Huku janga la virusi vya corona likiendelea kutikisa, klabu nazo zinaonekana kuyumba kiuchumi na mabingwa watetezi wa Hispania, Barcelona, wanajadiliana na wachezaji wao ili kuwapunguzia mishahara.
Barcelona, ambao pamoja na Real Madrid wamekuwa wakipata mgawo mkubwa sana kwenye mapato ya siku za mechi, wapo katika wakati mgumu kutokana na kufutwa kwa mechi za Ligi Kuu ya Hispania – La Liga na haijulikani zitarudia lini.
Inaelezwa kwamba klabu hiyo imeanza mazungumzo kwanza na wachezaji waandamizi, wakiongozwa na Lionel Messi, kwa ajili ya kuona uwezekano wa kutengua mikataba yao kwa kuwakata baadhi hadi asilimia 70 ya mishahara yao.
Wachezaji wanaelezwa kwamba wapo katika hali nzuri ya kupokea ombi la uongozi, lakini hawatasaini hadi wajue ni lini ligi itarudia na kuona pia mustakabali wao. Ni Barcelona pekee katika klabu za La Liga waliochukua hatua ili kujikinga na mdororo wa uchumi uliosababishwa na janga la virusi hivyo hatari vinavyoendelea kusambaa na kuua watu katika nchi mbalimbali.
Bodi ya La Liga, hata hivyo, ilisema kwamba itajitahidi kuwasaidia wanachama wake wakati huu mgumu kiuchumi. Inatarajiwa kwamba klabu nyingine zitachukua hatua pia. Real Madrid wanaotamba kwa ukwasi, wamekaa kimya na kila mchezaji anaendelea kujitenga kwa karantini, baada ya mmoja wao – anayecheza mpira wa kikapu – kupatikana na maambukizi ya virusi hivyo.
Sheria za kazi nchini Hispania zinaruhusu kampuni kuchukua hatua za dharura kuwaweka kando wafanyakazi wakati wa mazingira yasiyo ya kawaida kama haya, lakini Barcelona wanapendelea zaidi kufanya kwa kujadiliana na wahusika ili baadaye wasonge mbele sawa. Sheria pia inataka wafanyakazi husika warejeshwe baada ya hali kutengamaa.
Upo uwezekano wa kampuni zinazodhamini ligi hiyo kuacha kutoa fedha au kutaka kurejeshewa walizotoa kwa sababu ya masharti na vigezo kutozingatiwa kutokana na janga la corona. Wenyewe wanakabiliana na hali ngumu, wakisema kwamba watapunguza zaidi ya wafanyakazi 1,000.
Wakurugenzi wa Barcelona walio Camp Nou walikuwa wamesema Septemba kwamba wangekuwa klabu ya kwanza kuvunja rekodi ya mapato ya euro bilioni moja (saw ana £924m), lakini kwa hali inavyokwenda sasa, huenda tangazo hilo likafutwa baada ya kufanyiwa mapitio.
Kima hicho pia kilikuwa kikitarajia na kuuza wachezaji kadhaa ili kuzalisha pauni milioni 92 na nyingine ni mapato mbalimbali, ikiwa ligi inaendelea. Sasa wanasema kwamba kuzuiwa kwa michezo ya La Liga ambayo haijulikani itaanza tena lini, kumeiathiri klabu sana kimapato na kwa ujumla kiuchumi.
Klabu ya Barcelona inategemea mapato kutokana na tiketi za viingilio vya mechi, ziara za wageni kwenye makumbusho yao lakini pia mauzo ya jezi za wachezaji wao na vitu vingine vya soka na yote hayo yamezuiwa. Inatarajiwa kwamba wadhamini watazuia kiasi cha fedha kilicho kwenye mikataba kwa sababu haijatekelezwa kuendana na vigezo na masharti, lakini pia wao pia wana matatizo yaliyosababishwa na corona.
Klabu inaweka bayana kwamba kuahirishwa kwa mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) dhidi ya Napoli pekee kumeigharimu klabu hii pauni milioni 5.5 na sasa tayari wamefunga malango yote ya uwanja wao na maduka na vingine vilivyomo kuzunguka complex hiyo.
Hata hivyo, wachezaji wanaona kwamba hawataweza kukubaliana dili lolote kabla ya kujua msimu wenyewe wa La Liga wa 2019/2020 utamalizika lini. “Ni wazi kwamba mgogoro huu wa Corona utaleta athari hasi kwenye sekta ndogo ya soka na kwenye sekta ya michezo kwa ujumla. Klabu inatakiwa kuwa tayari kukabiliana na hali yoyote itakayojitokeza,” klabu wakasema.