LIGI KUU inatarajiwa kuanza kunguruma mwezi ujao. Wakati wapenzi na mashabiki wa mpira wanaendelea kushuhudia namna klabu za Ligi zinavyofanya kazi ya kutafuta vipaji vya soka. Kipindi hiki timu mbalimbali zinajitahidi kusajili wachezaji wazuri wa Ligi kuu ili kuimarisha vikosi vyao.
Simba ni miongoni mwa tim ambazo zimetema wachezaji ambao walitegemewa kubaki kwenye klabu hiyo. Simba wamelazimika kuongeza nguvu katika klabu yao ili kuhakikisha wanapata magoli ya kutosha kwenye mashindano ya CAF.
Tathmini ya TANZANIASPORTS inaonesha kuwa klabu ya Simba ilikuwa na uhaba wa magoli katika mashindano ya CAF licha ya kufanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho. Katika kikosi cha Simba safu ya ushambuliaji ilikuwa na washambuliaji wakuu wawili, Lionel Ateba na Stephn Mukwala, na pembeni yao kulikuwa na mawinga Joshua Mutale na Kibu Dennis huku kiungo mshambuliaji mkuu alikuwa Jean Ahoua.
Hata hivyo katika mashindano ya CAF, Simba ilikuwa inapigania ubingwa ikiwa katika shinikizo mara kadhaa kutokana na uhaba wa magoli kutoka kwa washambuliaji wao. Si Lionel Ateba wala Mukwala ambaye ameweza kufunga magoli angalau 20 kwa msimu. Katika Ligi Kuu hawajafikisha magoli 20. Kwenye mashindano ya CAF pia hawajafikisha magoli 10. Hii maana ya safu ya ushambuliaji ya Simba ilihitaji magoli ya kutosha kumaliza mechi kadhaa.
Kwa mfano katika mechi mbalimbali washambuliaji wake walikosa utulivu, na walikuwa wanapoteza nafasi mbalimbali. Matukio ya kufunga magoli yao bado yalikuwa na changamoto kwani hawakuwa katika kiwnago cha kuritdhisha na ambacho kinaweza kuipeleka mbali zaidi Simba kwa msimu huu. Kufika fainali ya Kombe la Shirikisho ni mafanikio kwao na wanapasawa kupewa heko.
Lakini utendaji wa kazi katika safu ya ushambuliaji ya Simba haukuwa ule wenye uchu wa kupachyika mabao mengi. Ni sababu Simba kufikisha mabao 2 au 3 kwenye mashindano ya CAF ilikuwa kwa mbinde. Katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho safu ya ushambuliaji ilikosa mabao mengi sana kiasi kwamba iliwapa ahueni wapinzani waop RS Berkane.
Je nini wanachotakiwa kufanya Simba?
Usajili wa Suleiman Mwalimu ‘Gomez’ huenda ukawa sehemu ya suluhisho na kumpandisha thamani nyota huyo. Simba wapo mbele katika ubora wa CAF kuliko Wydad. Kwa maana hiyo Suleiman Mwalimu anapotua msimbazi anapanda daraja kwa kujiunga na timu kubwa akitokea nchini Morocco.
Katika hatua hii ni vyema mashabiki wa soka nchini wakajikumbusha kuwa Wydad Casablanca chini ya Rhulani Mokwema ndiyo iliyomsajili nyota huyo. Ni ujumbe kuwa viongozi na benchi la ufundi la Wydad lilikuwa limeona kitu cha ziada kutoka kwa mshambuliaji huyo. Upatikanaji wake katika kikosi cha Simba utaleta mchango na ushindani katika safu hiyo.
Simba wanahitaji kufunga mabao kutosha kwenye mashindano ya CAF. Si mashindano ya CAF peke yake bali hata kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania wanatakiwa kuwa na uhakika wa kupachika mabao mengi.
Mshambuliaji anayesajiliwa Simba anatakiwa kuwa na uhakikwa kupachika mabao 20 ya Ligi Kuu huku kwenye mashindano ya CAF akiwa na deni ya kuhakikisha miguu yake inafunga si chini ya mabao 15. Hadhi ya Simba inawalazimisha kuwa na kiwango cha juu cha mshambuliaji ambaye atakuwa na uwezo wa kutikisa nyavu za timu pinzani. Hadhi waliyonayo Simba inawafanya wawe kwenye darubini kutoka kwa wapinzani wao wengi kwahiyo wanahitaji wachezaji wenye hadhi na wenye uchu na maarifa zaidi katika kupachika mabao.
Suleman Mwalimu anakuwa ingizo jipya, lakini anahitaji benchi la ufundi limwandalie mpango maalum wa kufikia malengo ya klabu ya Simba. Endapo Simba watafunga mabao mengi kwenye mashindano ya CAF maana yake wanajiandalia nafasi nzuri ya kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita. Ni wakati wa Suleman Mwalimu kuthibitisha thamani yake kama walivyofanya akina Joseph Kaniki, Mohammed Hussein na wengineo waliopata kutikisa katika vilabu vya nchini, kwani kwa ujio wa wachezaji wa kigeni umechangia ushindani mkali na kuamsha maarifa ya wachezaji wazawa. Kwahiyo Suleiman Mwalimu akitumika ipasavyo anaweza kuimarisha safa ya ushambuliaji ya Simba.

