Kwa kawaida huwa naandika sana juu ya michezo. Ila leo nimeona niandike kidogo juu ya virusi vya corona, inahitaji uongozi imara na kauli sahihi kwani hili ni janga la kimataifa.
Tumeona jinsi hali inavyozidi kuwa mbaya kadiri siku zinavyokwenda katika nchi mbalimbali, kwa zile ambazo hazikuwa na maambukizi kabisa zikiyapata, zikiwamo za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Lakini tumeona kwamba hali ni mbaya sana katika Italia na sasa hofu na taharuki inakuwa kubwa kwenye nchi nyingine za Ulaya, Marekani bila kusahau Mashariki ya Kati na mataifa ya Kiarabu yaliyo kaskazini mwa Afrika, ambako tangu mwanzoni mwa mwaka kuna hali kubwa ya baridi wanakostawi virusi wanaosababisha Covid-19.
wakati Italia ilipofikia kwamba watu walioambukizwa walikuwa 400 na vifo kufikia tarakimu mbili, kiongozi wa chama kinachotawala huko cha Democratic alitundika picha mtandaoni akiwa na bilauri za kinywaji chenye kilevi kinachotumiwa kabla ya chakula ili kuleta hamu ya kula ‘Apetitivo in Milan’, akiwataka watu wasibadili tabia na tamaduni zao.
Hiyo ilikuwa Februari 27 mwaka huu, pungufu ya mwezi mmoja uliopita, lakini siku 10 tu baada ya kauli yake hiyo, maambukizi yalifikia watu 5,883 na vifo vikawa 233, ndipo bosi huyo wa chama, Nicola Zingaretti, alipotundika video, safari hii akiwajulisha Wataliano kwamba naye alikuwa amepata virusi hivyo mwilini mwake.
Tunavyozungumza Italia wana maambukizi kwa watu zaidi ya 53,000 na vifo vya zaidi ya watu 4,800, huku kasi ya kusambaa kwa maambukizi ikiongezeka, na zaidi ya nusu ya maambukizi na vifo yametokea wiki iliyopita. Jumamosi maofisa waliripoti kwamba kulikuwa na ongezeko la vifo 793, likiwa ni ongezeko kubwa zaidi kwa siku moja hadi sasa.
Italia imewapita China kwa vifo, China ikiwa ndiyo nchi iliyoanza kupata virusi hivyo – kwa maambukizi na kisha vifo, kwa hiyo sasa macho na masikio ni Italia zaidi na kuona jinsi ya kuzuia maambukizi kwa wengine, huku watu katika mataifa ya Ulaya wakiwa na hofu hata ya kupoteza kabisa kazi.
Serikali imelazimika kutuma wanajeshi huko Lombardy kwa ajili ya kuzuia watu kutoka nje ya nyumba zao, wakitakiwa wajitenge peke peke ndani mwao. Huko ni upande wa kaskazini mwa nchi, lakini kwa ujumla mamlaka zinaimarisha udhibiti wa watu kukaa ndani nchini kote, wakifunga viwanja vya mapumziko, michezo na hata kuzuia mazoezi ya mbio za pole pole nje zilizokuwa zimezoeleka.
Jumamosi hii, Waziri Mkuu Giuseppe Conte, alitangaza hatua zaidi katika kile alichokiita tatizo kubwa zaidi kwa taifa hilo tangu zama za Vita ya II ya Dunia. Italia itafunga viwanda vyenye uzalishaji ambao si wa lazima sana, ikiwa ni sadaka inayolenga kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo hatari mno.
“Serikali iko hapa,” alisikika akisema, katika kile kinachoonekana ni kurejesha imani ya wananchi kwayo.
Hata hivyo, balaa hili kwa Italia linatoa onyo au hadhari kwa majirani zake wa Ulaya na Marekani kadhalika, ambako virusi vinaonekana kuingia kwa kasi. Ikiwa kuna la kujifunza kutoka Italia, basi ni kuwatenga waathirika, lakini pia na maeneo walimo kwa kuzuia kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine, kuongeza uelewa wa ugonjwa huo na kuwa wakali katika kusimamia amri na maelekezo yanayotolewa.
Licha ya kwamba sasa Italia wanaongoza kwa hatua kali zaidi duniani kwenye kudhibiti ugonjwa huo, awali mamlaka zilijisahau sana au kwenda tenge katika hatua za kudhibiti wakati walipotakiwa kuwa makini na mipaka na hali ya watu kuchangamana, wakiacha tu watu kubaki huru na kuona shughuli za kiuchumi zikiendelea.
Ipo hatari kwa mataifa mengine sasa kufuata njia ya Italia, kwa kurudia makosa ana kufikiri corona ni ugonjwa wa mchezo mchezo. Hali hii inahitaji uongozi imara, makini na wenye kuchukua hatua za hadhari haraka kuwaokoa watu wake na uchumi wao, na hawatakuwa na visingizio kwa namna yoyote iwapo wataathirika, kwani ni ugonjwa unaozuilika kwa kuchukua hatua stahiki kwa wakati mwafaka.