Nimefuatilia kwa makini na kwa muda sasa suala la mkanganyiko juu ya
kadi tatu za njano kwa Mohammed Fakhi wa Kagera Sugar na kutotolewa
adhabu yoyote.
Suala hili ni kubwa, kwa sababu limeonesha udhaifu uliopo kwenye soka
Tanzania, kwa namna ya pekee kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
likielekea kukosa rekodi muhimu na pia kutozingatia vyema sheria za
soka.
Simba walilalamika kwamba wapinzani wao, Kager Sugar walichezesha
mchezaji Fakhi akiwa na kadi tatu za njano, jambo ambalo ni kosa, n
ahata bila kulalamika huko Kagera walitakiwa kuadhibiwa moja kwa moja
na TFF.
Baada ya kuadhibiwa kwa kuchezesha mchezaji asiye na sifa kwa wakati
husika, wangeweza kuzitoa pointi hizo kwa Simba au kuwapokonya Kagera
na kuziacha hewani, kama ambavyo imepata kufanywa hata huku ambako
soka imeendelea.
Ajabu ni kwamba baada ya Simba kulalamika, ile Kamati ya Saa 72
ikaamua kuwapokonya Kagera pointi hizo ilizopata kwa ushindi wa mabao
2-1 na kuwapa Simba, Kagera walikata rufaa kwenye Kamati ya Sheria na
Haki za Wachezaji, na huko ikafanikiwa kurejeshewa mabao na pointi
zake tatu.
Hiki ni kituko; cha kujiuliza ni kwamba inakuwaje Simba wapokwe tena
pointi hizo lakini Kagera wasiadhibiwe kwa kosa la kumchezesha
mchezaji mwenye kadi tatu za njano?
TFF hawajasema kwamba Fakhi hakuwa na kadi hizo, isipokuwa
walichofanya ni kutafuta sababu nyingine za kuwanyang’anya Simba
pointi zao halali. Sababu zenyewe ni kwamba rufaa ilichelewa, Simba
hawakulipa gharama za kusimamia rufaa na kwamba Kamati ya Saa 72
ilikaribisha wajumbe kutoka nje ya TFF.
Ajabu ni kuwa TFF hawajajibu hoja ya msingi ya Fakhi kucheza akiwa na
kadi tatu za njano. Kwenye sheria kuna vitu vinaitwa ‘material and
immaterial facts’. Suala la rufaa kuchelewa ni ‘immaterial’ kwa sababu
halikuwa sehemu ya mgogoro (undisputed).
Mgogogo ulikuwa; je, Fakhi ana kadi tatu au lah. TFF wanakiri kuwa
Fakhi ni kweli alikuwa na kadi tatu za njano, isipokuwa
wamewanyang’anya Simba pointi zao tatu kwa sababu eti walichelewesha
rufaa. Hiki ni kichekesho kikubwa.
Ikiwa Simba wameadhibiwa kwa kuchelewesha rufaa na ‘blahblah’
nyingine, je Kagera Sugar wamechukuliwa hatua gani kwa kumchezesha
mchezaji mwenye kadi tatu za njano? Huwezi kuiadhibu timu
iliyochelewesha rufaa ukaiacha timu iliyomchezesha mtu mwenye kadi
tatu za njano.
=-=