Mlinzi wa zamani wa Manchester United na Timu ya Taifa ya England, Gary Neville ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa Valencia ya Hispania.
Hizi ni habari za kushangaza kiasi, kwani mdogo wake, waliyecheza naye Man United, Phil Neville alipewa mikoba ya ukocha msaidizi hapo kitambo kidogo nyuma.
Gary (40) amepewa kazi hiyo, ikielezwa kwamba ni hadi mwishoni mwa msimu huu na ataanza kazi yake rasmi Jumapili hii.
Anachukua nafasi ya Nuno Espirito Santo, aliyejiuzulu nafasi hiyo Jumapili iliyopita baada ya kufungwa 1-0 na Sevilla, matokeo yaliyowaacha Valencia katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania – La Liga.
Msimu uliopita walimaliza katika nafasi ya nne, lakini safari hii wamejikuta wakishinda mechi tano tu kati ya 13 za kwanza
Mwanamichezo huyu ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya michezo kwenye mechi zinazorushwa mubashara kwenye televisheni, ataendelea kuwa kwenye benchi la ufundi la Timu ya Taifa ya England – Three Lions.
Mmiliki wa Valencia, raia wa Singapore, Peter Lim, ana hisa kwenye klabu ndogo ya Salford City iliyo nchini England, ambayo Garry ni mmiliki mwenza.
Taarifa zinasema kwamba, ndugu yake na Garry, yaani Phil, aliyejiunga na Valencia kama kocha msaidizi Julai mwaka huu, atabaki kwenye benchi la ufundi klabuni hapo akiwa msaidizi wake.
“Kwa kweli nimefurahishwa sana kupewa fursa hii ya kufanya kazi Valencia kwani ni klabu kubwa na wana heshima isiyo ya kawaida.
“Nawajua tangu enzi hizo nikiwa mchezaji, na nimekuwa navutiwa sana na mahaba na kujitolea kwa nguvu zote kwa washabiki wa Valencia,” akasema Gary.
Kwa uteuzi huo, kocha huyu mkuu mpya wa Valencia ameachia ngazi mara moja katika kazi yake ya uchambuzi kwenye kituo cha televisheni cha Sky Sports.
Rais wa Valencia, Layhoon Chan amesema kwamba Gary anaheshimiwa sana katika soka ya England na kwamba wamezingatia viwango vyake binafsi kumpatia kazi hiyo.
Gary alicheza mechi ya kwanza na Man United 1992 na kukaa hapo kwa muda wa miaka 19, akitwaa nao mataji 20 ya michuano mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na manane ya Ligi Kuu ya England.
Alianza kuchezea Three Lions 1995, akawakilisha taifa lake katika mechi 85. Alianza kazi Sky Sports msimu wa 2011/12.
Mwaka 2012 aliteuliwa kuwa kocha msaidizi wa England, chini ya Roy Hodgson katika timu ya taifa.
Mwaka jana alikuwa mmoja wa watu walioingia makubaliano ya kununua klabu ya Salford City, sambamba na wachezaji wenzake wa Man U, kaka Phil, Ryan Giggs na Paul Scholes.
Mwaka jana pia waliuza asilimia 50 ya hisa za klabu hiyo kwa Lim, ambaye ni mfanyabiashara na aliyekuwa tayari anamiliki asilimia kubwa ya hisa za Valencia.
Wakati Phil ataongoza kikosi kwenye mechi mbili dhidi ya Barakaldo kwenye michuano ya Kombe la Mfalme (Copa Del Rey) na dhidi ya Barcelona Jumamosi hii, Gary atashika hatamu kwa mara ya kwanza kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya  dhidi ya Lyon.