SIMBA wamecheza mchezo wao wa 17 kwenye Ligi Kuu siku ya Alhamis ya Februari 6 dhidi ya Fountain Gate Fc. Katika mchezo huo Simba walilazimishwa sare ya 1-1 na hivyo kushindwa kukwea kileleni mwa Ligi hiyo. Yanga wanaongoza Ligi Kuu wakiwa na alama 45 kutokana na Michezo 17 waliyocheza.
Katika mchezo huo, kuliibuka tukio ambalo limewasononesha mashabiki wa Simba na kuwachekesha watani wao Yanga. Winga mwenye kasi Ladaki Chasambi ameingia katika mjadala mzito kutokana na matokeo waliyopata Simba katika mchezo huo. TANZANIA SPORTS inakuletea uchambuzi Makini juu ya tukio lenyewe na namna ambavyo mashabiki wa Simba wanapaswa kuelewa kuwa matukio kama hayo si mageni lakini hutokea na ndiyo sababu huitwa “Siku Mbaya kazini”.
FOUNTAIN GATE WAPEWE MAUA
Kuizuia Simba yenye Stephen Mukwala na Lionel Ateba kutopachika mabao ya kutosha ni dhahiri wanastahili sifa. Simba walikuwa wanatafuta alama tatu ili kufikisha 46, lakini sare hiyo imewabakiza katika alama 44. Wamezidiwa alama tatu na Yanga. Kiuchezaji Fountain Gate wanajipanga vyema linapokuja suala la kutawama mchezo. Sehemu ya kiungo kulikuwa na wachezaji watano ambao waligawana majukumu; wawili walianza kukabia juu (Highline) na hivyo kuwazuia mabeki wa Simba wenye jukumu la kuandaa shambulizi (build up). Kadiri Simba walivyokuwa wanapigiana pasi katika eneo lao la 18 ndivyo waliwavuta Fountain Gate lakini wapinzani hao walikuwa mahiri katika kulinda lango lao. Mabeki wa Simba walivyoanzisha mpira kwa Nia ya kupanda mbele, walijikuta wanakabiliana na wachezaji watatu, kisha eneo la kiungo la Fountain Gate likawa limebakiza wawili kati ya watano. Katika mfumo huu mara nyingi timu pinzani inasubiriwa kufanya makosa ili iiadhibiwe. Katika mbinu naweza kukumbusha namna Manchester City walivyochapwa bao la kwanza na Arsenal ambalo lilifungwa na Martin Odegaard. Namna Man City walovyopoteza mpira ule ndivyo Arsenal walivyoutamani ili kupachika bao. Na hakika bao likaptikana. Kwa kuangalia namna pasi za skwea zinazopigwa eneo hilo, lazima wapinzani makini wataongeza shinikizo na kuwalazimisha wafanye makosa. Kosa likatokea.
WATANO DHIDI YA WANNE
Katika mstari wa katikati ya dimba kama nilivyosema awali wachezaji wa Fountain Gate walikuwa watano, wenye majukumu tofauti. Wawili walikwenda mbele ya mabeki wa Simba kama chambo, huku watatu wakisogea taratibu kuzuia mipango ya vijana wa Fadlu Davids. Katika mpango huu wachezaji wa Simba wanne walikuwa wanakabiliana na wachezaji watano wa timu ya Fountain Gate. Nyuma ya wachezaji watatu wa Fountain Gate kulikuwa na kiungo mmoja wa ulinzi, huku walinzi wanne katika uzuiaji kwani kiungo mmoja alirejea kuungana nao katika ulinzi na kuhakikisha lango lao halitikiswi. Katika mtindo huu washambuliaji wa Simba hawakupata huduma ya wapishi wa mabao kwa sababu njia zao zilikabiliwa na wachezaji wa Fountain Gate.
Licha ya nafasi kadhaa walizozipata na kukosa bado hawakuwa hodari dhidi ya mbinu ya 3-5-2. Kwa mfumo huo mpira ulikuwa unachezwa katikati ya dimba zaidi. Ushahidi upo katika mabao waliyofungana ambayo yametokana na makosa binafsi ya wachezaji. Bao walilopata Simba lilitokana na faulo lakini namna ilovyopigwa ndivyo unahitaji kuelewa kazi ya makocha ni pamoja na kuwajengea utayari wa kunusa hatari. Makosa yao yakawaadhibu.
