in , ,

JONAS MKUDE, HADITHI AMBAYO TULIKUWA TUKIITAMANI

Masikio yetu yanapenda vingi sana vya kufurahisha, na muda mwingi masikio yetu hupenda kutabasamu.

Ni ngumu sana kuweka tabasamu kwenye sikio lako kwenye dunia hii ambayo ina watu wengi ambao hawana upendo kwako.

Muda mwingi wanawaza kukuumiza hata siku ambayo wakikuona uko sehemu ambayo ni juu hutamani kukushusha chini ambapo walipo.

Furaha yao ni utekeseke nao kwenye vumbi ambalo wapo wao!, hawawezi kufurahia kukuona ukila upepo wa juu.

Mioyo yao hujawa na chuki sana, ndiyo dunia ambayo tulipo. Dunia ambayo hata wachezaji wetu huendeana kwa waganga ili kumfanya mchezaji fulani apate majeraha ili yeye apate nafasi.

Wachezaji ambao hawaamini hata kidogo katika kujituma. Neno kujituma kwao halipo kabisa katika akili yao ndiyo maana kila uchwao wanakuwa katika kiwango cha kawaida sana.

Lakini kwenye dunia hii tuliyopo sisi Watanzania huwa tunawaamini sana na kuwapa nafasi sana katika midomo yetu. Hili ndilo soka letu, soka ambalo mwenye kipaji kikubwa hana thamani kubwa mbele ya macho yetu.

Soka ambalo hata viongozi wa vilabu vyetu hutumika Mara kwa Mara kuwashusha wachezaji wetu tu bila sababu na wakati mwingine ni chuki tu huwa zinawaongoza.

Hawaoti mafanikio ya mpira wetu, ubinafsi umewatala sana na hawaogopi kumpoteza mchezaji mwenye kipaji kwa hila zao ambazo hazina msingi.

Tuko hapo!, na tumefikia hapo na hatutaki kuondoka hapo kwa sababu tunapenda kusimama kwenye uchafu bila kujishtukia.

Leo hii kuna mtu katika dimba la timu ya Simba katulia sana, haongei sana na Inawezekana hana muda na mtu.

Yeye anafikiria kazi yake tu hamfikirii mtu mwingine yeyote. Alipitia katika kipindi kigumu. Kipindi ambacho hakikumpa nafasi ya kufikiria jinsi ya kukidumisha kipaji chake.

Aliporwa unahodha, kitu ambacho ni kikubwa sana. Ulizoea kuwaongoza watu. Ukawa kiongozi wao ambao kuna wachezaji walikuamini.

Lakini mwisho wa siku unaporwa unahodha. Mapokeo binadamu hutofautiana mmoja baada ya mwingine.

Wengine hupokea vitu kulinagana na vilivyo na wengine hukaa na kufikiria kwanza ndipo huruhusu akili yao kupokea hicho kitu.

Kwenye soka letu hatuna hao wachezaji ambao hukaa na kufikiria kwanza. Wachezaji wengi hupokea kitu kulingana na walivyokisikia, kitu ambacho huwaathiri sana kiakili.

Na ikizingatia hatuna wataalamu wa saikolojia ndipo hapo huwa ni mwanzo wa kuwapoteza vijana wetu kutokana na kukosa mtu wa kumshauri baada ya kupokea kitu ambacho alikuwa hakitegemei katika maisha yake.

Hiki ndicho kilichomkuta Jonas Mkude. Alipitia kipindi kigumu sana, kipindi ambacho alikuwa hajajiandaa nacho.

Kilikuja ghafla na hakuwa na maandalizi yoyote ya kukipokea hicho kitu. Hali ambayo ilimfanya ayumbe kuanzia ndani mpaka nje ya uwanja.

Alipoteza nafasi yake ndani ya kikosi cha Simba. Akawa anaanzia benchi!, na hii ni kwa sababu hakuwa amejiandaa na tukio la yeye kupokea unahodha wa timu ya Simba.

Ilimchukua muda mrefu sana kurudi kwenye hali yake ya kawaida. Leo hii katulia na hana kitu chochote cha kulalamika kwa sababu anafanya kazi yake mara mbili tofauti na alipokuwa nahodha.

Hana majukumu mengi tena uwanjani kwa sasa, jukumu lake alilo nalo ni kumiliki dimba la katikati tu.

Hawazi kuwa yeye ni kiongozi wa timu, ameshakubali kuongozwa tayari. Anatii amri ya kiongozi na yeye anaufanya mpira utii amri katika miguu yake kwa kuhakikisha anamiliki eneo la kati vizuri kuliko kawaida.

Ilimchukua muda mrefu kurudi katika kiwango chake cha awali, na hili jambo linaweza kuwa somo kubwa sana kwa vijana wetu wa sasa.

Wengi huanguka kila wanapokuwa wanakutana na nyakati ngumu katika maisha yao ya mpira. Huonekana hawafai na kuonekana kama wametengwa na wakati mwingine hujiona hawafai kabisa katika timu yao.

Na huu ndiyo huwa mwanzo wa kupoteza vipaji vingi ambavyo huonekana vina faida kubwa katika soka letu. Leo hii tungempoteza Jonas Mkude lakini tushukuru Mungu amerudi kwenye mstari ulio na faida.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

TUNAUFICHA UKWELI KWENYE MAMBO YA UCHAWI

Tanzania Sports

MAMBO KUMI YANAYOISIBU MANCHESTER UNITED