Bodi ya Ligi Kuu ya England (EPL) huenda ikapoteza hadi pauni bilioni moja ikiwa itashindikana kuchezwa mechi zilizobaki za ligi hiyo kwa msimu huu wa 2019/2020.
Ligi hiyo imesitishwa kwa muda usiojulikana, kutokana na kusambaa kwa virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu (COVID-19) na hali bado ni mbaya kwa sababu watu wanaendelea kuambukizwa na kupoteza maisha.
Ipo hatari pia kwa klabu kuathirika zaidi kiuchumi na janga hilo kutokana na kukosa mapato kwenye mechi pamoja na fedha zitokanazo na haki za matangazo kwenye televisheni. Hali sasa inatikisa klabu hasa zile zisizokuwa imara kifedha, zikitengeneza hasara kubwa.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya EPL, Richard Masters anaonya kwamba athari kiuchmi zitazidi kuwa kubwa iwapo janga hilo la COVID-19 litaendelea kwa muda mrefu zaidi. Inatabiriwa kwamba kuna uwezekano wa klabu kadhaa kufilisika au kufungwa kabisa, hasa zile zinazomilikiwa na jamii.
Masters pia ametetea klabu zilzioamua kuingia kwenye mpango wa kuwaingiza wafanyakazi wasio wachezaji katika likizo za lazima na kutegemea sapoti ya serikali katika kuwalipia sehemu ya mishahara yao. Hata hivyo, Kamati ya Dijiti, Utamaduni, Vyombo vya Habari na Michezo imejibu kwa kuitaka EPL iache kutetea klabu kwa kitu kisichoweza kutetewa.
Baadhi ya klabu zimewaweka wafanyakazi wao chini ya mpango huo, huku mijadala ikibaki juu ya hatima ya wachezaji. Ilipendekezwa na EPL kwamba kila klabu iwakate wachezaji wake asilimia 30 ya mapato yao kwa ajili ya kukabiliana na athari za virusi vya corona.
Liverpool walikuwa wamechukua hatua hiyo, lakini baada ya kushambuliwa na washabiki na wadau wengine wa soka, wakabadili uamuzi huo juzi, wakisema kwamba walikanganyika wkenye mchakato na kufikia uamuzi ambao si sahihi, wakaomba radhi. Klabu nyingine zilizoweka wafanyakazi chini ya mpango huo ni Tottenham Hotspur, Newcastle na Norwich.
Wachezaji wamekuwa katika mtifuano mkali na EPL, wakisema kwamba wanaonewa, wakichukuliwa kama mbuzi wa kafara – kwamba ndio wakatwe mishahara kwa lazima wakati wenyewe walikuwa na wazo na kufanya mpango wa kusaidia Idara ya Taifa ya Afya (NHS).
Masters ameonya katika barua aliyomwandikia mwenyekiti wa kamati husika, Julian Knight (Mbunge) ambaye alikuwa amewalaumu wachezaji kwa kutojitolea sehemu ya mishahara yao kwenye janga hilo, akisema walikuwa na ukosefu wa maadili ndani mwa nafsi zao.
Katika barua hiyo, Masters ametetea wachezaji na kusema klabu zina haki ya kuweka baadhi ya wafanyakazi wao kwenye mpango huo wa kuwa likizo kwa lazima na kutaka serikali ichangie. Akasema kwamba kila klabu itakuwa na fursa binafsi ya kuamua mambo yao.
Akasema kwamba mpango huo ulioanzishwa na serikali na upo kisheria ni kwa ajili ya uchumi mzima, ikiwa ni pamoja na mashirika, kampuni na taasisi zikiwamo klabu, hivyo haoni kulikoni klabu zilaumiwe zikitumia fursa hiyo.
Huku kukiwa hakuna mechi zinazochezwa katika nyakati hizi, klabu za soka zina hali mbaya kifedha kwa sababu mapato yamepotea – yakiwa ni ya tiketi, mauzo ya bidhaa zao kama jezi lakini pia kuna hofu ya kupoteza fedha za kampuni za utangazaji wa mechi kwa televisheni kwa zilizobakia iwapo hazitamalizika.
Jumatatu ya wiki hii, Kocha wa Timu ya Taifa ya England – Three Lions, Gareth Southgate na mwenzake wa timu ya taifa ya wanawake, Phil Neville walitangaza kwamba watakatwa asilimia 30 ya mishahara yao kwa ajili ya kushughulikia kisa cha virusi vya corona.
Mtendaji Mkuu wa Chama cha Soka (FA), Mark Bullingham, anasema kwamba athari za kifedha kutokana na kuahirishwa kwa mechi, ikiwa ni pamoja na za EPL, Kombe la FA na matukio ya Uwanja wa Taifa – Wembley zinaweza kugharimu hadi pauni milioni 150.
Hata hivyo, Bodi ya EPL imedhamiria kumaliza mechi zilizobaki msimu huu ili kufanikisha kutimiza malengo makubwa, ikiwa ni pamoja na bingwa kupatikana kihalali kama ilivyo kwa timu za kushuka na kupanda daraja pasipo malumbano au malalamiko.
Ubelgiji wameamua kumaliza msimu kutokana na matata ya virusi vya corona na kumtangaza aliyekuwa akiongoza ligi kuwa bingwa na waliokuwa katika nafasi za chini kushushwa daraja na wa daraja la chini waliokuwa juu kupandishwa.
EPL, hata hivyo, pamoja na klabu, wanakubaliana kwamba hawatarejea uwanjani kabla ya serikali kuruhusu tena mikusanyiko, NHS kuhakikisha usalama kiafya na kwa ujumla mazingira kuwa wezeshi.
Tayari Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limesogeza mbele msimu, likitoa mamlaka kwa kila nchi kujipangia jinsi ya kumaliza msimu hu una kupanga pia muda wa kuanza kwa msimu ujao. Mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) na Ligi ya Europa nazo zimeahirishwa kwa muda usiojulikana ambapo Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) limesema si ajabu likafutilia mbali mashindano hayo kwa mwaka huu.
Janga hili litafuatiwa na athari za kiuchumi kwa sekta mbalimbali, na michezo haitakosa kuathiriwa. Mwenyekiti wa Ligi ya Taifa aliyekuwa pia Ofisa Mtendaji Mkuu wa FA, Brian Barwick anakiri kwamba soka itabadilika kutokana na janga hili, lakini anasisitiza kwamba hatua ya kwanza itakuwa kulinda klabu zisianguke.
Kuna jumla ya klabu 38 kwenye madaraja matatu na mkuu huyo anasema kwamba wanachotaka kuhakikisha ni kwamba baada ya janga hilo klabu zinabaki hizo hizo 68, isipotee hata moja.
“Ni jambo litakalokuwa gumu kwa hakika, kwa hiyo fursa zozote zile zitakazotolewa na serikali kwetu au wadau wengine katika sekta nzima ya michezo, tutazichukua kwa mikono miwili na kuhakikisha tunazilinda klabu zetu,” anasema.