BAO LA CHASAMBI
Winga Ladaki Chasambi anaweza kulaumiwa kwa kosa alilofanya na kuwapatia bao Fountain Gate. Je nini kilichotokea katika tukio hilo? Ni makosa ya Chasambi pekee au safu ya ulinzi? Katika kulichambua tukio hilo tuanze kuangalia muundo wa wachezaji wa Fountain Gate na wale wa Simba.
Chasambi anaweza kulaumiwa kwa sababu alipiga kwa nguvu pasi yake kwenda kwa golikipa (alizotumia kupiga mpira). Lakini ukitazama kwa jicho la kiufundi;
Mosi, kulikuwa na wachezaji watano wa timu pinzani. Wachezaji hao waligawa katika makundi mawili. Wachezaji wawili walitangulia mbele kuwakabilia mabeki wa Simba. Wakati wachezaji watatu waliondoka kwenye mstari katikati ya uwanja kwenda kuungana na wale wawili. Baada hao watatu kuwasili, mmoja wa mbele aeliekea eneo la beki wa kati wa Simba, kisha mwingine akaelekea upande wa kulia kwake (kushoto kwa Simba). Kisha watatu wakawa wanasubiri namna Simba watakavyoanzisha pasi zao (build up). Hilo tayari lilikuwa shinikizo.
Pili, kati ya wachezaji hao, ni wanne walikuwa wanazuia Simba huku chezaji mmoja akiwa katika “free role”, na ambaye angeenda kwa golikipa wa Simba, Moussa Camara.
Tatu, nyuma ya Chasambi kulikuwa na mchezaji mwingine ambaye alikuwa sehemu ya mabeki mwenye jukumu la kusubiri kama mpira ungepigwa eneo hilo.
Hata hivyo ukitazama muundo wa pasi za Simba, golikipa alianzisha vizuri kwenda kushoto, na kisha ukapelekwa kwa Chasambi. Katika mazingira yale Chasambi alikuwa na machaguo mawili; kupiga mpira kwa kuukunja uende katikati-mbele au kurudisha kwa golikipa ili kuanzisha upya mipango.
Chasambi alifikia hitimisho ule mpira uende kwa golikipa wake katika pasi inayomfikia mlengwa bila kuathiriwa na nguvu zake. Lengo lilikuwa Simba ianzishe “move” yake upya kutokea nyuma.
Lakini je nafasi ya golikipa katika mbinu hiyo iko wapi? Unaweza kutazama namna alivyojipanga utaona alivuka mstari wa eneo lake, hivyo alipaswa kurudi nyuma kidogo (kunusa hatari). Kwa msingi huo, golikipa baada ya kuona namna wapinzani walivyo na idadi ya mabeki wake, Kwa kawaida alitakiwa kusubiri pasi akiwa ndani ya eneo la 18 pembeni mwake (upande wa kushoto kwake). Katika hili golikipa hakujipanga vizuri sababu ya kuacha umbali uliosababisha mpira kumpita kirahisi. Laiti angekuwa eneo la 18 pembeni kushoto kwake maana yake mpira ule ungetua kifuani kwake na kutulizwa vyema.
Nini maana ya kurudisha mpira kwa Kipa? Chasambi alitaka “build up” ianze upya sababu wapinzani walishafunga njia ya mtu na mtu, na hata nafasi ya kupeleka pasi ili ifikiwe na Simba mwingine isingekuwa rahisi. Hivyo lilikuwa suala la kiufundi zaidi kuliko uamuzi mbaya. Katika makosa kama haya, Ladaki Chasambi anapaswa kusaidiwa kukua na kushauriwa aendeleze kipaji chake Kwa kucheza kwa utulivu. Anaweza pia kujifunza kwa makosa mfululizo ya beki wake Che Malone ambaye ameendelea kuaminiwa kwa sababu anaweza kubadilika na mchango wake ni Mkubwa. Hali kadhalika mchango wa Ladaki Chasambi ni mkubwa na bado kijana, anaweza kuendelezwa zaidi Kwa kumwambia “Tulia, cheza mpira”.
Comments
Loading…