Lwandamina jana alifunga hesabu iliyofunguliwa na Hans Van Der Pluijm.
Kitabu cha hesabu alichokabidhiwa na Hans Van Der Pluijm hakikuwa na
hesabu nyepesi, akili kubwa ya ziada ilihitajika ili kufanikiwa
kukokotoa hesabu hizi ngumu.
Ndani ƴya miaka mitatu wamefanikiwa kuchukua ubingwa wa ligi kuu mara
ya tatu mfululizo. Lakini katika misimu hiyo mitatu yote , msimu huu
ndiyo ulikuwa msimu ambao ulikuwa na changamoto kubwa sana kwa Yanga.
Ugumu mwingi wamepitia Yanga katika msimu huu ukilinganisha na misimu
miwili iliyopita. Pamoja na kwamba msimi huu walianza vizuri kwa
kufanikiwa kusajili baadhi ya wachezaji nyota kwa gharama kubwa kama
Obrey Chirwa lakini mambo yalianza kubadilika lakini Yanga walitembea
katika ugumu.
Kwa wachezaji kuondokewa na kocha ambaye walikuwa wameshamzoea kuishi
naye kwa muda mrefu tena akaondoka katikati ya msimu na kuletewa kocha
mwingine mpya na wao kuonekana wanaweza kufanya kazi na mtu yoyote
yule lilikuwa jambo ambalo lilionesha ukomavu kwa wachezaji wa timu ya
Yanga.
Ndani ya misimu mitatu iliyopita, ni msimu huu pekee ambao neno ukata
limehubiriwa ndani ya kikosi cha Yanga. Kiuchumi Yanga haikuwa vizuri
ukilinganisha na misimu miwili iliyopita. Hali hii ilisababisha
wachezaji kutopata mishahara kwa wakati lakini wachezaji pamoja na
benchi zima la ufundi lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kutembea katika
ugumu huu na kufanikiwa kuchukua ubingwa .
Michuano ya kimataifa msimu huu , Ushiriki wa Yanga ulikuwa siyo mzuri
kwani timu haikufanya vizuri ukilinganisha na msimu uliopita ambapo
ilifanikiwa kufika hatua ya robo fainali ya kombe la shirikisho barani
Afrika. Na hii ilisababishwa kwa kiasi kikubwa na hali mbaya ya uchumi
iliyokuwa kwenye klabu ya Yanga.
Msimu huu wamefanikiwa tena kupata ticket tena ya kushiriki michuano
ya kimataifa baada ya kuchukua ubingwa.
Ubingwa huu ambao wamechukua , wanatakiwa wasibweteke sana kwa kiasi
kikubwa, kitu ambacho wanatakiwa wakifanye ni wao kukaa chini na
kuanza kupanga mipango mizuri ambayo itawasaidia kufanya vizuri kwenye
michuano ya kimataifa msimu ujao.
Uzuri kuna neema imewashukia baada ya kupata udhamini wa Sport pesa
hali itakayowasaidia kupunguza makali katika uendeshaji wa timu.
Ni wakati sahihi kwao wao kukaa na benchi la ufundi vizuri na kuchukua
tathimini ya kiufundi zaidi ili wajue ni aina gani ya wachezaji ambao
watahitajika katika kikosi cha Yanga ili wafike mbali.
Kipindi hiki Mascouts wa Yanga wanatakiwa kutumika vizuri kuwaleta
wachezaji ambao ni hitaji la kocha na siyo hitaji la viongozi.
Ule wakati wa kumsajili mchezaji fulani kutokana na matakwa ya
kiongozi fulani bila kufuata ushauri wa kiufundi kutoka kwa kocha
umeshapita. Ni wakati wa kufanya sajili za kiufundi na siyo za
kisiasa. Ni vyema muda huu wakae na kujiuliza ni wapi walianguka msimu huu
kwenye michuano ya kimataifa ili msimu ujao uwe kama msimu uliopita
kwao.
Wasiruhusu kubweteka na ubingwa huu hata kidogo, cha muhimu ni wao
kutafakari kwa umakini ni kwa njia gani watakuwa imara kwenye michuano
ijayo ya kimataifa.