Vigogo wa Ligi Kuu ya England, Chelsea wamerejea kwa nguvu kileleni kwa kuwachapa Stoke 2-0, huku kocha wao, Jose Mourinho akiwasifu kwa kujituma kwao.
Hii ni mara ya nne Chelsea kuingia Krismasi wakiwa katika nafasi ya kwanza, Cesc Fabregas akitoa pasi ya 12 kuzaa bao katika mechi 17, lakini nyota wao Eden Hazard akipata majeraha. Mourinho alisema ni hali ya kipekee kuingia kwenye sikukuu wakiwa nafasi ya kwanza.
Ushindi wao haukuwa rahisi, kwani Stoke walicheza vyema licha ya kuruhusu bao dakika ya pili tu, lililofungwa na beki na nahodha wa Chelsea, John Terry. Fabregas alifunga bao la pili dakika ya 78.
Steven Nzonzi alipata nafasi kadhaa za kufunga lakini mashuti yake ama yalidakwa au kwenda nje. Chelsea wamefikisha pointi 42, tatu zaidi ya wanaoshika nafasi ya pili, Manchester City.
Hazard anaonekana kuumia enka yake, kutokana na kuchezewa vibaya na Jonathan Walters. Kabla ya mechi, wengi walikuwa wakijiuliza iwapo nyota wa Chelsea wangeweza kufanya vyema katika mwezi wenye baridi kali huko dimba la Britannia.
Stoke waliwafunga Arsenal msimu huu na pia katika msimu uliopita Stoke waliwanyuka Chelsea hapo, ambapo Mourinho alisema timu inayoshinda katika uwanja huo lazima iwe na wachezaji wazuri.
“Ushindi huu unamaanisha zaidi ya pointi tatu tulizovuna. Huwezi kufanikiwa hapa Stoke kama huna wachezaji wazuri wanaojituma na ambao kiakili wapo timamu,” akasema Mourinho.
Utata ulitokea kwenye mehi hiyo, baada ya mwamuzi Neil Swarbrick kumpa kadi ya njano Phil Bardsley wa Stoke licha ya kumchezea rafu mbaya na hatari, kiungo wa Chelsea, Hazard.
Kocha wa Stoke, Mark Hughes alisema kwamba vijana wake walikanganyikiwa baada ya kuruhusu bao la mapema kiasi cha kuathiri mpango wao wa kucheza. Hata hivyo alisema kwamba Chelsea hawakucheza vyema tofauti na alivyotarajia.
MSIMAMO WA LIGI
Baada ya mechi 17 kwa kila timu, Chelsea wanaongoza wakiwa na pointi 42 na uwiano wa mabao 25, mzuri kuliko timu zote, wakati Man City wana pointi 36 na uwiano wa mabao 22. Manchester United wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 32 na uwiano wa mabao 12 huku West Ham wakifunga nne bora kwa pointi 31 na uwiano wa mabao 10.
Southampton wanashika anfasi ya tano kwa pointi 29, Arsenal ni wa saba kwa pointi 27 sawa na wapinzani wao wa London Kaskazini, Tottenham Hotspur. Hata hivyo, ni kuanzia hapo kwa Spurs kwenda chini timu zote zina uwiano hasi wa mabao, isipokuwa Everton wenye sifuri, kwani Spurs wana -1.
Swansea ni wa nane kwa pointi 23, Newcastle wa tisa kwa kujikusanyia pointi 23 huku Liverpool wakifunga 10 bora kwa pointi moja pungufu ya Newcastle.
Everton waliozoea kuwa nafasi sita za juu wanashika ya 11 kwa pointi 21, mabao yao ya kufunga na kufungwa yakilingana, Aston Villa wanafuata kwa pointi 20, Stoke na Sunderland pointi 19 kila moja wakati West Browmwich Albion na Queen Park Rangers wanafungana kwa pointi 17.
Crystal Palace wanashika anfasi ya 17 kwa pointi 15 sawa na Burnley, lakini Burnley wapo chini katika mstari wa kushuka daraja kutokana na uwiano wao mbaya
Comments
Loading…