Wakati wa uongozi wa rais TFF, Leodgar Tenga tulishuhudia timu ya taifa ya Brazil ikiwa mgeni wa Taifa Stars kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa siku chache kabla ya kuanza fainali za kombe la dunia nchini Afrika kusini mwaka 2010.
Brazil na wachezaji wake walishangazwa jinsi uwanja wa Benjamin Mkapa ulivyo mzuri na kuvutia zaidi, kuanzia ndani ya dimba hadi majukwaa yake. si Brazil pekee, bali mataifa mengi yamecheza katika uwanja wa Benjamin Mkapa.
Hivi karibuni mechi za mbili za makundi ya Ligi ya mabingwa Afrika kati ya CD Belouzidad na Kaizer Chiefs ulichezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa. Mechi za mabingwa wa soka nchini Simba wametumia uwanja huo kama wa nyumbani. Hiyo ni mifano michache ambayo kwa namna moja au nyingine imetangaza Tanzania.
Ni uwanja ambao unafurahiwa na timu mbalimbali kutokana na ubora wake na umesifiwa na mataifa mengi juu ya kiwango kilichopo. Tanzania ina viwanja vitatu vya uhakika, Benjamin Mkapa, Uhuru na Amaan visiwani Zanzibar.
Tatizo la ubora wa viwanja barani Afrika limekuwa jambo la kusikitisha mno. Viwanja vingi vinavyomilikiwa vinakosa mambo muhimu ambayo sasa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA limeamua kiuvalia njuga ili kukomesha mataifa yanayotumia viwanja vibovu.
Ubovu wa viwanja vingi Afrika unatokana na kushindwa kuvihudumia, kutaka kupata mapato bil kuendeleza na kuimarisha viwanja vyenyewe. Ni sawa na kauli ya nyota wa zamani wa Senegal, El Hadji Diouf ambaye alisema “katika soka Afrika, viongozi wengi wanapenda fedha za mchezo huo lakini hawana mipango madhubuti ya kuendeleza mchezo wenyewe”.
Kauli ya El Diouf inasadifu uamuzi wa FIFA kupiga marufuku kwa viwanja kadhaa vya soka barani Afrika. Uamuzi huo pia umetajwa kuwa utaathiri mechi za ufunguzi za kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa ukanda wa Afrika kuanzia mwezi ujao.
FIFA imepiga marufuku katika viwanja vya mataifa ya 10 kati ya 40 yanayoshiriki katika kampeni ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia ambayo yanakabiliwa na tishio la kucheza mechi zao nje nje ya mipaka yao.
Kutokana na uamuzi huo, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) nalo limewasilisha barua kwa mashirikisho wanachama yenye orodha ya viwanja vilivyoidhinishwa kwa mizunguko miwili ya kwanza katika hatua ya makundi.
Nchi zilizoathiriwa ni pamoja na Senegal, ambao walishiriki kwenye Fainali zilizopita za Kombe la Dunia huko nchini Urusi mwaka 2018. Nyingine ni Mali ambao walikuwa miongoni mwa timu zilizoshinda nafasi ya kwanza.
Zipo nchi za Burkina Faso, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Liberia, Malawi, Namibia, Niger na Sierra Leone zote hazijaidhinishiwa viwanja vyao vya nyumbani wakati CAF ikiwa imesimama kidete kuhakikisha wanachama wake wanakuwa na viwanja vyenye ubora kote barani humu.
Baada ya viwanja hivyo kupigwa kufuli, sasa timu hizo zina muda mfupi wa kujiandaa na kuboresha viwanja wanavyotaka vitumike kwenye michezo ya kufuzu kabla ya tarehe ya mwisho ya kuthibitisha majina ya viwanja vya nyumbani ifikapo Juni 5 mwaka huu.
Na ikiwa nchi hizo zilizopigwa marufuku zitashindwa kukidhi vigezo vya ubora wa viwanja vya kucheza mechi hizo, basi zitalazimika kuchagua viwnaja vya nchi nyingine ili viwe viwanja vya nyumbani.
Kwa upande wao, Senegal inatarajia kufungua dimba dhidi ya Togo katika mchezo wa kundi H wiki ya kwanza ya mwezi Juni, lakini Uwanja wao maarufu wa Leopold Senghor umefungwa kwa ukarabati ili kufikia vigezo vinavyotakiwa na FIFA na CAF.
Nchi zingine DR Congo, Libya na Uganda wamekataliwa viwanja vyao lakini bado wataweza kucheza nyumbani kwenye viwanja vidogo kama mbadala.
Uganda iliripotiwa kuomba kutumia uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kama uwanja wao wa nyumbani ikiwa FIFA na CAF watakataa moja kwa moja kutumika viwanja vyao, hivyo kulaizmika kutoka nje hadi Tanzania.
Hatua ya awali ya makundi ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia barani Afrika ina nchi 40 zilizogawanywa katika vikundi 10 yenye timu nne. Timu hizo zitacheza mechi sita kila mmoja hadi ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.
Kiha mwezi Novemba, washindi wa makundi wataungana kwa mechi tano za mchujo na washindi wa jumla watafuzu kwa fainali zitakazofanyika Qatar mwakani.
Kw kiasi kikubwa mchezo wa soka barani Afrika umeathiriwa kwa muda mrefu kwa kutokana na viwanja dunia vya kuchezea mchezo huo unaopendwa na wengi na wenye utajiri mkubwa miongoni mwa michezo yote barani humu.
Licha ya wanachama kukumbushwa na kuelimishwa mara kwa mara kuhusu viwnaja, lakini hatua madhubuti zimekuwa za kusuasua kwahiyo safari hii CAF wameshikia bango na kuwa wakali zaidi baada ya kupiga marufuku viwanja visivyo na ubora unaohitajika.
Machi mwaka huu CAF ilipiga marufuku kwa viwanja kadhaa barani kote kwa raundi ya mwisho ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika, kabla ya baadaye kubatilisha uamuzi huo. CAF haikutoa ufafanuzi kuhusu kubadilisha uamuzi wake wa awali, lakini angalau ilichukua hatua kali dhidi ya ubovu wa viwanja barani Afrika.
Viwanja vingi vimekuwa na matatizo ya majukwa, ulinzi na usalama,nyasi kukauka katikati ya uwanja,huduma zinazozunguka viwanja kuwa mbovu, ubovu wa vyumba vya kubadilishia nguo kuwa vibovu,ukosefu wa maji na hewa ya kutosha,usalama hafifu wa waamuzi,majukwaa kutokidhi vigezo na mengineyo.
Viwanja vingi vimekuwa kama magofu ambayo yanatumika pale yanapohitajika, na huduma za kutunza hakuna. Bila shaka huu ni wakati sahihi FIFA na CAF kudhibiti na kuwakaripia kivitendo wanachama wake ili wawe na viwanja vyenye hadhi ya kutumika kwenye mashindano yake. Ni somo maridadi.
Comments
Loading…