MSIMU mpya wa Ligi Kuu England utaanza ijumaa wiki hii, yaani tarehe 13 ya mwaka 2021. Kwahiyo hii inakuwa Ijumaa ya kwanza inayoleta Ligi Kuu England katika msimu mpya wa 2021/2022.
Kivumbi kikali kinatarajiwa kutimka Agosti 13 mwaka huu ambapo kutakuwa na mechi 10 za kufungua pazia la EPL. Mabingwa watetezi wa EPL Manchester City wataongozwa na kocha wao Pep Guardiola kuwa wageni wa vijana wa Tottenham Hotspurs ambao wapo chini ya kocha mpya Nuno Espranto.
Kwa upande wa Liverpool watapepetana na mabwanyenye wa mjini, Norwich City, huku vijana wa Mikel Arteta watafungua dimba ugenini kwa kuchuana na wageni wa EPL Brentford.
Kana kwamba haitoshi Ole Gunnar Solskjaer atawaongoza vijana wake katika dimba lao la nyumbani la Old Traford kukabiliana na vijana wanaocheza soka la kufa mtu maarufu kama Murderball yaani Leeds United.
Mabingwa wa soka wa Ulaya, Chelsea wataongoza na kocha wao Thomas Tuchel katika dimba lao la nyumbani Stamford Bridge ambako watamenyana na Cruystal Palace.
Kwa upande mwingine mlinda mlango aliyetia fora katika Fainali za Euro wa England, Jordan Pickford atasimama langoni kuwaongoza Everton chini ya kocha wao mpya Rafa Benitez kukabiliana na watakatifu wa Sauthampton.
Nao Watford watakuwa nyumbani kupimana ubavu na Aston Villa. Wageni hao wataanza kampeni za kuwania taji la EPL baada ya kumpoteza nahodha wao Jack Grealish aliyejiunga na Manchester City.
Wababe wa zamani Newcatsle United watawakaribisha waponda nyundo wakongwe West Ham United. Vilevile Burnley watawakaribisha Brighton siku hiyo.
Mabingwa wa kombe la FA na washindi wa Ngao ya Jamii, Leicester City wataongozwa na kocha wao mpenda soka la nakshi nakshi Brendan Rogders kuwakaribisha mbwa mwitu Wolves.
Hizo ni mechi za wiki ya kwanza ya ufunguzi wa Ligi Kuu England, ambayo ilikuwa mapumzikoni kwa miezi miwili na siku kadhaa baada ya kumalizika msimu wa 2029/2021.
NINI MATARAJIO YA MSIMU MPYA?
Msimu mpya wa 2021/2022 unaanza rasmi ijumaa hii, huku wachezaji wakiwa hawajapata moto wa kutosha kuchea mechi za maandalizi kama ilivyozoeleka miaka ya nyuma.
Zamani ilikuwa rahisi kuziona timu mbalimbali zikielekea nchi za mbali kujiandaa na msimu kwa kucheza mechi za kutosha. Kwa mfano nchi kama Marekani na za bara la Asia zimekuwa wenyeji wa timu nyingi za EPL ambazo zinakwenda huko kucheza mechi za kirafiki kwaajili ya kujiandaa na msimu mpya.
Hata hivyo maandalizi ya safari hii yamekuwa tofauti kwani timu zilikuwa zinahofia maambukizo ya ugonjwa wa corona ambao unaisumbua dunia kwa sasa.
Matarajio ya sasa ni mashabiki kurejea viwanjani na kuendeleza amsha amsha zilizozoeleka. Mashabiki waliojazana kwenye mechi za Fainali za Euro na mchezo wa ufunguzi wa pazia la kuanza EPL yaani ngao ya jamii ni ushahidi kuwa msimu huu kuna matarajio makubwa mashabiki kurudi viwanjani kwa hali ya kawaida.
JICHO LA QATAR
EPL inaanza huku makocha na wachezaji wakitupia jicho kuelekea fainali za Kombe la dunia nchini Qatar mwaka ujao wa 2022. Wachezaji wanafahamu kuwa ili wajumuishwe kwenye vikosi vya nchi zao ni lazima wacheze kwa viwango vya juu katika klabu zao za EPL.
Inafahamika kuwa EPL ina wachezaji wengi ambao wanatumikia pia timu zao za taifa. Kwahiyo kila mmoja atakuwa anajifua zaidi ili kumshawishi mwalimu ampange. Kwahiyo msimu huu unaanza na ukiwa na aria kubwa kutoka kwa mashabiki,makocha na wachezaji wenyewe.
BINGWA MPYA?
Timu karibu zote zimesajili wachezaji wapya. Mabingwa wa EPL wamemsajili nahodha wa Aston Villa Jack Grealish na kumfanya kuwa mchezaji ghali zaidi EPL na England kwa ujumla. Usajili huo una maana kuwa Manchester City wameimarisha kikosi chao katika ushambuliaji wakiwa na matarajio ya kutetea ubingwa wao.
Vilevile Grealish atakuwa na kibarua cha kuonesha umwamba wake uliosababisha Man City wamwage kitita kikubwa cha fedha kumsajili cha pauni milioni 100.
Hata hivyo kutetea ubingwa ni suala ambalo linaweza kuwa gumu kwa sababu wababe wengine Liverpool, Manchester United na Chelsea wanalitolea macho taji hilo. Kwahiyo kuibuka bingwa mpya wa EPL halitakuwa jambo la ajabu msimu huu, lakini hatapatikana kirahisi sababu ya ushindani uliopo kwa timu mbalimbali.
Comments
Loading…