*Bility nje, Platini amesubirishwa
*Wagombea watano sasa rasmi
Rais wa Shirikisho la Soka la Liberia, Musa Bility ameondoshwa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kufanyika uchambuzi wa sifa za wajumbe wote walioomba kugombea, ambapo yeye ameenguliwa kwa sababu za upungufu wa maadili kwa upande wake.
Baada ya mapitio hayo, FIFA imeidhinisha wagombea watano, huku Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA), Michel Platini naye akiachwa na alama ya kuuliza, kwani amefungiwa kujihusisha na soka kwa siku 90 huku akichunguzwa.
Iwapo atasafishwa kwenye uchunguzi unaofanywa dhidi yake sambamba na Rais wa FIFA, Sepp Blatter ambaye pia amesimamishwa kwa siku hizo, anaweza kuongezwa kwenye orodha ya wagombea hao watano kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari mwakani.
Kwa msingi huo, walioidhinishwa kwa sasa kuwania urais wa FIFA ni Prince Ali bin al-Hussein, Jerome Champagne, Gianni Infantino, Sheikh Salman bin Ebrahim al-Khalifa na Tokyo Sexwale.
Bility, 48, alipata kusimamishwa kwa miezi sita kujihusisha na shughuli zozote za michezo, nayo ilikuwa 2013, baada ya kubainika kwamba alitumia nyaraka za siri kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) katika shauri dhidi ya Rais wa CAF, Issa Hayatou.
Alihusika pia katika kupinga kubadilishwa kwa kanuni za CAF, mchakato ambao hatimaye alishindwa na kanuni kubadilishwa na kumruhusu Hayatou kuwania na kuchaguliwa tena kwenye nafasi hiyo bila kupingwa Machi mwaka huu.
Kwa sasa Hayatou ndiye anakaimu nafasi ya urais wa FIFA. Bility amesema kwamba ameshajulishwa na shirikisho hilo kwamba ugombea wake umekataliwa kwa sababu ya marufuku aliyokuwa amewekewa, lakini hakubaliani na uamuzi huo.
“Nalikataa hili na nadhani ni bahati mbaya sana. Uamuzi wangu wa kupinga CAF wakati ule ulikuwa njia sahihi za kujaribu kubadili soka ya Afrika na kuzuia kanuni kukiukwa hovyo hovyo. Nasubiri jopo langu la wanasheria kupitia uamuzi huo na kupanga hatua itakayofuata,” akasema Bility ambaye ni mfanyabiashara mkubwa wa mafuta nchini mwake.
FIFA kwa upande wake, imesema haitajadili zaidi sababu za kuondoshwa kwa Bility kwenye kinyang’anyiro hicho, uamuzi ambao anaweza kuukatia rufaa kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).
Uchaguzi huu unafanyika kutafuta mtu wa kuchukua nafasi inayoachwa wazi na Blatter (79) aliyeamua kuachia ngazi kwa maelezo kwamba licha ya kushinda kwenye uchaguzi wa Mei mwaka huu, si ulimwengu wote wa soka unaomuunga mkono.
Pamoja na kufungiwa kwake kushiriki shughuli za michezo, hatua iliyochukuliwa na Kamati ya Maadili ya FIFA, Blatter yupo chini ya uchunguzi wa jinai, hatua inayofanywa na mamlaka za dola ya Uswisi. Alitangaza uamuzi wa kuachia ngazi siku nne tu baada ya kuchaguliwa, lakini alikuwa akiendelea na kile anachokiita mchakato wa mageuzi makubwa kwenye masuala ya FIFA.
Pamoja na mambo mengine, Blatter anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha, ambapo 2011, muda mfupi kabla ya mchakato wa uchaguzi wa rais wa FIFA, alimpatia Platini pauni milioni 1.35 na Platini akajitoa kumpinga punde baadaye. Platini anatuhumiwa kutenda kosa kwa kuzipokea, akisema ni malipo ya kazi ya ushauri wa ufundi wa rais wa FIFA, aliyokuwa ameifanya kitambo kirefu kabla.