Ligi Kuu ya England (EPL) imeingia mzunguko wa pili, huku timu zikionekana kuendelea kujipanga wakati dirisha la usajili likiwa wazi kwa wiki mbili zaidi.
Wakati baadhi ya matokeo yamekuwa ya kawaida, kuna timu ambayo haijapata kushinda mechi ya EPL tangu 2007, huku baadhi zikishangaza kwa matokeo mazuri.
EVERTON WAWACHAKAZA SOUTHAMPTON
Everton waliokuwa hovyo msimu uliopita wameonesha nguvu ugenini baada ya kuwachakaza Southampton 3-0.
Mshambuliaji wa Ubelgiji ambaye msimu uliopita ulikuwa mbaya kwake, Romelu Lukaku ndiye aliyewavuruga Saints kwa kupachika mabao mawili katika kipindi cha kwanza, akitumia vyema nafasi mbili alizopata za kulenga goli la adui, likiwamo bao maridadi la kichwa.
Vijana hao wa Roberto Martinez walikuwa wakifanya mashambulizi makali ya kushitukiza, ambapo Lukaku alishirikiana vyema na Ross Barkley aliyefunga bao la tatu dakika sita kabla ya kipenga cha mwisho.
Saints nusura wapate bao, lakini kipa wao Mmarekani, Tim Howard alifanya kazi ya ziada kuokoa shuti la Sadio Mane mapema kipindi cha kwanza. Kocha wa Southampton, Ronald Koeman ameeleza kusikitishwa na matokeo na kusema lazima vijana wake wabadilike.
SPURS WAKATALIWA NA STOKE
Bao la kichwa la dakika za mwisho la Mame Diouf kwa Stoke liliwaezesha kuwakatalia Tottenham Hotspur ushindi wa kwanza msimu huu dimbani White Hart Lane. Spurs walikuwa wakitafuta ushindi baada ya kupoteza mechi ya kwanza dhidi ya Manchester United ugenini.
Eric Dier aliwapa Spurs bao la kuongoza kwa kichwa safi na Nacer Chadli akatia la pili. Wakati Spurs na washabiki wao wakidhani kwamba wangemaliza kwa ushindi, Stoke ambao wanajulikana kwa ugumu wao walipambana, wakipokea mara kwa mara maelezo ya kocha wao, Mark Hughes.
Jitihada zao zilizaa matunda, kwani Marko Arnautovic alikomboa moja kwa penati baada ya Toby Alderweireld kumwangusha Joselu kwenye eneo la hatari. Diouf alizima furaha za Stoke kwa kumalizia vyema majalo ya Stephen Ireland.
SWANSEA WAWAZIDI NGUVU NEWCASTLE
Swansea wamecheza vyema na kuwashinda Newcastle waliomaliza mechi wakiwa 10, na kuwa pigo la kwanza kwa kocha mpya wa Magpie, Steve McClaren.
Jonjo Shelvey alicheza vyema kwenye mechi hiyo, na ni yeye aliyemtilia Bafetimbi Gomis pasi safi, kisha Gomis akamlamba chenga kipa mkongwe Tim Krul kabla ya kutikisa kamba na kuwapa Swansea bao la mapema.
Swansea wanaofundishwa na Garry Monk walitawala mchezo huo na kazi haikuwawia ngumu sana, kwani muda mfupi kabla ya mapumziko wapinzani wao walipata pigo kwa Daryl Janmaat kupewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mara kwa mara Jefferson Montero.
Ingizo jipya la Swansea msimu huu, Andre Ayew alifunga bao la pili baada ya kutiliwa mpira na Gomis. Wangeweza kushinda kwa idadi kubwa zaidi ya mabao, kama mashuti ya mbali ya Montero na Gylfi Sigurdsson yangezaa matunda, bali yaliishia kugonga mwamba.
Newcastle wamepoteza mechi ya saba mfululizo ugenini katika ligi, ikijumuishwa na michezo ya msimu uliopita.
LEICESTER WAWATUNGUA WEST HAM
Mkongwe Claudio Ranieri ameendelea kufanya vyema kwenye mechi ya pili tangu arudi England, kwani vijana wake wa Leicester wamewatungua West Ham na kumwacha akifurahia, japo amewahadharisha wachezaji wake kuongeza nguvu.
Hii ni mara ya kwanza tangu msimu wa 1997/98 kwa Leicester kushinda mechi mbili za awali kwenye EPL. Bao lao la kwanza Jumamosi hii lilifungwa Shinji Okazaki na Riyad Mahrez aliandika bao la pili kwa kiki kali, likiwa ni bao lake la tatu msimu huu.
West Ham walioanza ligi vyema kwa kuwakung’uta Arsenal 2-0 Jumapili iliyopita walionesha udhaifu, lakini kipindi cha pili walikuwa bora zaidi ndipo Dimitri Payet alipochomoa bao, lakini baadaye kipa Kasper Schmeichel akimkatalia Diafra Sakho alipokaribia kabisa kusawazisha.
Nusura Schmeichel awazawadie wapinzani wao penati baada ya kuonekana kufanya makosa alipogongana na Sakho, lakini yule wa West Ham, Adrian alilambwa kadi nyekundu dakika za mwisho za mchezo kutokana na kumchezea vibaya Jamie Vardy alipopanda kwa ajili ya kona.
Kiungo chipukizi wa West Ham aliyecheza vyema dhidi ya Arsenal na kuwaliza, Reece Oxford, 16, alikuwa hovyo jana, akikutana na mambo magumu, akionekana wazi kwamba bado hajapata uzoefu wa EPL na wiki jana ilikuwa bahati tu.
Alishindwa kwenda na kasi ya washambuliaji wa Leicester na ndani ya dakika 28 tu wageni walikuwa mbele kwa 2-0 kwa kumvuruga kwenye kiungo mara nyingi.
NORWICH WAWASHANGAZA SUNDERLAND
Norwich wakicheza ugenini wamewaduwaza Sunderland katika Stadium of Light kwa kuwafunga na kupata ushindi wa kwanza wa msimu.
Russell Martin alifunga bao la kwanza baada ya kipa Costel Pantilimon kuutema mpira uliopigwa na Robbie Brady. Kana kwamba hiyo haikutosha, Steven Whittaker alitikisa nyavu kuandika la pili baada ya kugongeana vyema na Wes Hoolahan, aliyechangia bao la tatu lililofungwa na Nathan Redmond katika kipindi cha pili.
Duncan Watmore aliwafungia Sunderland bao la kufutia machozi kwenye mechi yake ya kwanza nao, huku kocha Dick Advocaat aliyewanusuru kushuka daraja akipokea kichapo cha pili katika mechi mbili msimu huu, wakitangulia kuchabangwa 4-2 na Leicester wiki jana.
WATFORD, WEST BROM HAKUNA MBABE
Watford wametoshana nguvu na West Bromwich Albion, na sasa wanaendelea kusubiri kwa hamu ushindi wa kwanza katika EPL tangu 2007.
Walitawala vyema mchezo lakini walishindwa kuipenya ngome ya West Brom iliyojipanga vyema. Odion Ighalo alikuwa na nafasi za kufunga, lakini hakuweza kufanya hivyo hata akiwa na kipa tu alipiga nje.
Mchezaji mwenye asili ya Burundi, Saido Berahino ambaye aliwika sana msimu uliopita ameonekana kupunguzwa kasi na alikosa bao la wazi dakika za lala salama.