Ilikuwa Jumapili ya aina yake kwenye raundi ya mwisho ya mechi za Ligi Kuu ya England (EPL), na sasa pazia limeshushwa rasmi.
Jumapili ilikuwa kwa timu zote kushuka dimbani kwa wakati mmoja, kujua nani anakwenda Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), Ligi ya Europa na akina nani zaidi wangeshuka daraja baada ya Norwich kuwa wameshakwenda chini.
Ikawa kwamba Manchester United na Chelsea waliungana na wababe Liverpool na Manchester City kwenda UCL wakati Leicester wakikosa nafasi hiyo na kuangukia ligi ndogo ya Ulaya – Europa na watakuwa na Tottenham Hotspur.
Liverpool wamemaliza ligi wakiwa na alama 99, wakishindwa kufikia lengo la alama 100 au zaidi – rekodi inayoshikiliwa na Man City ambao safari hii wamemaliza wakiwa na alama 81, Man U 66 sawa na Chelsea.
Wanne hao bora walimaliza msimu wa 2019/2020 kwa Liverpool kuwapiga Newcastle 3-1, Manchester City kuwanyuka Norwich 5-0, Manchester United kuwashinda Leicester 2-0 na Chelsea kuwashinda Wolves kwa idadi hiyo hiyo ya mabao.
Walioungana na Norwich kushuka daraja ni Watford na Bournemouth, ambapo makocha na wachezaji wa timu hizo mbili walisononeka sana baada ya mechi zao, wakijua kwamba watakuwa chini – umaarufu unashuka, kipato nacho pia kitashuka na itakuwa kazi ngumu kujaribu kurudi juu.
Watford walishuka baada ya kupokea kipigo cha 3-2 kutoka kwa Arsenal wakati Bournemouth wameshuka licha ya kuwafunga Everton 3-1. Matokeo mengine katika mechi za mwsho wa EPL ni Brighton kuwafunga Burnley 2-1, Crystal Palace kwenda sare ya 1-1 na Spurs, Southampton kuwashinda Sheffield United 3-1 na West Ham kwenda sare ya 1-1 na Aston Villa.
Matokeo ya Villa anakochezea Mtanzania Mbwana Samatta yamewaokoa kushuka daraja kwa tofauti ya alama moja na Bournemouth. Villa wamemaliza wakiwa na alama 35 wakati Bournemouth ambao kocha wao Eddie Howe alikuwa akilia wana 34, wakati Norwich wana chache mno – 21.
Timu zilizopanda daraja kwa ajili ya msimu wa 2020/2021 ni Leeds, West Bromwich Albion na wataungana na timu mja kati ya Bentford, Fulham, Cardiff au Swansea, kutegemeana na matokeo ya mechi za mtoano zinazoendelea. Msimu utakamilishwa kwa mechi ya fainali ya Kombe la FA baina ya Arsenal na Chelsea katika Uwanja wa Taifa – Wembley.
Comments
Loading…