Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Kenya wanakwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil kwa ajili ya kujifunza.
Rais Uhuru Kenyatta ndiye anagharamia safari na malazi ya timu hiyo, ikiwa ni zawadi kwa kufanya vizuri katika eneo lao na kuwachochea kufuzu kwa michuano ijayo.
Nahodha wa Harambee Stars, Jeremy Onyango anasema kwamba ndoto yao ya kwenda kwenye fainali hizo kujionea moja kwa moja inatimia.
Kenyatta anasema yeye na mkewe, Margaret walitoa ahadi ya kuwapeleka Brazil wachezaji hao iwapo wangefanya vizuri kwenye michuano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
Rais na mkewe wanatoa dola 120,000 kwa safari hiyo huku Kampuni ya Bia ya Afrika Mashariki (EABL) ikiamua kuchangia dola 40,000.
Kenya ni moja ya nchi zenye mafanikio kimichezo lakini haijawahi kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia.
Mapema wiki hii, Rais Kenyatta aliwaonya Wakenya dhidi ya kutazama mechi za michuano hiyo kwenye baa zilizojaa watu kwa maelezo kwamba magaidi wangeweza kushambulia.
Hata hivyo, tangu mechi ya ufunguzi Wakenya walikusanyika kwa wingi kwenye baa wakipata kinywaji na kutazama mechi hizo bila wasiwasi.
Haijajulikana wachezaji hao wa Harambee Stars watakaa Brazil kwa muda gani wala ni mechi zipi watashuhudia.
Ghana ambao wamefuzu kwa fainali hizi, japokuwa wapo kwenye kundi la kifo lenye timu za Ujerumani, Ureno na Marekani, wamepeleka washabiki 500 kushangilia Black Stars.
Washabiki hao wanagharamiwa na fedha kutoka katika sekta binafsi iliyoamua kuchangisha kampuni mbalimbali ili kuwatia moyo vijana wao.
Kenyatta ni mmoja wa matajiri wakubwa Afrika, na inaelezwa kwamba atargharamia wachezaji 11 wa kikosi cha kwanza kwa fedha za mfukoni mwake.
“Ninyi vijana tunataka mwende huko Brazil mkajifunze, mpate mori wa kufanya vizuri zaidi siku zijazo.
“Nendeni muangalia viwango vya kimataifa katika soka na muige ili hatimaye nanyi mfuzu katika michuano ijayo. Ahadi ile ni ya binafsi,” akasema Rais Kenyatta.
Ameongeza kwamba serikali yake itaweka wazi hivi karibuni hatua itakazochukua kuongeza nguvu kwenye michezo ambayo viongozi wake wamekuwa wakituhumiwa kushindwa kusimamia vyema.
Comments
Loading…