Nguvu ya fedha waliyo nayo klabu za Ligi Kuu ya England (EPL) umeanza kuwatisha viongozi wa soka wa mataifa mengine, kwani wanahofu mafuriko ya wachezaji wazuri yataelekea England.
Mtendaji Mkuu wa Bayern Munich, mabingwa wa Ujerumani, Karl-Heinz Rummenigge ameeleza wasiwasi huo, akisema kwamba klabu za England zitatawala iwapo zile za Bundesliga hazitaimarishwa kifedha.
Ili kukabiliana na hali hiyo, iliyoshuhudia Manchester City wakimnyakua Kevin De Bruyne wa Wolfsburg ya Ujerumani kwa pauni milioni 55, Rummenigge anazigeukia kampuni zinazomiliki vituo vya televisheni.
Anaona kwamba huko ndiko ulipo ‘mgodi’ kwa klabu, na hivyo kampuni ziongeze mafungu ya haki za matangazo na kukaribia pauni bilioni 5.136 ambazo EPL imeingia mkataba kwa miaka mitatu ijayo.
Rummenigge anaamini kwamba ni kitita hicho kinachowapa jeuri klabu za England kuchukua wachezaji, hata wachanga kwa bei kubwa, kama walivyofanya pia Manchester United kwa kumsajili kinda wa miaka 19 aliyekuwa mshambuliaji wa Monaco kwa pauni milioni 36 za awali.
Man U wataongeza pauni milioni 7.2 ikiwa mshambuliaji huyo wa kati atafunga walau mabao 25 katika misimu minne, kiasi kama hicho cha fedha iwapo atachezea Timu ya Taifa ya Ufaransa mara 25, akiwa ndio kwanza ameitwa huko, na kiasi hicho tena iwapo atatwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia.
Klabu za EPL zilitumia pauni milioni 870 kwenye dirisha la usajili lililofungwa kiangazi hiki, wakati zile za Bundesliga zimetumia pauni milioni 290 tu.
“Udhibiti huu wa Waingereza utaendelea kwenye soko la wachezaji. Hapa tulichoona ni ncha ya barafu tu, usajili wa kitsunami utaongezeka kwa nguvu na kimo,” akasema kwa hadhari Mjerumani huyo.
Kwa sasa malipo yanayotolewa kwa dili za televisheni nchini Ujerumani katika ligi kuu yao ni pauni milioni 365, kiasi ambacho Rummenigge anaona ni kidogo, na walau kwa kuanzia kiongezwe mara dufu. Klabu za EPL zimetumia zaidi ya mara mbili ya zile za Italia – Serie A kiangazi hiki.
Rummenigge anaeleza wasiwasi wake pia kwamba hali ikiwa hivyo, wachezaji wazuri walio Bundesliga watazidi kukimbilia England, kama alivyofanya Bastian Schweinsteiger kwenda United, karibu mwaka tu tangu aliposhiriki kuwapatia Ujerumani Kombe la Dunia.
Tottenham Hotspur nao wamemsajili mshambuliaji wa Bayer Leverkusen, Son heung-Min kwa pauni miioni 22, jambo linaloonesha ukuu wa klabu za England hata zile zilizo mbali na bingwa au tatu bora.
Hata hivyo, kocha wa Timu ya Taifa ya Ujerumai, Joachim Low anaamini kwamba matumizi makubwa kiasi hicho ya fedha kwa klabu za EPL kuchukua wachezaji wa ng’ambo yataiathiri Timu ya Taifa ya Uingereza – Three Lions.
“England watatakiwa kukabiliana na ukweli mchungu kwamba wachezaji wao chipukizi hawatapata dakika nyingi za kucheza katika ngazi ya klabu na hiyo ndiyo sababu timu yao ya taifa haijafanikiwa katika mashindano yoyote makubwa,” anasema Low.
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, anasema kwamba Man U kumsajili chipukizi Martial kunadhihirisha jinsi tatizo la klabu za England si fedha, bali wachezaji sahihi. Anasema kwamba fedha zipo lakini wachezaji hawaonekani, na ndiyo maana Arsenal wameshindwa kusajili majina makubwa.