in ,

HONGERA SERENGETI BOYS, VITA BADO MBICHI..

Taa za furaha ziliwaka mioyoni mwetu , nyuso zetu zilitengenezwa na
tabasamu ambalo lilitosha kuelezea furaha ya ushindi wa timu ya taifa
ya vijana iliyochini ya umri wa miaka 17 yani serengeti boys.

Tafasiri halisi na nzuri kuhusu furaha ambayo Watanzania walikuwa nayo
baada ya kupata ushindi dhidi ya timu ya taifa ya vijana ya chini ya
umri wa miaka 17 ni kwamba Watanzania walikuwa wana uhaba wa furaha
katika mpira wa miguu na wanahitaji tiba ya huu ugonjwa.

Daktari sahihi wa huu ugonjwa ameshaonekana na juhudi anazofanya
kwenye matibabu ya ugonjwa wetu zinatia moyo sana na wengi tunaomba na
kuamini kuwa tunaelekea kupata furaha ya kudumu.

Ni ngumu kutokuamini kuwa ndani ya kikosi cha Serengeti boys hakuna
furaha ya kudumu , goli zuri la Yohana Mkomola linatosha kutuaminisha
kuwa mguu wake uliletwa kwa ajili ya kufunga magoli kwa ajili ya
furaha yetu.

Ni matamanio ya wengi wetu kwa Yohana Mkomola kufuata nyayo za kina
Mbwana Samatta pamoja na Farid Musa hii ni kwa sababu ya uwezo wake
mkubwa wa kufunga unaochangiwa na yeye kuwa mtulivu na kujua sehemu
sahihi ya kujipanga akiwa katika lango la adui.

Unaona nini ukimwangalia Kababange ? Uwezo wake wa kukaba na
kupandisha mashambulizi ya timu na kurudi haraka kuzuia mashambulizi
pindi inaposhambuliwa hivi vyote vinatosha kukuonesha kuwa ndani ya
Kakabange kuna beki wa kushoto mkubwa sana ambaye ana uwezo wa kucheza
vizuri hata katika mazingira ya soka la kisasa, kwani pamoja na uwezo
wa kucheza beki wa kushoto pia anauwezo wa kucheza kama Wingback
katika mfumo wa kutumia mabeki watatu.

Haikuwa bahati, au hawakukosea kumpa mchezaji bora wa mechi Dickson
Job.Uwezo wake mkubwa uwanjani ulikuwa na ushawishi mkubwa wa kuvikwa
taji la mfalme wa mechi dhidi ya Angola.

Hii yote inaonesha timu yetu imejaza vipaji ambavyo vina uwezo mkubwa
na vinatoa nafasi kubwa ya timu yetu kufika sehemu kubwa.

Muunganiko wa timu katika maeneo makuu matatu ya uwanja, yani eneo la
ulinzi, kiungo na ushambuliaji linaonesha wazi kuwa timu hii imeundwa
kwa mtindo wa kila mchezaji kutimiza majukumu yake kwa kiwango
kikubwa.

Vipaji binafsi ni vingi na vinaonekana , lakini jambo kubwa
lililofanywa na benchi la ufundi ni kuunganisha vipaji hivi vilivyopo
kwenye timu na kuifanya timu icheze kitimu zaidi bila kumzunguka
mchezaji mmoja kwa kiwango kikubwa na hii ndiyo sifa kubwa ya timu ya
ushindi.

Timu imejengwa kiushindani na hii imejidhihirisha kwenye mechi mbili
za kundi B, ya kwanza dhidi ya bingwa mtetezi Mali na hii ya Angola.

Matokeo waliyoyapata ni mazuri sana ila yasiwafanye wasahau lipi
jukumu walilonalo kwa Watanzania. Hatima ya furaha ya Watanzania kwa
sasa iko katika mikono yao.

Viganja vyao ndivyo vimebeba hatima ya kutengeneza tabasamu la
Watanzania. Furaha ya muda mrefu itakuwa katika mikono yao ambayo
tumeiamini ni salama kwetu.

Ni wakati kwao kufuta kumbukumbu ya matokeo ya mechi zilizopita katika
akili zao na kuweka picha ya kwamba wanadeni kubwa la kuwapa ushindi
Watanzania.

Ni muda sahihi kwao kutamani medali za kombe la Afcon kwa vijana wa
umri chini ya miaka 17 kwa sababu medali hizi zitasaidia kunogesha
utamu wa soga na wajukuu zao pindi watakapozeeka.

Matamanio chanya ya kufika India kushiriki kombe la dunia la vijana
waliochini ya umri wa miaka 17 yawajae.

Roho ya upiganaji, upambanaji na ufiaji wa nchi iwe ndani yao. Matokeo
mazuri waliyoyapata yasiwe chanzo kwao kushusha morali kwa sababu ya
kubweteka na matokeo haya.

Vita bado mbichi hatujajihakikishia ushindi mbele ya wapiganaji wenzetu.

Silaha zetu zihusike kwa kiasi kikubwa katika vita hii.

Ni wakati sahihi kwa wachezaji kukumbuka jukwaani kuna mawakala na
mascouts wengi.

Ukiachana na kuipigania nchi yetu, wachezaji wanatakiwa wajue
wanapigania maisha yao. Macho ya mawakala na mascouts mbalimbali
waliomiminika katika viwanja vya Gabon yatashawishika kwa ubora
utakaooneshwa na wachezaji wetu, ndiyo maana nawakumbusha mwisho wa
vita haujafika kwani vita ndiyo inaanza wanatakiwa wajidhatiti zaidi.

Kila la heri jeshi la furaha la Tanzania, jasho lenu ni damu tosha ya
kutengeneza furaha yetu.
[email protected]

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

SportPesa Tanzania Welcomes Dar Giants Yanga SC To Its Family

Tanzania Sports

JIJI LINA MSINGI WA MAWE, MUNGU KAWAPA MBAO KWA AJILI YA PAA LENU