HATIMAYE Shirikisho la Soka nchini(TFF) limesalimu amri kumzuia mchezaji wa Simba Gervas Kago asicheze mchezo wa ngao ya Jamii dhidi ya Yanga baadaye leo saa mbili kamili usiku usiku katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.
Jumatatu TFF kupitia kwa Katibu Mkuu wake Angetile Osiah ilitangaza kumzui mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Afrika ya Kati kuichezea Simba katika mchezo wa ngao ya jamii na ligi kwa sababu ya kutokana na uhamisho wa mchezaji huyo kutofuata taratibu za uhamisho wa kimataifa kwa njia ya mtandao TMS.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Mikataba na Hadhi ya Wachaji ya TFF Alex Mgongolwa alisema kwamba mchezaji huyo sasa ruksa kuchezea klabu hiyo yenye masikani yake mtaa wa msimbazi katika mchezo wa ngao ya hisani dhidi ya Yanga leo.
Akitoa ufafanuzi Mgongolwa alisema kwamba wameamua kumruhusu mchezaji huyo acheze kwa sababu mchezo wa Ngao ya Hisani hauko kwenye kanuni za mashindano za TFF, hivyo hakuna haja ya mchezaji kufuata uhamisho wa kimataifa kwa njia ya mtandao.
Alisema sababu nyingine kuwa ni kwamba mchezo huo ni maalumu kwa ajili ya kusaidia jamii, hivyo mapato yatakayopatikana katika mchezo huo yataelekezwa katika huduma za jamii na kwamba timu ya Simba imeonyesha nia ya dhati katika kulishughulikia suala la mchezaji huyo.
Aidha, Mgongolwa alisema kwamba ligi ya Afrika ya Kati inafuata taratibu za uhamisho wa kimataifa kwa njia ya mtandao yaani TMS na kuongeza kwamba hata ukisoma katika mtandao utaona kwamba kuna meneja anayeshughulika na uhamisho kwa njia hiyo katika shirikisho la soka la nchi hiyo.
Aliongeza kwamba kama Simba itaweza au kutomtumia mchezaji huyo kwenye ligi bado itategemea na majibu kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambayo bado inafuatilia kuchelewa kwa usajili wa mchezaji huyo.
“Bado tunaendelea kufuatilia kuchelewa kwa usajili wa mchezaji huyo “ Mgongolwa alinukuu taarifa kutoka Fifa kwenda TFF kuhusu usajili wa mshambuliaji huyo tegemeo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Mgongolwa alisema kwamba kama Fifa ikimruhusu mchezaji huyo kucheza basi hakuna shaka atacheza katika ligi lakini kama ikimkataza basi Simba haitakuwa na jinsi zaidi ya kusubiri mpaka dirisha dogo lifunguliwe mwezi Novemba.
Katika hatua nyingine Uongozi wa Simba kupitia msemaji wao Ezekiel Kamwaga umesema kwamba umepokea kwa furaha taarifa za kuruhusiwa kwa mchezaji wao na kuwataka mashabiki wao wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu yao leo.
Kamwaga aliongeza kwamba tayari Mwenyekiti wa klabu hiyo Ismail Aden Rage yupo safarini kuelekea Jamhuri ya Afrika ya Kati kukamilisha usajili wa mchezaji huyo.
Comments
Loading…