England wametangaza kikosi cha Timu ya Taifa ya Vijana, ambapo mshambuliaji aliyeibuka wa Tottenham Hotspur, Harry Kane amejumuishwa licha ya kocha wa klabu yake, Mauricio Pochettino kutotaka aingizwe humo.
Kane atakuwa na mshambuliaji wa West Bromwich Albion, Saido Beraniho mwenye asili ya Burundi lakini akaamua kuwawakilisha Waingereza kuanzia U-21. Kadhalika mpachika mabao wa Burnley walioshuka daraja, Danny Ings yupo kikosini lakini beki wa kushoto wa Manchester United, Luke Shaw ameachwa.
Kocha wa Vijana England, Gareth Southgate amekuwa na mafanikio kwani kikosi chake kimeshinda mechi 13 kati ya 14 kilichocheza, na anasema wanaingia kwenye michuano ya Ulaya inayoanza Juni 17 hadi 30 nchini Jamhuri ya Czech Republic wakiwa na matumaini ya ubingwa.
England wapo kundi moja na wababe wao katika soka ya wakubwa, Italia lakini pia wamo Ureno na Sweden. Kane, 21, aliyefunga mabao sita katika mechi nane za kufuzu kwa michuano hiyo, aliitwa kwa mara ya kwanza kwenye timu ya wakubwa Machi mwaka huu na kufunga bao dakika mbili tu akitokea benchi dhidi ya Lithuania.
Bosi wa Manchester United, Louis van Gaal atafurahi Shaw kuachwa, kwani alishasema angependa kuona akikaa kando kujiuguza baada ya kukabiliwa na majeraha mengi msimu huu wake wa kwanza Old Trafford, ambapo amecheza mechi 16 tu za ligi kuu. Alinunuliwa kwa pauni milioni 27 kutoka Southampton.
Southgate ametetea uamuzi wake wa kuwaacha wachezaji waliokuwa na sifa ya kuingia kwenye kikosi chake, ambao hata hivyo walishajumuishwa kwenye kile cha wakubwa na kocha Roy Hodgson, akisema haoni sababu ya kuwashusha tena.
Hao ni pamoja na kiungo wa Everton, Ross Barkley; winga wa Arsenal, Alex Oxlade-Chamberlain; mshambuliaji wa Liverpool, Raheem Sterling na mlinzi wa Manchester United, Phil Jones.
England wametwaa ubingwa wa Ulaya kwa U-21 mara mbili – 1982 na 1984. Mara yao ya mwisho kwenye michuano hii 2013 waliishia hatua za makundi, timu ikiwa chini ya Stuart Pearce aliyepoteza pia kazi yake.
Kiungo wa Chelsea anayeibukia, Ruben Loftus-Cheek naye ameitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha Southgate, ambacho makipa wake ni Marcus Bettinelli (Fulham), Jonathan Bond (Watford) na Jack Butland (Stoke)
Walinzi ni Calum Chambers (Arsenal), Eric Dier (Tottenham Hotspur), Luke Garbutt (Everton), Ben Gibson (Middlesbrough), Carl Jenkinson (Arsenal, kwa mkopo West Ham), Michael Keane (Burnley), Liam Moore (Leicester), John Stones (Everton) na Matt Targett (Southampton)
Viungo ni Tom Carroll (Tottenham Hotspur, kwa mkopo Swansea), Nathaniel Chalobah (Chelsea), Will Hughes (Derby County), Jake Forster-Caskey (Brighton & Hove Albion), Jesse Lingard (Manchester United), Alex Pritchard (Tottenham Hotspur), Nathan Redmond (Norwich City), James Ward-Prowse (Southampton)
Mbali na waliotajwa awali kwa upande wa ushambuliaji, wengine niBenik Afobe (Wolverhampton Wanderers), Patrick Bamford (Chelsea, kwa mkopo Middlesbrough) na Cauley Woodrow (Fulham). Kikosi hiki cha watu 27 kitapunguzwa ili wabaki 23 kabla au ifikapo Juni 2.