Nimekumbuka kipindi ambacho Jurgen Klopp alipokuja Liverpool. Liverpool ilikuwa timu ya kuunga unga.
Haikuwa timu yenye ushindani ambao unaweza kujivunia kuwa hii ni timu bora. Hilo Jurgen Klopp aliliiona. Ndiyo maana aliomba muda wa miaka 3 kutengeneza timu anayoiona.
Hakuamini kupitia timu aliyoikuta kama inaweza kumpa mafanikio makubwa ndani ya uwanja. Mafanikio ambayo mashabiki wengi wa Liverpool walikuwa wanayataka.
Na kibaya zaidi mashabiki wa Liverpool wanawaza kubeba ligi kuu ya England. Miaka 28 imepita bila wao kupata kikombe hiki.
Wana kiu sana ya kikombe hiki. Wana njaa sana na kikombe hiki kwa sababu hajakipata kwa muda mrefu ndiyo maana wanashauku kubwa.
Jurgen Klopp hakutaka kuingia kwenye mtego wa kuwaambia kuwa anaweza kuwapa kikombe ndani ya muda mfupi kwa sababu tu hakuwa na timu hiyo.
Hata wapinzani wake aliowakuta kwenye ligi kuu ya England walikuwa na vikosi imara na bora kuzidi yeye na ndiyo maana alisita kabisa kuwaahidi kuwapa kikombe ndani ya muda mfupi.
Walimwelewa, na wakamwahidi watamvulimia ndani ya miaka mitatu atengeneze timu ambayo anaiona ni bora kwake.
Timu ambayo ingekuwa na uwezo mkubwa wa kubeba kombe la ligi kuu ya England. Timu ambayo ingeleta ushindani mkubwa kwenye michuano mingine.
Mashabiki walikuwa naye bega kwa bega. Hata alipokuwa anapoteza mechi yoyote walimpa nguvu na kumtia moyo.
Yote haya ni kwa sababu walikuwa wanajua wapo kwenye kipindi cha mpito. Kipindi ambacho ni ngumu kupata matokeo ambayo walikuwa wanayataka.
Hata viongozi wa Liverpool walikuwa na wanampa kila ambacho alikuwa anakitaka na kukiona kuwa kikiwepo ndani ya timu basi timu itaimarika.
Dunia ilishangaa alipomleta Mohammed Salah kwa bei ambayo ilivunja rekodi ya usajili wa klabu kwa kipindi kile ambacho anakuja Liverpool.
Lakini mwisho wa siku Mohammed Salah akawa mhimili mkubwa sana ndani ya klabu ya Liverpool tofauti na matazamio ya waliowengi.
Hata kipindi ambacho aliamua kutumia bei ya mshambuliaji kumleta Van Djik watu walimshangaa sana na wakamsema sana.
Kwa mara ya kwanza walishuhudia beki ananunuliwa bei ambayo washambuliaji ndiyo huwa wananunuliwa hivo.
Alikuja kuwaacha midomo wazi pale alipoamua kumchukua Allison kwa bei kubwa tena kwa mara nyingine kwa bei ya mshambuliaji.
Dunia iliongea sana lakini Jurgen Klopp alikuwa anajua kipi ambacho alikuwa anakifanya kwa wakati huo. Alikuwa anatembea kwenye ahadi yake.
Aliwapa misimu mitatu mashabiki wa Liverpool, walimwamini sana. Msimu wa pili alionesha mwanga. Alifika fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Lakini kilichomwangusha ni golikipa, ndiyo maana aliona tatizo liko wapi baada ya kugundua kwa mara ya kwanza kuwa ana beki mbovu.
Ndiyo maana akatumia pesa nyingi kumleta Van Djik. Safu ya ulinzi ikaimarika. Mabeki wa kati wakawa hawana makosa binafsi kama awali ilivyokuwa kwa Matip na Lovren.
Klaus aliwanyima kombe la ligi ya mabingwa barani ulaya kwa makosa binafsi ambayo aliyafanya. Ndicho chanzo cha Jurgen Klopp kumleta Allison.
Leo hii Liverpool inaonekana kama timu ambayo imeimarika zaidi. Timu ambayo ina nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa wa ligi ya mabingwa barani ulaya na hata wa ligi kuu ya England.
Timu ambayo ni imara zaidi. Ndiyo maana ilikuwa na uwezo wa kuifunga Arsenal kwa idadi kubwa ya magoli na hii ni kwa sababu wana timu imara kuzidi Arsenal.
Wakati nawatazama Arsenal, niligundua kitu kimoja ambacho Unai Emery anatakiwa kukifanya.
Jurgen Klopp alikuwa anampa ujumbe Unai Emery kuwa anatakiwa kufuata kitu ambacho Jurgen Klopp alikifanya.
Anatakiwa kutengeneza timu yake ambayo anaiona ni timu imara. Anatakiwa kuleta wachezaji ambao wanaweza kumsaidia hasa hasa kwenye eneo la ulinzi.