Ligi Kuu ya England (EPL) imefika patamu baada ya matokeo tofauti
mwishoni mwa wiki.
Wakati vinara Leicester wakienda vyema kwa kuendelea kushinda dhidi ya waliokuwa nafasi ya pili, Manchester City, Arsenal nao wamefufuka.
Baada ya mechi 25, Leicester wapo kileleni na pointi zao 53 wakati
City wakishushwa hadi nafasi ya nne, Arsenal wakipanda had ya tatu
wakifungana pointi na Tottenham Hotspur wanaoshika nafasi ya pili,
wote wakiwa nazo 48.
City wanazo pointi 47 wakiwa na kocha Manuel
Pellegrini anayeondoka mwisho wa msimu kumpisha Pep Guardiola aliye Bayern Munich kwa sasa.
Manchester United walipoteza pointi mbili dakika za mwisho Jumapili
hii baada ya kwenda sare 1-1 na Chelsea kwa bao la dakika ya mwisho la Diego Costa, akifuta lile la Man U la Jesse Lingard.
Arsenal wao walifunga mabao mawili katika sekunde 88 ugenini
walikokuwa wanacheza dhidi ya Bournemouth kwa mabao ya Mesut Ozil na Alex Oxlade-Chamberlain.
Arsenal wamepata ahueni kwani hawakuwa wameshinda tangu Januari 3,
ambapo Jumapili hii Aaron Ramsey alikuwa mchezaji bora wa mechi.
Chelsea kwa upande wao walifanikiwa kumpa raha kocha wao wa mpito, Guus Hiddink kwani tangu ajiunge nao hawajapoteza mechi, wamekuwa ama wakishinda au kwenda sare.
Matokeo mengine mwishoni mwa wiki ni kwa Villa kuwafunga Norwich 2-0,
Liverpool wakatoshana nguvu na Sunderland kwa 2-2, Newcastle
wakawabomoa West Bromwich Albion 1-0.
Stoke wakiwa nyumbani walilala 0-3 mbele ya Everton, Swansea na
Crystal Palace wakaenda 1-1, Spurs wakawafunga Watford 1-0 na
Southampton wakawashinda West Ham 1-0.
Bado Aston Villa wapo katika hali mbaya, wakishika nafasi ya mwisho
kwenye msimamo wa ligi kwa pointi zao 16, Sunderland wanazo 20,
Norwich 23 na Newcastle 24.