in , , ,

Chelsea sasa ushindi

*Man U wapigwa, Van Gaal tumbo joto

*Leicester wapiga tena, hawakamatiki

Chelsea wameanza maisha bila kocha wao Jose Mourinho kwa ushindi wa
3-1 dhidi ya vibonde Sunderland, lakini bado wanasota mbali chini
kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL).

Katika mechi iliyoshuhudiwa na mmiliki Roman Abramovich; kocha mpya,
Guus Hiddink na mshambuliaji wao nyota wa zamani, Didier Drogba wakiwa
juu jukwaani, wachezaji wamejengea umma hisia kwamba walikuwa
wakimhujumu Mourinho.

Mmoja wa wachambuzi wa masuala ya michezo aliuliza Jumamosi hii ikiwa
wangethubutu kushinda mara baada ya Mourinho kuondoka, bosi huyo akiwa
amesema majuzi tu kwamba anahisi usaliti katika kazi kubwa aliyofanya
kuwajenga nyota wake.

Mashabiki wakitoa yamoyoni..
Mashabiki wakitoa yamoyoni..

Ndio maana bado kivuli cha kocha huyo aliyefundisha vipindi viwili na
kuwapa ubingwa wa England mara tatu bado kinazingira Stamford Bridge.
Washabiki wengi walionekana kumuunga mkono Mourinho wakiwa na mabango
yenye picha zake na makombe pamoja na maneno ya shukurani kwake.

Washabiki hao hao waliwazomea Diego Costa na Cesc Fabregas kabla na
wakati wa mechi, wakiamini kwamba ndio walikuwa kiini cha kufukuzwa
kwa kocha huyo. Bao la kwanza la Chelsea lilifungwa na beki wa
pembeni, Branislav Ivanovic ambaye pia amepata kutuhumiwa kumhujumu
Mourinho.

Bao la pili lilitiwa kimiani na Pedro ambaye hakupata kuonesha makali
yake baada ya mechi yake ya kwanza hapo na la tatu lilifungwa na Oscar
kwa penati. Huyu pia amekuwa katika kiwango duni na Mourinho alikuwa
akifikiria kumuuza.

Sunderland walipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Fabio Borini,
lakini kwa ujumla ilikuwa siku iliyojaa hisia juu ya Mourinho.
Kulikuwapo bango moja lililosomeka kwa tafsiri ya Kiswahi: ‘Panya
Watatu – Hazard, Cesc na Costa’. Wachezaji wa Chelsea pia walikuwa
wakizomewa kwa pamoja na bao likifungwa washabiki walitaja jina la
Mourinho.

MAN U WAPIGWA, VAN GAAL AHOFIA KAZI

Van Gaal, ahofia kazi yake...
Van Gaal, ahofia kazi yake…

Manchester United wamepoteza mechi muhimu kwa kufungwa 2-1 na Norwich,
kipigo cha kushangaza katika dimba lao la Old Trafford kiasi cha kocha
Louis van Gaal kusema ameanza kuhofia juu ya hatima yake.

Matokeo hayo yanafanya Man U kupigwa mara tatu mfululizo katika
mashindano yote, ambapo baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa
Ulaya (UCL), walipoteza mechi iliyopita ya EPL pia.

Washabiki waliwazomea wachezaji wao wakiona kwamba wanawwaangusha na
Van Gaal anazidi kuwa kwenye shinikizo, ambapo alishaonywa na
washabiki, wachezaji wa zamani wa United na wachambuzi wa soka kwamba
mfumo anaotumia haufai.

Mara ya mwisho Norwich kuwashinda United uwanjani hapo ni 1989, na
licha ya Jumamosi hii Man U kutawala mchezo kwa asilimia 71, walikuwa
ni Norwich walioibuka na ushindi kupitia mabao ya Cameron Jerome na
Alex Tettey, huku Anthony Martial akifunga la kufutia machozi.

Alipoulizwa baada ya mechi iwapo anahofia kupoteza kibarua chake, Van
Gaal alijibu: “Ndio, bila shaka, nina wasiwasi juu ya hilo kwa sababu
najua kuwa na imani na kocha ni muhimu sana.”

