*Wawafumua Argentina na kutwaa ubingwa Copa America
*Ndilo kombe kubwa la kwanza kutwaa kwenye ardhi yao
Chile wameweka historia nyumbani, baada ya kuwazabua Argentina 4-1 kwa mikwaju ya penati na kutwaa ubingwa wa michuano ya Copa America.
Hili ni kombe la kwanza kutwaa nyumbani katika historia ya soka yao, ambapo wakati Alexis Sanchez wa Arsenal aliyeng’ara tangu mwanzo alicheka hadi mwisho, Lionel Messi wa Argentina alikumbana na kigingi.
Sanchez ndiye alitia kimiani mkwaju wa ushindi na kushangilia kwa nguvu kubwa, huku Gonzalo Higuain wa Argentina alikosa shabaha wakati penati ya mwenzake, Ever Banega ilipanguliwa na kipa Claudio Bravo.
Higuain alikuwa na siku mbaya, kwa sababu katika dakika ya 90 alishindwa kufunga bao la wazi ambalo lingemaliza mchezo katika muda wa kawaida. Wakiwa suluhu walilazimika kucheza dakika 30 za nyongeza lakini hakuna aliyebahatika kufumania nyavu za mwenzake.
Sanchez naye nusura afunge katika dakika za mwanzo za muda wa nyongeza lakini ilibidi wafike hatua za matuta ambapo Argentina waliowatoa Paraguay 6-1 kwenye nusu fainali walijikuta wakiachwa hoi.
Timua ya Taifa ya Argentina, au Le Albiceleste kama wanavyojulikana kwa utani, hawajatwaa taji kubwa kwa miaka 22 sasa, kwani mara ya mwisho walitwaa hili walilobeba Chile la America nchini Ecuador 1993.
Kwa upande wa mabingwa wapya, hii ni mara ya kwanza kutwaa kombe hili katika kipindi cha miaka 99 na nusura imalizike karne bila lenyewe. Hata hivyo, kutokana na uimara wa kikosi chao, wengi walisema wakikosa safari hii huenda ikabaki historia.
Chile ni moja ya timu zilizocheza mashindano haya kwa mara ya kwanza kabisa 1916 nchini Argentina lakini walichoweza kufanya vyema zaidi ilikuwa ni kupata ushindi wa pili, ambao wameutwaa mara nne; 1955, 1956, 1979 na 1987.
Kwenda kwa hesabu hapa inaonesha kwamba wametwaa ubingwa huu baada ya kucheza mechi 173 katika mashindano yote, yaani tangu mashindano ya kwanza ya Copa America ya 1916.
Chile hawakucheza kwa kushambulia kishinikizo wakijua uzuri wa Argentina, hivyo walichofanya ni kuwavuta, kucheza kwa nidhamu wakijituliza lakini mara moja moja walifanya mashambulizi wakiongozwa na Sanchez na Charles Aranguiz.
Washabiki wao walikuwa wakishangilia mwanzo mwisho kwenye fainali hii ya Jumamosi, wakipeperusha bendera zao nyekundu. Kila timu ilifunga penati ya kwanza, Matias Fernandez akitia yake kwenye kona ya juu kwa Chile kabla ya Messi kuingiza yake kima cha chini kwenye kona.
Hata hivyo, baada ya kiungo wa Juventus, Arturo Vidal kupiga mkwaju mkali na kujaa wavuni kwa Chile, Higuain alipiga juu ya mwamba; Aranguiz akafanya mabao kuwa 3-1 ndipo Banega akazuiwa na Bravo huku Sanchez akicheka na nyavu na kuanza ‘amsha amsha’ ya aina yake ndani na nje ya uwanja.
Argentina wananyang’anywa tonge la pili mdomoni, baada ya mwaka jana kuukosa ubingwa wa dunia wakiangalia mbele ya Wajerumani, ambapo Mario Goitze aliyeingia kipindi cha pili alitia bao katika dakika za mwisho mwisho.
Messi wa pia atakumbuka sana kushika nafasi ya pili, kwani msimu uliopita kwenye tuzo za mwanasoka bora duniani alitarajia lakini akaishia nafasi hiyo hiyo huku hasimu wake, Cristiano Ronaldo wa Ureno akiitwaa Ballon d’Or ambayo Messi alipata kuichukua mara nne