Licha ya Hull City kushuka daraja msimu wa mwaka juzi, moja ya wachezaji waliokuwa bora kwenye kikosi hiko walikuwa ni Harry Maguire na Andy Robertson na ndio wachezaji pekee walioonekana kustahili kubaki ligi kuu.
Na mpaka kumalizika kwa michuano ya kombe la dunia na msimu wake wa kwanza ndani ya jiji la Leicester, Maguire anaonekana kuimarika kwa kasi akiwa amefanya poa sana katika mashindano makubwa zaidi ya soka.
Harry Maguire amekuwa na kombe la dunia ambalo atalikumbuka sana mwaka huu. Amekuwa bora sana kwenye safu ya ulinzi ya Gareth Southgate na si ajabu ni jina ambalo haliishi tetesi.
Nguvu kubwa ya England ilikuwa ni kupitia mipira iliokufa na licha ya kufunga bao 1 lakini Maguire ndio alikuwa sababu ya mengine mengi. Maguire tangu akiwa Leicester ni beki ambae anapenda kuuchezea mpira na ni Marc Albrighton msimu uliopita kwenye kikosi cha mwalimu Claude Puel ambae amegusa mpira zaidi yake. Hii inakufunza nini?
Maguire ni ambae anaweza kuuchezea mpira miguuni na ni mtu anaejitenga aweze kuchezeshwa na wenzie. Lakini pia ni beki anaejiamini na mwenye uthubutu wa kupiga chenga na kuisogeza timu mbele kule upande wa kushoto alikokuwa na Ashley Young na kupiga pasi kwenda mbele lakini Maguire ana takwimu bora za kushambulia kuliko Stones, Jones na hata Gary Cahill na hii ndio ilikuwa silaha ya siri ya waingereza.
Njia kubwa ambayo England waliitumia kufika kwenye sanduku la wapinzani ilikuwa ni kupitia mipira ya kutenga na Maguire alikuwa ni mtu msumbufu kwa walinzi wa timu pinzani. Huyu ndio alikuwa kama chambo huku wengine wakitawanyika kushambulia mipira.
Wakati kona inaingia Harry Kane, John Stones na Harry Maguire walikuwa wanajipanga kama mshkaki karibu na mstari wa 18. Lakini wakati kona zinapigwa ni Kane na Stones ndio walikuwa wanatoka zaidi na kushambulia, huku Maguire yeye akiishambulia zaidi ile mipira ambayo ilikuwa inakuja kwenye mwelekeo wake zaidi.
Kwaiyo uwepo wake na jinsi alivyoonesha kuwa tishio ndio kulikuwa kunawafanya wachezaji wa timu pinzani wawe tight zaidi na Maguire jambo ambalo liliwaruhusu Stones na Kane kuwa huru kwenye boxi na kufunga.
Mechi ya kwanza kwenye makundi dhidi ya Tunisia, Maguire alikutana na kona na kupiga kichwa akiwa amekaliwa na wachezaji kadhaa lakini baada ya kipa, Ben Mustapha kukipangua, Kane akawa huru na kufunga.
Mechi na Panama nayo wachezaji walim-target zaidi Maguire na ndipo kina Stones na Kane wakachomoka. Stones akafunga mara 2 vichwa huru kabisa huku Kane yeye akifuatwa kwa kasi na kuangushwa kwaiyo mpaka yale matukio ya penati unakuta kwamba Maguire alihusika kwenye kuwapa faida ile England japo ni kwa njia ambayo haionekani moja kwa moja.
Maguire ndio alikuwa sehemu kubwa ya ulinzi lakini sehemu kubwa ya ushambuliaji pia. Ni beki mwenye mwili mkubwa akiwa na kilo 100 mwilini na haishangazi kuwa huyu ndio nyota kwenye kikosi cha England mara hii ambae amekuwa akihusishwa na vilabu kadhaa vikubwa.