Mkutano maalumu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) umepitisha
mageuzi makubwa, yakilenga kurejesha hadhi yake baada ya kutikiswa na
umangimeza na ufisadi.
Pamoja na mambo mengine, kutakuwapo kuanikwa wazi mishahara pamoja na
ukomo wa muda wa urais wa Fifa. Baraza jipya la Fifa litachukua nafasi
ya kamati kuu ya sasa, na litatakiwa kuwa na walau mwanamke mmoja
kutoka kila shirikisho.
Baada ya kuidhinisha mabadiliko kadhaa, wajumbe wa mkutano mkuu huo wa
Fifa watafanya uchaguzi kupata rais mpya atakayechukua mikoba
inayoachwa na Sepp Blatter aliyekuwa katika nafasi hiyo tangu 1998.
Pamoja na kushinda kwenye uchaguzi wa mwaka jana, Blatter aliahidi
kuachia ngazi Ijumaa hii kwa sababu haoni akiungwa mkono na ulimwengu
wote wa soka. Alishauriwa tangu mwanzo asiwanie tena nafasi hiyo, na
kabla ya uchaguzi washirika wake kadhaa walidakwa na askari wa Uswisi
kwa maombi ya Marekani na wamefunguliwa kesi za utakatishaji fedha,
wizi na ubadhirifu wa mali ya umma.
Hata hivyo, alikuja kusimamishwa kazi na Kamati ya Nidhamu na Maadili
ya Fifa, baada ya kutiwa hatiani kujihusisha na mlungula yeye pamoja
na Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Michel Platini
aliyekuwa anataka kugombea nafasi hiyo. Wote rufaa zao zimetupwa na
wanabaki na madoa.
Wagombea wanaowania urais wa Fifa ni Sheikh Salman bin Ebrahim
al-Khalifa, Gianni Infantino, Prince Ali bin al-Hussein, Tokyo Sexwale
na Jerome Champagne. Fifa imekuwan ikiongozwa na kaimu rais, Issa
Hayatou ambaye ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF)
aliyesema kwamba Fifa itabaki kuwa moja na wanaoiunda watakuwa na
usharika mzito.
Viwango vya mishahara kwa rais wa Fifa, wajumbe wote wa baraza, katibu
mkuu na viongozi wa kamati maalumu na zile za kimahakama vitawekwa
wazi kila mwaka. Kuanzia anayechaguliwa leo, rais wa Fifa hatakaa
madarakani kwa zaidi ya vipindi vitatu vya miaka minne minne. Blatter
alikaa vipindi vitano.
Katika hatua nyingine, wajumbe wa mkutano huo wameamua kutenganisha
kazi za kisiasa na za kiutawala, ambapo baraza litawajibika kubuni
mkakati wa mwelekeo wa shirikisho hilo. Katibu mkuu wa Fifa atasimamia
utawala na masuala ya biashara katika utekelezaji wa mikakati husika.
Pamoja na viongozi mbalimbali wa soka wa sasa na wa zamani wa Fifa
kudakwa na askari na kushitakiwa, wadhamini mbalimbali wamekuwa
wakijiondoa ili kujitenga na uchafu wa Fifa. Mamlaka za Uswisi nazo
zinaendesha uchunguzi kwa maofisa wa Fifa.
Blatter anadaiwa kutoa hongo ya pauni milioni 1.3 kwa Platini ili
asimpinge kwenye uchaguzi wa 2011. Muda mfupi baada ya malipo hayo
Blatter alijitoa na kuwavuruda wadau waliokuwa wamepanga kumuunga
mkono ili kumng’oa Blatter.
Hata hivyo, wawili hao wanapinga kuwa ilikuwa hongo, bali wanadai
yalikuwa malipo halali kwa Platini aliyekuwa mshauri wa ufundi wa rais
wa Fifa (Blatter). Kinachoshangaza ni kwamba mshahara huo ulitolewa
miezi mingi baada ya kuwa amemaliza kazi hiyo na muda mfupi tu kabla
ya uchaguzi, kisha akajitoa kwenye kinyang’anyiro.