in

Corona na madhila ya kujifungia ndani Uingereza

ndani

MAISHA yamebadilika sana; watu hapa Uingereza sasa tunaishi katika hali iliyo ngumu kuzoeleka kutokana na mlipuko wa virusi vya corona vinavyosababisha maradhi ya homa kali ya mapafu, maarufu kama COVID-19.

Si baba, mama, bibi, babu wala watoto wadogo wanaojiona salama na tangu Waziri Mkuu Boris Johnson atoe tangazo la kuiweka Uingereza yote katika kujifungia ndani au lockdown kama wenyewe wanavyoita, basi maisha yamegeuka magumu na kiza kinene kimetanda.

Watu wamo ndani tu; hakuna kwenda kazini isipokuwa zile muhimu ambazo lazima ziendelee kama madaktari, manesi na wauguzi wengine au wauzaji wa mahitaji muhimu. Wengine sote tumeambiwa tukae ndani na kutulia, kujikinga kwa kunawa kila mara na ikibidi kuvaa barakoa kujikinga na kukinga wengine.

Hakuna kutembeleana; mitaa imekuwa tupu sana na vitakasa mikono vimekuwa ndio mpango mzima hapa. Maduka yanayouza bidhaa ambazo zinaelezwa kwamba si za lazima sana kama kwa sasa, kama nguo, vifaa vya kielektronki pamoja na huduma za maktaba, viwanja vya michezo na gyms za nje zimelazimika kufungwa.

Wataalamu na viongozi wanaendelea kufuatilia hali hii mbaya ya ugonjwa unaoendelea kuambukiza watu na kuua wengine hapa na kwingineko ili kuona kama tarehe iliyowekwa ya marufuku ya mikusanyiko hadi mwishoni mwa mwezi huu itaweza kuondolewa au kuongezwa kulingana na hali ya maambukizi na udhibiti wake.

Watu wanatakiwa kutoka kwa uchache kabisa kama ni kwenda kununua chakula, dawa na vitu vingine walivyopangiwa na hayo yanatakiwa kufanywa kwa uchache kabisa. Waziri Mkuu alilihutubia taifa muda mfupi kabla ya yeye mwenyewe kuambukizwa virusi hivyo kwamba ilikuwa wazi watu zaidi wangeendelea kufariki dunia kwa janga hili.

Watu walio na dalili za COVID-19 wanatakiwa wenyewe kuchukua hatua za kujitenga kabisa (self-isolate) na wengine kupata tiba za magonjwa nyemelezi, kwa sababu ugonjwa huo wenyewe hauna tiba wa kinga. Wanatakiwa kuvaa barakoa ili kuzuia kuambukiza wengine.

Self-isolation ndiyo njia mwafaka na rahisi kukinga wengine kuambukizwa virusi hivyo vilivyoanzia Wuhan nchini China na kusambaa katika nchi nyingi duniani, vikiua zaidi nchini Italia.

Maagizo ya Shirika la Huduma za Afya kwa Umma (PHE) ni kwamba lazima watu wabaki majumbani mwao, hakuna kwenda kazini, shuleni wala kwenye sehemu za mikusanyiko ya umma. Hakuna kutumia usafiri wa umma bila sababu maalumu kama matabibu. Kwa maana hiyo tunachoshuhudia hapa ni utupu katika utoaji huduma kama za mabasi, treni na tyubu na hata teksi.

Ili mmoja atoke lazima awasiliane na watu wa PHE ambao ni wataalamu watakaopima umuhimu wa kutoka na iwapo ni salama. Kama mimi sasa ni zaidi ya wiki tangu nimeacha kwenda kazini na huko wamekuwa kila mara wakipulizia dawa (fumigate).

Ujumbe ulifikishwa kwa wamiliki wote wa simu juu ya amri ya katazo la kutoka majumbani kwa ajili ya afya, usalama wa mwenye simu na watu wengine. Wenye dalili hapa wanaambiwa kwamba wajitenge kwa siku saba ili kuona kama virusi hao wapo na wataanza kuleta matata mwilini.

Kwa anayetokea akawa anaishi na mtu mwenye virusi vya corona hapa, sharti ni kujitenga kwa siku 14 ambazo ndizo huchukua kwa wingi kuweza kuonesha dalili za mwathirika. Serikali sasa inachukua hatua zaidi, ikiwa ni pamoja na kuandika barua na kuzituma katika majumba ya wakaazi kueleza ni akina nano watakaotakiwa kujitenga kwa walau wiki 12 – ikisema ni ‘kujiondoa kwenye jamii’.

