*Tembo wake wawakanyaga Tunisia 3-0
*Togo chereko kwa kuwatungua Algeria
Ivory Coast wamekata tiketi ya kuingia robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa staili ya aina yake, baada ya kuwaadhibu Tunisia kwa mabao 3-0.
Tembo hao walianza vyema mchezo huo huku Tai wa Tunisia wakizubaa kwa karibu kipindi chote cha kwanza, hivyo kuonekana Ivory Coast wangepata ushindi mkubwa.
Hata hivyo, baada ya bao la kwanza la mshambuliaji wa Arsenal, Gervais Yao Kouassi ‘Gervinho’ katika dakika ya 21, Tembo walionekana kutokamia mabao zaidi.
Nyota wao wa kimataifa, Didier Drogba alianzia benchi, lakini muda mwingi alikuwa akiwapa wenzake maelekezo akiranda randa, na hata waliposhangilia bao kupita kiasi aliwaasa kurejea uwanjani kuchakarika.
Hawakupata bao jingine na kipindi cha pili Tunisia waliamka, kuwasakama na kutokea kosakosa nyingi, hadi dakika 10 za mwisho Ivory Coast waliporudi tena kwenye fomu, Drogba akiwa ameshaingia.
Alikuwa kiungo mahiri wa Manchester City, Yaya Toure aliyefunga bao zuri la pili dakika ya 87. Toure na Gervinho walifunga mabao kwenye mechi ya awali dhidi ya Togo kwenye mechi za kundi D.
Mchezai Didier Ya Konan aliyeingia kipindi cha pili alipachika bao la tatu na kuwahakikishia vijana wa kocha Sabri Lamouchi nafasi ya robo fainali, baada ya mwaka jana kupoteza tonge mdomoni mwa Zambia.
Gervinho amerejea kwenye kiwango kizuri kiuchezaji, tofauti na alipokuwa na Arsenal, ambapo washabiki kutaka aachwe benchi, kutolewa kwa mkopo au kuuzwa kwa klabu nyingine kwa kushindwa kuzifumania nyavu.
Ushindi huo wa Ivory Coast unatuma salamu kwa timu nyingine, ambapo wamechezesha nyota kama Lacina Traore wa Anzhi Makhachkala, Salomon Kalou wa Lille na Christian Koffi Ndri ‘Romaric’ wa Real Zaragoza.
Wengine ni Cheick Tiote wa Newcastle United, Emmanuel Ebou anayekipiga Galatasaray baada ya kutisha akiwa na Arsenal, Siaka Tiene wa Paris Saint-Germain wakati Kolo Toure wa Manchester City alikuwa benchi.
Nguzo yao nyingine muhimu ya ushindi wa Jumamosi hii alikuwa golikipa Boubacar Barry aliyedaka mipira mingi ya hatari, ikiwamo baadhi aliyookoa kwneye mstari wa goli.
Togo wamefufua matumaini ya kupata nafasi ya kucheza robo fainali, baada ya kuwafunga Algeria mabao 2-0. Kwa maana hiyo, safari ya Algeria imeishia jangwani, kwani katika mechi ya awali walifungwa bao 1-0 na Tunisia.
Togo walipata bao kupitia kwa mshambuliaji wa Tottenham Hotspurs, Emmanuel Adebayor aliyedhibiti mpira wa kichwa wa Moustapha Salifou na kumtungua golikipa Rais Mbolhi kutoka kona ya eneo lake.
Katika dakika 15 za mwisho, lilitokea jambo lisilo la kawaida, kwa jozi ya goli la Togo kuharibika kwa kupinda kiasi cha kuhitaji matengenezo na mpira kusimama kwa muda.
Jamaa aliyevaa suti aliitwa kuutengeneza, naye akaita wenzake, lakini hawakufanikiwa kusawazisha mambo, kisha wakaamua kuondoa jozi yote, ikadhaniwa walikwenda kuchukua jozi nyingine ya goli, lakini wakarejea mikono mitupu.
Hali hiyo haikuwafurahisha Algeria, lakini itabidi wajilaumu wenyewe, kwa sababu kiungo wao, Adlene Guedioura ndiye aliyeliharibu kwa kurukia na kupitiliza nyuma ya neti.
Hatimaye ‘mafundi’ walifanikiwa kutengeneza jozi hiyo ya goli baada ya kama dakika 15 hivi, na mpira kuanza tena, ambapo Algeria waligeuka kama waliomwagiwa maji.
Walipachikwa bao la pili na mchezaji aliyeingia kipindi cha pili, Dove Wome aliyekokota mpira tangu katikati ya uwanja, mabeki wakifunga tela hadi akafanikiwa kumfunga kirahisi golikipa Mbolhi.
Walipopata bao la pili, wachezaji wote 11, wale wa akiba na benchi la ufundi walikusanyika kushangilia, kuona vijana hao wa kcha Didier Six wanavuka kuingia hatua muhimu.
Matokeo hayo yalikuwa maumivu makubwa kwa Algeria, mabingwa wa 1990, walioingia kwenye mashindano wakiwa nafasi ya pili kwa ubora Afrika, kwa mujibu wa FIFA.
Togo na Tunisia zitakutana wiki ijayo katika mpambano utakaoamua wa kuungana na Ivory Coast kwenye robo fainali.
Kwa msimamo wa kundi hivi sasa, Ivory Coast wanaongoza wakifuatiwa na Togo kwa sababu wana pointi tatu na mabao matatu ya kufunga wakati Tunisia wana pointi tatu na bao moja. Uwiano wa mabao wa Togo ni +2 wakati wa Tunisia ni -2, hivyo hata suluhu au sare itawavusha Togo.
Jumapili itashuhudia timu za kundi A zikirejea dimbani, zote zikiwa na nafasi ya kusonga mbele. Cape Verde watawavaa Angola na Morocco watakwaana na wenyeji Afrika Kusini.
Comments
Loading…