in , , ,

Injinia Hersi Umeibomoa Mwenyewe Yanga

Ukilizungumzia soka la Tanzania basi huwezi kuacha kutaja klabu ya Yanga kwani ni moja ya timu maarufu hapa nchini Tanzania. Katika siku za hivi karibuni, licha ya mafanikio ya awali ambayo wamekua wakiyapata ni wazi kuwa matokeo yasiyoridhisha katika mashindano ya kimataifa haswa Ligi ya Mabingwa Afrika yamezua maswali na mijadala mbalimbali katika mitandao ya kijamii kuhusu mwelekeo wa klabu hii kutoka mitaa ya Twiga na Jangwani pale Kariakoo. Wakati lawama mara nyingi hutupwa kwa wachezaji na benchi la ufundi, ukweli ni kwamba chanzo cha changamoto hizi ni uongozi wa klabu.

Wanasema kuwa kiongozi mzuri anapaswa kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi yanayojali maslahi ya muda mrefu ya klabu. Hata hivyo, kwa namna ambavyo matokeo yamekua hivi karibuni kwa klabu ya Yanga huwezi kuwalaumu wachezaji wala kocha mpya ambaye amepewa timu kipindi kama hiki bali unatakiwa kulaumiwa uongozi.

Ninaamini kuwa uongozi ulifanya maamuzi ya haraka ambayo yameathiri utendaji wa timu haswa katika kipindi hiki ambacho klabu ilikua inaingia katika mashindano makubwa ya kimataifa. Mfano hai ambao nadhani hakuna ambaye atanibishia ni namna ambavyo  alivyoondoshwa Kocha Mkuu Miguel Gamondi

Kufukuzwa kwa kocha Miguel Gamondi ni hatua iliyozua sintofahamu kubwa hasa kwa kuwa alionekana kuwa na uwezo wa kuimarisha timu kuelekea mashindano ya kimataifa kama Ligi ya Mabingwa Afrika lakini pia tayari alikaa na wachezaji kwa muda mrefu na walikua tayari washazoea mifumo yake. Badala ya kumwacha aendelee na kazi yake, uongozi ulifanya maamuzi ya haraka ambayo yameathiri muunganiko wa kikosi.

Yanga SC inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa mkakati wa muda mrefu wa maendeleo. Badala ya kujenga timu imara yenye wachezaji na benchi la ufundi wanaoelewana, uongozi umeonekana kuwa na mawazo ya muda mfupi yanayoongozwa zaidi na shinikizo la mashabiki na matokeo ya haraka.

Katika ligi kama Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo inahitaji utulivu na maandalizi makini, ukosefu wa mpango wa muda mrefu umekuwa ukichangia matokeo mabaya. Uongozi wa Yanga haujaweza kuonyesha uvumilivu unaohitajika kujenga msingi imara wa ushindani wa kimataifa haswa kwa namna ambavyo wamefanya usajili wao msimu huu kwani wachezaji ambao waliwasajili ni kama ilikua kwa ajili ya kuwafurahisha Zaidi mashabiki na kuwamuiza wapinzani wao wa karibu kwenye Ligi ambao ni Simba pamoja na Azam Fc.

Katika mazingira ya ushindani mkubwa, wachezaji wanahitaji uongozi imara unaowapa msaada wa kiufundi na kisaikolojia. Kukosekana kwa mazingira haya kumesababisha wachezaji kukosa uthabiti uwanjani, hali inayoathiri matokeo ya timu.

Pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Yanga SC, ni wazi kwamba rasilimali hizi hazitumiki ipasavyo. Badala ya kuwekeza katika vitu vya msingi kama mafunzo ya kiufundi, miundombinu bora, na usajili wa wachezaji sahihi, fedha nyingi zimetumika kwa maamuzi yasiyo na tija ya moja kwa moja kama kulipa madeni ya wachezaji ambao iliwasajili na kuwavunjia mikataba yao.

Kwa mfano, usajili wa wachezaji wa gharama kubwa bila kuwapa muda wa kuzoea mfumo wa timu ni tatizo sugu linaloharibu maelewano ndani ya kikosi. Na katika jambo hili sioni Yanga kama wataendelea kuwa na mshambuliaji Prince Dube.

Kwa hali ilivyo, lawama za kufanya vibaya kwa Yanga zinapaswa kuelekezwa kwa uongozi. Maamuzi yasiyopimwa, ukosefu wa mkakati wa muda mrefu, na kushindwa kutumia rasilimali vizuri ni mambo yanayodhoofisha juhudi za klabu.

Mashabiki wa Yanga wanahitaji kuona viongozi wao wakichukua hatua za dhati kurekebisha hali hii, badala ya kuendelea kutoa visingizio kwa matokeo mabaya lakini pia uongozi unapaswa kubadili mbinu zake, kuwekeza katika mipango ya muda mrefu, na kuhakikisha kwamba maamuzi yote yanazingatia maslahi ya timu. Bila mabadiliko haya, ni vigumu kuona Yanga ikirejea kileleni na kufikia ndoto zake za kuwa timu bora katika bara la Afrika.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Taifa Stars

Safari ya Tanzania katika mapinduzi ya michezo

Tanzania Sports

Hili la waamuzi AFCON litupiwe macho