Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Issa Hayatou amekanusha yeye au wajumbe wa Afrika kupokea rushwa ili kuiidhinisha Qatar kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2022.
Makamu huyo wa rais wa Fifa amesema tuhuma hizo zilizowekwa wazi Jumapili hii na kuambatanishwa na takwimu na nyaraka kuwa ni za kipuuzi.
Hayatou aliyeshika urais huo kana kwamba ni wa maisha na ni mjumbe mwandamizi katika Kamati ya Utendaji ya Fifa ametajwa kuwa mmoja wa wajumbe waliopokea mlungula kutoka kwa aliyekuwa Makamu Rais wa Fifa, Mohammed Bin Hammam.
Takwimu husika zimepatikana kutokana na kunaswa mawasiliano mbalimbali kati ya Bin Hammam na wajumbe wa mkutano huo wa Fifa, ikiwa ni pamoja na barua pepe.
Hii si mara ya kwanza kwa tuhuma za rushwa kuelekezwa kwa Hayatou ambaye 2011 alidaiwa kulipwa pauni 923,000 ili aweke kura yake kwa Qatar na akafanya hivyo.
Bin Hammam anadaiwa kumwalika Hayatou katika maeneo ya kifahari huko Doha, Qatar kwa ajili ya kutaka utayari wake kuichagua Qatar lakini pia Bin Hammam akamtumia tiketi za Kombe la Dunia zenye thamani ya dola 3,800 hotelini kwake.
Kadhalika, ilikuwa mwezi mmoja tu kabla ya Bin Hammam kuwezesha ufadhili wa dola milioni moja kudhamini mkutano mkuu wa mwaka wa CAF.
Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza, Nick Clegg amependekeza Qatar ivuliwe uenyeji huyo, jambo linaloungwa mkono na Chama cha Soka (FA) cha England.
Uchunguzi juu ya rushwa hiyo umeshaanzishwa na Fifa, ambapo CAF imethibitisha kwamba mawasiliano yamefanywa kwa hayatou kwa barua pepe kukiwa na maswali mengi juu ya mwenendo wake.
Inaelezwa kwamba Hayatou amekuwa akipokea zawadi za thamani kubwa kutoka kwa Bin Hammam na kwamba katika ziara yake aliyofanya Doha alipewa heshima kubwa sana.
Hata hivyo, taarifa ya CAF inakanusha kwamba Hayatou alihudhuria hafla au mikutano ya Bin Hammam Doha wala Kuala Lumpur, Malaysia au kupokea fedha kutoka kwake au kamati ya maandalizi ya Qatar.
CAF imedai rais huyo anasubiri kwa hamu ushahidi na anaweza kuchukua hatua za kisheria ili jina lake linalochafuliwa lisafishwe.
Watu wengine wa Asia wanahusishwa na mlungula kutoka kwa Bin Hammam, unaodaiwa walipokea ili waichague Qatar kuwa mwenyeji, na Qatar ikaupata uenyeji huo.
Comments
Loading…