Uholanzi wawaadhibu Hispania
Ureno walizwa na Cape Verde
Timu za mataifa mbalimbali zimeendelea na wiki ya mechi zao, ambapo Jumanne hii imeshuhudia matokeo mchanganyiko.
England wameendeleza rekodi ya kutofungwa katika mechi tisa mfululizo walipofanikiwa kwenda sare na Italia 1-1.
Italia ambao hawajaoteza mechi tangu walipotoka kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka jana, walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wa Southampton, Graziano Pelle.
Huku timu zikiwa zimeanza na wachezaji kama wa kujaribisha, wakiwamo chipukizi, Andros Townsend aliyekuwa akilalamikiwa kwa kuingizwa kikosi cha England alisawazisha bao kwenye mechi hiyo ya kirafiki.
Winga huyo wa Tottenham Hotspur alifunga kwa kiki nzuri kutoka umbali wa yadi 20 dakika 11 tu kabla ya mpira kumalizika na ilikuwa ngumu kwa kpa mkongwe wa Italia, Gianluigi Buffon kuizuia.
Nahodha wa England, Wayne Rooney alikosa bao kwa kugonga mtambaa wa panya, akiwa katika harakati za kufikia rekodi ya mfungaji bora wa kihistoria wa England, Bobby Charlton mwenye mabao 49 huku Rooney akiwa na 47.
Kocha Roy Hodgson alijaribu kumwanzisha Phil Jones kwenye kiungo lakini mambo yakawa hovyo ndipo alipopelekwa kwenye ulinzi baada ya Chris Smalling kutoka kabla tu ya nusu ya kwanza.
Hodgson pia alimtumia vibaya winga wa Arsenal, Theo Walcott aliyemtumia mbele badala ya pembeni.
HISPANIA HOI KWA UHOLANZI
Hispania wamekumbukia mzimu wa Kombe la Dunia kwa kuanguka kwa mabao 2-0 mbele ya Uholanzi jijini Amsterdam.
Waholanzi walianza kwa kasi na kufunga mabao yote ndani ya dakika 16 za mwanzo na kuwanyamazisha vijana wa Vincente Del Bosque.
Itakumbukwa kwamba Wadachi hao waliwafyatua Hispania 5-1 kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Dunia mwaka jana.
Timu hizi pia zilikutana kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2010, ambapo Andres Iniesta aliwapa ubingwa Hispania kwa bao lake.
Vijana wa Guus Hiddink Jumanne hii walipata mabao yao kupitia kwa Stefan de Vrij‘s aliyetia kwa kichwa na Davy Klaassen kwa mkwaju, wote wakimzidi nguvu kipa wa Manchester United, David De Gea.
URENO WAAIBISHWA NA CAPE VERDE
Ureno waliokuwa wakicheza bila nyota na nahodha wao, Cristiano Ronaldo walijikuta wakiangukia pua walipocheza na Visiwa vya Cape Verde.
Japokuwa wapo katika nafasi ya kwanza kwenye hatua ya makundi ya Euro 2016, waliadhirika kwenye mechi hiyo ya kirafiki waliyocheza ugenini.
Kadhalika Ureno walimaliza wakiwa pungufu ya mtu mmoja baada ya Andre Pinto kutolewa nje kwa mchezo mbaya.
Mabao ya Cape Verde yalifungwa na Odair Fortes kabla ya Admilson Gege kutia la pili kabla ya mapumziko.
Cape Verde waliotolewa kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Mataifa ya Afrika, wanashika nafasi ya 38 katika kiwango cha soka cha Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) wakiwa kati ya Wales na Scotland.
MATOKEO MENGINE MECHI ZA KIRAFIKI
Katika mechi nyingine za kirafiki za kimataifa, Uswisi waliwalazimisha Marekani sare ya 1-1, Sweden wakaenda 1-1 na Iran pia huku Urusi wakishindwa kufungana na Kazakhstan.
Puerto Rico walipigwa 3-0 na Canada, Liechtenstein wakawafunga San Marino 1-0, Estonia wakatoshana nguvu 1-1 na Iceland.
Ukraine na Latvia walienda sare ya 1-1 pia, Luxembourg wakalala 2-1 kwa Uturuki wakati Austria walitoshana nguvu 1-1 na Bosnia Herzegovina.
Comments
Loading…