*Ujerumani namba moja, Hispania ya nane
Maumivu ya kufanya vibaya kwenye fainali za Kombe la Dunia yameanza kuisumbua England, ambapo imeanguka hadi nafasi ya 20 kwa viwango vipya vya ubora wa soka vilivyotolewa na Fifa.
England wameanguka kwa kishindo, kwani walikuwa wakishikilia nafasi ya nane kabla tu ya mashindano hayo kuanza nchini Brazil, ikimaanisha wameanguka kwa nafasi 12 kutokana na kushindwa mechi mbili mfululizo na kwenda sare moja.
Three Lions wanaofundishwa na Roy Hodgson wameweka rekodi mbaya, kwani tangu 1996 hawajapata kuwa kwenye nafasi ya chini kiasi hicho, ambapo sasa wapo nyuma ya hata mataifa madogo kisoka kama Bosnia-Hercegovina, Costa Rica na Marekani.
Hispania waliokuwa wanashika nafasi ya kwanza, wakiwa mabingwa watetezi waliochezea pia kichapo mara mbili sawa na England wameanguka kwa nafasi saba hadi ya nane, wakiwaposha Ujerumani kuchukua usukani.
Ujerumani walikuwa wakishika nafasi ya pili, lakini baada ya kufanya vyema kwenye fainali zilizopita, wamechupa hadi ya kwanza, na kila mtu anaona ni sahihi. Ujerumani mara ya mwisho kushika nafasi ya kwanza ni miaka 20 iliyopita.
Ujerumani walifanya vibaya sana miaka 10 iliyopita katika soka ya kimataifa, wakakaa chini na kuweka mikakati ya kung’amua vipaji na kukuza soka ya wachezaji wa ndani, mkakati ambao umelipa mwaka huu, takriban miaka 10 tangu ulipoanzishwa.
Katika viwango vipya vya ubora wa soka duniani, Argentina wanashika nafasi ya pili , wakipanda moja kutoka ya tatu waliyokuwa wakishikilia kabla, na pia walikuwa washindi wa pili kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Nafasi ya tatu inakwenda kwa Uholanzi ambao walikuwa ya 12 kabla na pia walishika nafasi ya mshindi wa tatu kwenye fainali hizo.
Colombia waliowika na kushindwa kwa ncha ya sindano dhidi ya Brazil kwenye robo fainali wanashika nafasi ya nne, wakiwapokonya Brazil eneo walilokuwamo, huku Ubelgiji waliotia timu yenye vijana na kutikisa dunia wanashika nafasi ya tano.
Uruguay waliowafunga England na Italia wanashika nafasi ya sita licha ya Luis Suarez kuendeleza utovu wake wa nidhamu kwa kutaka damu ya watu, na Brazil waliokuwa wenyeji na walioshika nafasi ya nne wametupwa ya saba katika ubora wa kiwango cha soka.
Wakati Hispania wapo nafasi ya nane kama ilivyoelezwa awali, Uswisi wameshuka hadi nafasi ya tisa kutoka ile ya sita waliyokuwa nayo kabla na Ufaransa wamepanda kwa nafasi saba hadi ya 10, kutokana na soka safi waliloonesha hadi kufika robo fainali chini ya kocha Didier Deschamps.
Comments
Loading…