*Arsenal wamchukua Sir Keswick kuwa mwenyekiti mpya
Maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya England (EPL) yanapamba moto, kwa klabu kuingiza wachezaji, makocha na viongozi wapya, na zamu hii ni Manchester City na Arsenal.
Wakati Arsenal wakimtangaza Sir Chips Keswick kuwa mwenyekiti mpya, kuchukua nafasi ya Peter Hill-Wood, hatimaye matajiri wa Etihad, Manchester City wamemtangaza rasmi Manuel Pellegrini kuwa kocha wao mpya.
Pellegrini ambaye kwa muda amekuwa akipiga danadana kuhusu safari yake ya kujiunga na City wanaomilikiwa na mabilionea wa Mashariki ya Kati, anachukua nafasi hiyo akiitwa ‘injinia’ au mhandisi, aliyekuwa akiongoza Malaga, klabu iliyokuwa ikiitwa ‘Manchester City ya Hispania’.
Raia huyo wa Chile anachukua nafasi ya Roberto Mancini aliyefutwa kazi, baada ya kushindwa kuwaongoza City kutetea taji walilotwaa msimu wa 2011/12 na badala yake akaacha majirani zao wa Manchester City waliowapokonya kulirejesha.
Pellegrini (59) anayezungumza Kiingereza kizuri tofauti na Mancini, ana kazi nzito ya kuisuka upya City na kuwaridhisha wamiliki wanaotaka kuona mataji yakimiminika na kuzima kabisa upinzani wa United, hasa wakati huu ambapo Sir Alex Ferguson amestaafu na nafasi yake kuchukuliwa na David Moyes aliyekuwa Everton.
City wanaonekana kujisuka upya, kwani mtendaji mkuu ni Ferran Soriano na Mkurugenzi wa Soka, Txiki Begiristainwote wakiwa na asili ya klabu kubwa ya Hispania na maarufu duniani ya Barcelona, na ilikuwa dhahiri wangemtafuta kocha ama Mhispania au aliyekaa huko, kama Pellegrini.
Baada ya kufanya kazi nchini mwake kwa muda mfupi, Pellegrini alikwenda Ulaya na kujiunga na Villarreal (2004-2009 na katika mechi 259 alishinda 123 sare 72 na kupoteza 64. Alijiunga Real Madrid (2009-2010) ambapo katika michezo 48 alishinda 36 sare mitano na kushindwa saba. Baada ya hapo aliingia Malaga 2010 alikoshinda mechi 52, sare 30 na kupoteza 46 kati ya jumla ya michezo 128.
Ama kwa upande wa Arsenal, uteuzi wa mwenyekiti mpya wa bodi atakayefanya kazi na Kocha Arsene Wenger katika kutafuta makombe kuanzia sasa, umefanyika kwa sababu ya afya mbaya ya Hill-Wood ambaye ameamua kupumzika.
Sir Chips Keswick aliyetunukiwa tuzo na Malkia Elizabeth II, anasema Arsenal ni moja ya klabu kubwa kabisa duniani, na atafanya kila awezalo kuihakikishia mafanikio. Hill-Wood anasema amefikia uamuzi huo katika mazingira magumu, kwani alitaka bado kuitumikia klabu.
Comments
Loading…