Kocha wa Timu ya Taifa, Hemed Suleiman ameita wachezaji 23 kwa ajili ya maandalizi ya kucheza mechi za kufuzu fainali za Kombe la Dunia. Katika kikosi hiki amewarejesha wachezaji 13 waliokuwa kwenye kikosi cha CHAN kilichoishia hatua ya robo fainali ya mashindano hayo. Pia ameita wachezaji kadhaa ambao aliwaacha kwenye kikosi cha CHAN pamoja na wale wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya na kwingineko. TANZANIASPORTS inafanya uchambuzi juu ya kikosi hiki na kuibua swali la msingi uti wa mgongo wa kikosi cha benchi la ufundi la Taifa Stars ni upi?
Mchango wa wachezaji wa kulipwa
Kulingana na taribu za mashindano ya CHAN, wachezaji wanaotakiwa kushiriki ni wale wa ligi za ndani. Kanuni hii inaeleweka kwa usahihi. Ujio wa wachezaji wanaocheza soka la kulipwa unakuwa chachu kwenye kikosi na kuongeza nguvu zaidi. Wachezaji wanaopcheza soka la kulipwa walioitwa ni wanne pekee. Wachezaji hao ni nahodha Mbwana Samatta (Ufaransa), Simon Msuva (Iraq), Charles M’mombwa (Malta) na Novatus Dismas Miroshi (Uturuki). Katika kikosi hiki wachezaji wanaofanya vizuri kama Kelvin John ameachwa na kocha hajaeleza sababu za kutoitwa kikosini.
Ben Starkle ni miongoni mwa wachezaji waliotumika kama nguzo ya kujenga kikosi kipya kuelekea mashindano mbalimbali ametupwa nje, sambamba na Kwesi Kawawa na nyota wengine. Kuitwa wachezaji wanaosakata soka barani Ulaya na kwingineko kunatoa fursa ya kuongeza wigo wa mbinu kwa mwalimu , wachezaji wengine na kikosi kwa ujumla wake. wachezaji wa ligi ya ndani na wale wanaocheza nje wanakabiliana na wapinzani tofauti na hivyo wanaleta uzoefu na mchango tofauti.
Hata hivyo kocha wa Hemed Suleiman amenekana kuvunja nguzo hii bila kutoa maelezo sababu ya kuwaacha baadhi ya nyota wenye sifa ya kuchezea kikosi chake. Hii ina maana hata kwa wachezaji wa wanaosakata soka nje bado hakuna nguvzo ambayo inaweza kuimarisha kikosi kwenye mashindano mbalimbali.
Sakata la Kelvin John
Baada ya kumalizika mashindano ya CHAN, kocha wa Taifa Stars alisikika akisema kuna uhaba wa washambuliaji katika kikosi chake na zaidi hata kwenye Ligi yetu. Pia katika mazungumzo yake na vyombo vya habari kutoa tathmini baada ya CHAN, kocha huyo alisema tatizo lingine ni umaliziaji. Sasa katika kikosi cha CHAN unaweza kusema hapakuwa na wamaliziaji wazuri, na kwa hiyo angeweza kufanya mabadiliko kwenye kikosi cha kucheza mechi za kufuzu kombe la Dunia.
Miongoni mwa washambuliaji ambao wanafanya vizuri kutoka Tanzania ni Kelvin John. Nyota huyu anasakata soka hapa Ulaya, na ameoneshwa kuanza vizuri msimu huu ambapo video mbalimbali zinaonesha jinsi mashabiki wa klabu yake walivyopagawa. lakini kwa kocha wa Taifa Stars anayelalamikia uhawa wa washambuliaji na umaliziaji amethubutu kukiacha kipaji hiki ambacho kinaweza kutoa mchango mkubwa. Hii inaleta jibu kuwa kocha wa Tanzania hana nguzo kwa wachezaji nje ambayo ametengeneza na kuwa uti wa mgongo wake, liwake jua ama lisiwake.
Kuitwa Yahya Zaid
Kwenye mashindano ya CHAN, nyota huyu hakuitwa. Kuitwa sasa kunadhihirisha kuwa benchi la ufundi la Taisfa Stars lilifanya makosa kuunda kikosi chake. Madhara ya makosa hayo ni kutumia beki w akushoto kama winga. Pascal Mshindo hawezi kuwa winga bora kumzidi Yahya Zaid, na kama mwalimu alihitaji wachezaji wa nafasi hiyo angeweza kuimarisha kwa kuhakikisha Yahya anaitwa. Badala yake kocha alimtegemea Iddy Nado, huku mabadiliko yake yakiwa yanatabirika, huku Yahya akiwa ametulia tu pale Azam.
Changamoto ya kocha wa Hemed Suleiman, muundo wa kikosi chake unawanyima nafasi mawwinga wa ziada. Mfano katika kikosi cha sasa ameita mawinga watatu; Simon Msuva, Iddy Nado, Yahya Zaid na Charles M’mombwa, hii inaonesha inawezekana kocha huyo angeita mawinga wawili kwenye mashindano ya CHAN. Hapa pia hana nguzo wala uti wa mgongo kikosini.
Eneo la kiungo mkabaji
Kwenye mashindano ya CHAN, wachezaji watatu tofauti walitumika kucheza namba 6 ambayo ilikuwa inachezwa na mchezaji mmoja, Yusuf Kagoma. Katika kikosi cha kucheza mechi za kufuzu fainali za kombe la dunia, kocha amewaita Yusuf Kagoma na Novatus Dismas Miroshi. Pengine kocha wa Taifa Stars akumbushwe makosa yaliyotokea kwenye mechi dhidi ya Morocco hatua ya robo fainali ambapo kitendo cha kumtoa Yusuf Kagoma kiliwapa uhuru wapinzani wao. Morocco walionekana kufurahishwa sana na uamuzi wa kumtoa uwanjani Yusuf Kagoma na kumrudisha nyuma Feisal Salum kama kiungo mkabaji.
Kitendo hiki kiliwapa sit u uhuru bali kujiamini zaidi kwani kikwazo chao cha kwanza kilikuwa kimeondolewa. Matokeo yake kwenye benchi la ufundi kocha wetu hakuwa na mbadala wa Yusuf Kagoma. Ingawaje Fei Toto si mgeni na anaweza kutumikia vyema nafasi ya Yusuf Kagoma lakini anakuwa na madhara zaidi pale anapopewa uhuru wa kuwashambuliaji wapinzani.
Kwenye mashindano ya CHAN mwalimu alijaribu kumtumia Abubakar Hamza kama kiungo mkabaji lakini alidumu uwanjani kwa dakika 33 tu. Je kocha Hemed Morocco hakuona matatizo haya hadi anarudia tena kwenye kikosi cha kufuzu fainali za kombe la dunia? Vilevile uamuzi wakumtema Pipino unaonesha kuwa mwalimu na benchi lake walifanya makosa ya kutomzingatia Edmund John na Wilson Nangu. Hapa pia hana nguzo wala uti wa mgongo wa eneo hili.


Comments
Loading…