Crystal Palace v Man United
Jumamosi hii kuna kivumbi kwenye Uwanja wa Wembley, pale Crystal
Palace watakapomenyana na Manchester United katika fainali ya Kombe la
FA na kumaliza mambo ya soka kwa msimu huu hapa nyumbani.
Pande mbili hizi zilikutana kwenye fainali ya 1990, ikiwa ni fainali
pekee Palace waliyofanikiwa kufika katika historia. United walishinda
1-0 katika mechi ya marudiano, baada ya timu kwenda sare ya 3-3 kwenye
mechi ya awali.
Kocha wa sasa wa Crystal Palace, Alan Pardew aliicheza timu hiyo
kwenye mechi zote mbili. Hii ni mara ya kwanza tangu 2007 kwa United
kufika fainali hiyo lakini kwa ujumla wamefanikiwa kufika mara 19,
wakishinda 11 na kupoteza saba. Ni Arsenal tu wametwaa kombe hilo mara
nyingi zaidi kuliko Mashetani Wekundu, kwani wametwaa mara 12.
Takwimu zinaonesha kwamba Manchester United hawajapata kutwaa kombe
hilo tangu 2004 na hawajapata kulitwaa katika uwanja wa Wembley tangu
1999.
Hata hivyo, Palace nao historia haipo nao, kwani hawajapata kuwafunga
Man United kwenye michuano hiyo zaidi ya kwenda sare mara mbili na
kupigwa mara mbili pia. Ushindi pekee wa The Eagles dhidi ya Mashetani
Wekundu hao kwenye mashindano yoyote yale ulikuwa Novemba 2011
walipowafunga 2-1 kwenye mechi ya Kombe la Ligi.
Manchester United wameshinda mechi 15 kati ya 20 walizocheza dhidi ya
jamaa hawa wa Old Trafford, na hii ni kwenye mashindano yote. Vijana
hao wa London wameshinda mechi zao tatu za mwisho hapo Wembley, ikiwa
ni pamoja na mechi zote mbili tangu kufunguliwa uwanja huo 2007, na
kichapo waliwapa Watford.
Hii itakuwa mechi ya 14 kwa Manchester United dimbani hapo, sawa na
Chelsea, na hakuna timu iliyocheza hapo zaidi ya idadi hiyo. Palace
wameshinda mechi sita kati ya saba za Kombe la FA walipokutana na
wenzao wa Ligi Kuu ya England (EPL). Man U wameshinda mechi zao mbili
zilizopita za Kombe la FA dhidi yawenzao wa EPL, baada ya kukwamba
kupata ushindi kwenye mechi tano kabla ya hizo.
Ni Reading tu ambao wamefunga mabao mengi zaidi, 14, kuliko Manchester
United kwenye msimu huu wa Kombe la FA. Anthony Martial ameshiriki
katika nusu ya mabao 12 ya Man U msimu huu, akifunga mawili na kutoa
usaidizi kwa manne.