*James Rodriguez ajiunga Madrid
Wabrazil wanajipanga upya kurejesha ‘Samba’ baada ya kumteua Dunga kuwa kocha mpya anayechukua nafasi ya Luiz Felipe Scolari aliyejiuzulu baada ya kuchapwa 7-1 kwenye nusu fainali na Ujerumani na kisha 3-0 kwenye kutafuta mshindi wa tatu na Uholanzi.
Hii ni mara ya pili kwa Dunga kupewa nafasi hiyo, kama ilivyokuwa kwa Scolari ambaye mara yake ya kwanza aliwapa ubingwa. Dunga amepata kuchezea timu hiyo ya taifa kwa mafanikio makubwa.
Dunga (50) aliyekuwa nahodha wa kikosi cha Brazil 1994 kilichotwaa ubingwa wa dunia kisha akaja kuwafundisha kuanzia 2006 hadi 2011, amesema anafurahi sana kurudia kwenye kazi hiyo.
Chini ya uongozi wake, Brazil walitolewa katika hatua ya robo fainali 2010 nchini Afrika Kusini na japokuwa safari hii Brazil wamefika nusu fainali, wadau wa soka wanaona aheri ya Dunga kuliko Scolari kwa sababu anasemekana haambiliki.
Maumivu ya fainali hizo za Kombe la Dunia yanazidi ambapo Nahodha wa England, Steven Gerrard (34) ameshatangaza kubwaga manyanga, baada ya timu yake kutolewa hatua za mwanzo za makundi kwa kupoteza mechi mbili za mwanzo na yeye kutocheza vyema.
Kocha wa zamani wa England, Sven-Gorran Eriksson amependekeza kwamba Wayne Rooney (28) apewe mikoba ya unahodha wa nchi yake lakini wapo wanaoona kwamba hata fainali zijazo hatakuwapo tena kwa sababu ya kiwango chake kuendelea kushuka na umri ukipanda.
Kipa wa Manchester City, Joe Hart na Garry Cahil wa Chelsea wanapewa nafasi pia ya kutuliwa na kocha Roy Hodgson aliyeepuka panga la FA katika wadhifa huo. England wanatakiwa kujipaga vyema kwa michuano ya Ulaya 2016, lakini hawajajua wapi wanakosea katika michuano ya kimataifa.
RODRIGUEZ ASAINI REAL MADRID
Mshambuliaji wa Colombia, James Rodriguez amesajiliwa rasmi na mabingwa wa Ulaya, Real Madrid na kuwa mchezaji ghali namba nne duniani, kwani ada yake ya uhamisho ni pauni milioni 63 kutoka Monaco ya Ufaransa.
Rodriguez (23) ndiye alikuwa mfungaji bora kwenye fainali zilizopita za Kombe la Dunia, licha ya nchi yake kutolewa katika hatua za robo fainali.
Mchezaji ghali zaidi kwa maana ya uhamisho ni Gareth Bale akifuatiwa na Cristiano Ronaldo (wote wa Real Madrid) na Luis Suarez aliyenunuliwa kiangazi hiki na Barcelona kutoka Liverpool.
Rodriguez alianzia soka yake ya kulipwa katika klabu ya Envigado mwaka 2007, kabla ya kwenda Banfield ya Argentina 2008 kisha kunyakuliwa na Porto ya Ureno 2010 alikodumu hadi Julai hii akaenda kwa mabingwa wa Ulaya wanaonolewa na Carlo Ancelotti.
Comments
Loading…