kiu ya mashabiki na bodi ya uongozi ya Liverpool sio kuwemo kwenye nafasi nne za juu. Wanachokiota ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England ambao waliutwaa kwa mara ya mwisho msimu wa 1989/90. Imepita misimu 25 sasa tangu timu hiyo yenye historia kubwa England ilipotwaa ubingwa wake wa mwisho.

Uwezekano wa Rodgers kuondolewa kwenye kibarua chake ni mkubwa na huenda akatimuliwa wiki chache zijazo ikiwa mambo yataendelea kwenda vibaya Anfield. Pengine atabakia mbaka mwishoni mwa msimu ikiwa timu itakuwa na muelekeo mzuri lakini sioni uwezekano wa kocha huyu kuendelea kuinoa Liverpool msimu ujao.

Kocha wa zamani wa Borussia Dortmund, Jurgen Klopp amekuwa akihusishwa na kuchukua nafasi ya Rodgers ikiwa atatimuliwa. Baadhi ya vyanzo vinaarifu kuwa Klopp anatamani kwenda kufundisha soka England. Rekodi za Jurgen Klopp zinashawishi kuwa kocha huyu ndiye mtu sahihi zaidi wa kukata kiu ya mashabiki Anfield.

Klopp aliteuliwa kuwa kocha wa Dortmund mwaka 2008 baada ya timu hiyo kumaliza kwenye nafasi mbaya ya 13 kwenye msimu ulikuwa umemalizika. Kwenye msimu wake wa kwanza akaipandisha timu hiyo mbaka kwenye nafasi ya 6 kisha nafasi ya 5 kwenye msimu wake wa pili.

Kwenye misimu ya 2010/11 na 2011/12 akaiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani ambao timu hiyo ilikuwa imeutwaa kwa mara ya mwisho kwenye msimu wa 2001/02. Mafanikio ambayo Klopp aliyapata akiwa na Dortmund ni makubwa mno hasa inapozingatiwa kuwa kiasi cha fedha alichokitumia kusajili kilikuwa ni kidogo mno ikilinganishwa na waliokuwa wapinzani wake wakuu Bayern Munich.

Kabla ya kuanza kwa msimu wa 2010/11 Klopp alitumia kiasi cha chini ya euro milioni 6 kusajili wachezaji na bado akafanikiwa kuiwezesha Dortmund kutwaa ubingwa wa Bundelsiga zikiwa zimesalia mechi mbili. Bayern Munich walikuwa wametumia zaidi ya mara mbili ya kiasi hicho lakini hawakuweza kufua dafu.

Msimu uliofuata, 2011/12 Klopp akaipa Dortmund ubingwa kwa mara ya pili mfululizo akiwa ametumia kiasi cha chini ya euro milioni 10 wakati Bayern walitumia takribani euro milioni 45 kwa ajili ya usajili. Zaidi ya hapo aliiwezesha Dortmund kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliofuatia.

Hii ianonyesha kuwa Klopp ndiye kocha atakayeweza kuwafanya Liverpool kuwa washindani wa kweli wa ubingwa wa EPL dhidi ya Manchester City, Chelsea na Manchester United ambazo huwa zinatumia pesa nyingi mno kusajili wachezaji wa viwango vya juu.

Klopp ana uwezo mkubwa wa kimbinu na uhamasishaji kwenye timu ambao unaweza kuipa mafanikio Liverpool ingawa haina uwezo wa kifedha kusajili wachezaji ikilinganishwa na timu nilizozitaja hapo juu. Kwa namna yoyote ile kocha huyo anahitajika Anfield.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

KASHFA YA JINAI FIFA:

Tanzania Sports

YANGA WAWATWANGA WATANI