Kilio cha kuwa na wachezaji wengi zaidi wa England katika Ligi Kuu ya EPL kimeendelea, safari hii Mwenyekiti wa FA, David Bernstein akisema lazima waongezwe.
Mwenyekiti huyo anayeng’atuka madarakani mwezi ujao, anasema kwamba ni asilimia 30 tu ya wachezaji wa England kwenye ligi hiyo, wakati nchini Ujerumani ni asilimia 60, lakini akasema alishaanza kusuka mipango ya kurekebisha kasoro hiyo.
Pamekuwa na malalamiko kutoka maeneo mbalimbali, kwamba EPL ina wachezaji wengi mno wa kigeni, na kwamba athari zake ni kufanya vibaya kwa timu ya taifa ya England, ambayo kwa miaka mingi imeshindwa kuvuka hatua za robo fainali za mashindano yote.
Bernstein anasema kwamba suala la uzawa katika ngazi za klabu na nchi ni muhimu sana na kwamba anasikitishwa kuona kiwango kidogo cha wachezaji wa England, hivyo jitihada zaidi zinawekwa katika kukuza vipaji na kuwaendeleza vijana,
Hata hivyo, alijigamba kufanya kazi kubwa ya ukuzaji vipaji, akitoa mfano wa wachezaji mahiri kama Jack Wilshere wa Arsenal, ambaye ni kiungo anayejituma vilivyo uwanjani, ambaye hata hivyo alikuwa nje ya dimba kutokana na majeraha.
Mwenyekiti huyo anasema licha ya tatizo walilo nalo, ana imani kwamba timu ya taifa ya England itafuzu kuingia Fainali ya Kombe la Dunia Brazil mwakani, akisema uzalendo na moyo wa kazi alio nao kocha Roy Hodgson vinazaa matunda mazuri.
England walitoka sare ya mabao 2-2 na Brazil Jumapili kwenye uwanja wa Maracana nchini Brazil, ambapo nchi zote mbili zinaonekana kuwa na udhaifu, na hazitarajiwi kufanya vyema kwenye mashindano hayo yajayo.
Comments
Loading…