Yeyeote aliye kwenye jamii hiyo atapewa angalizo kali sana juu ya kukaa ndani na kuepuka kuwasiliana uso kwa uso na mtu. Hawa wanazuiwa pia kutoka nje kwa ajili ya kufanya manunuzi ya chakula, dawa au mambo mengine ili kuhakikisha kukutana ni sawa na sifuri.

Hawa wa jamii hii ni pamoja na watu wenye magonjwa makubwa ambayo yatawaweka katika hatari kubwa ya kupigwa na virusi hivyo na uwezekano mkubwa ni kupoteza maisha. Wazee wanaofikia kuanzia umri wa miaka 75 na watu wenye magonjwa kama kisukari na mengineyo.

Watu wanaandikiwa barua za kujitenga kwa hadi wiki 12, ukiachilia mbali hao wazee ni wale wenye ugonjwa wa saratani ya mapafu ambamo virusi hawa huenda kushambulia, watu waliopandikizwa viungo vilivyoshindwa kufanya kazi sawa sawa kama mapafu, ini, moyo, figo na kongosho.

Hayo ndiyo maisha ya hapa kwa sasa, na kwa hakika inatisha na sintofahamu iliyopo bado ni kubwa. Kila mmoja anasali kuomba hali hii imalizike na maisha yarejee kama kawaida. Watu wenye saratani wanaoendelea kuchomwa mionzi – kemotherapi au radiotherapy kwa ajili ya saratani ya mapafu wanahusika.

Lakini pia watu wenye saratani ya damu au ya kwenye uteute unaokaa kwenye maungio ya mifupa wakiwa katika hatua yoyote ya matibabu wanatakiwa kutulizana nyumbani kwa wiki hizo 12 na matabibu watawafikishia dawa huko huko.

Wengine ni wale wenye saratani ya kwenye protini zao na wengine ambao kwa ujumla hali yao imepunguza nguvu ya kinga ya miili yao. Kadhalika katika kundi hili ni wenye matatizo ya mfumo wa hewa na kupumua, wenye pumu, wajawazito wenye matatizo ya moyo kwa sababu kimsingi hawa watashambuliwa na kuumizwa zaidi na virusi hawa kama si kupoteza maisha kabisa.

Inavyoendelea sasa, ikiwa ni pamoja na kwa baadhi ya watu ninaowafahamu, ni kwamba wanavyojitenga ikiwa wanaishi kwenye familia moja au kundi, ni mhusika kujitenga chumbani kabisa na akienda kujisaidia awe amevaa barakoa.

PHE wanashauri kwamba wagonjwa au wanaohisiwa kuwa na virusi hawa wakae kwenye chumba chenye hewa ya kutosha – yaani kuwe na madirisha au uwazi ili kwamba hewa iingie na kutoka lakini ihakikishwe kwamba wanatenganishwa na wengine walio wazima na pia matumizi ya bafu na maliwato yawe tofauti.

Ikiwa ni nyumba isiyokuwa na bafu la ziada kwa ajili ya mgonjwa imeshashauriwa kwamba uwekwe mpango wa rota kwa ajili ya kunawa au kuoga ambapo mgonjwa awe wa mwisho kutumia huduma husika na baada ya hapo upulizaji dawa ufanywe kuua virusi wanaoweza kuwa wamebaki humo.

Kwa wanaotumia jiko pamoja na wengine PHE imeelekeza mgonjwa asitumie wakati wengine wakiwapo na ikiwezekana barakoa zivaliwe na vyakula viliwe kwenye vyumba vya wahusika wakiwa peke peke.

Ni zoezi ambalo si la mchezo mchezo – masharti ni mengi na kwa hakika lazima ushirikiano utolewe kwa kiasi kikubwa kutoka kwa waajiri ambao baadhi wameendelea kulipa mishahara kama kawaida na wengine wakiikata sambamba na posho. Lakini familia na rafiki wanaoishi pamoja lazima wawe katika ushirikiano wa hali ya juu ili kulindana.

Serikali iliweka bayana mapema orodha ya wafanyakazi muhimu ambao watoto wao lazima waendelee kupewa huduma za hali ya juu dhidi ya janga hili kuwaepusha. Hawa ni pamoja na wafanyakazi wa kada ya afya na huduma za jamii, wanaoendesha mfumo wa haki kama mahakama, polisi na magereza; wale wa kada ya dini, wa kwenye wakfu za kusaidia watu, waandishi wa habari na walio kwenye sekta ya usafirishaji.
Wengine ni wale walio katika sekta za uzalishaji, uuzaji na usambazaji wa huduma muhimu za kila siku pamoja na watawala.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Lack of sports investment in Tanzania

Tanzania Sports

Klabu EPL zajipanga