Hakutoa jibu la moja kwa moja alipoulizwa iwapo atapewa muda wa
kubadilisha mambo Old Trafford, bali alisema: “Ndio, nadhani hivyo
lakini siwezi kujua, duniani humu huwezi kujua. Si juu yangu lakini
tutaona.”

Aliongeza: “Huo ndio ulimwengu wa soka. Najua hilo, bodi yangu inajua
hilo, wachezaji wangu wanajua pia. Sidhani kwamba kubadilisha kocha
kutaleta mafanikio ya haraka – lakini hilo ndilo ninaloamini, pengine
haivutii sana kihivyo.

“Siku zote huwa najitathmini kwa sababu nafikiri ni sehemu ya falsafa
yangu. Lakini falsafa yenyewe pia hufanya mageuzi – mie si kocha yule
yule wa miaka 25 iliyopita. Hivyo, siku zote unatakiwa kujitathmini na
falsafa hiyo ni muhimu sana kwangu. Kwa sababu ya hiyo, mimi ni – au
labda niseme sasa kwamba nilikuwa kocha mwenye mafanikio sana.”

Kocha Msaidizi, Ryan Giggs alionekana akifoka na kutoa maelekezo kwa
wachezaji wakati kocha wake akiwa amekaa kwenye benchi na vitabu
vyake. Kuna taarifa kuwa Van Gaal hutawala kidikteta wala hamsikilizi
msaidizi wake katika mambo mengi, ikiwa ni pamoja na mfumo wa kutumia
na kupanga timu.

LEICESTER HUWAAMBII KITU, KILELENI NOELI

Riyad Mahrez akifunga moja kati ya penati zake mbili, dhidi ya Everton
Riyad Mahrez akifunga moja kati ya penati zake mbili, dhidi ya Everton

Leicester wameendeleza mwendo wa ushindi na kujihakikishia kwamba
watakuwa kileleni wakati wa Krismasi baada ya kuwafunga Everton 3-2
kwenye dimba la Goodison Park.

Vijana hao wa Mtaliano Claudio Ranieri ‘The Tinkerman’ walipata mabao
mawili kwa njia ya penati zilizofungwa na Riyad Mahrez zilizotolewa
baada ya Ramiro Funes Mori kumchezea vibaya Shinji Okazaki.

Baada ya penati ya kwanza, Romelu Lukaku aliwasawazishia Everton,
lakini kipa wao, Tim Howard alimchezea vibaya Jamie Vardy na kumpa
fursa Mahrez kutia bao la pili. Okazaki aliwafungia Leicester bao la
tatu na katika dakika za mwisho Kevin Mirallas akawafungia Everton bao
la pili.

Mwenendo wa Leicester unawashangaza wengi, kwani wataalamu wa soka
walikuwa wametabiri hadi Agosti mwaka huu kwamba wangeshushwa daraja,
lakini ushindi baada ya ushindi, ikiwa ni pamoja na dhidi ya timu
kubwa umewafanya kutabiriwa kutwaa ubingwa.

Wameweka historia katika EPL, kuwa timu waliokuwa mkiani mwa msimamo
wa ligi Krismasi moja (ya mwaka jana) na kuwa kileleni Krismasi
inayofuata. Kibarua kinachofuata ni Desemba 26 watakapowafuata
Liverpool wanaofundishwa na Jurgen Klopp.

MATOKEO MENGINE EPL

Matokeo mengine ya EPL, kwa michezo iliyochezwa jana.
Matokeo mengine ya EPL, kwa michezo iliyochezwa jana.

Katika matokeo mengine Jumamosi hii Southampton wakicheza nyumbani
walizidiwa nguvu kwa kufungwa 2-0 na Tottenham Hotspur, Stoke nao
wakashindwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kulala 2-1 mbele ya
Crystal Palace.

West Bromwich walifuata mkono wa timu za nyumbani, kama Manchester
United kufungwa, pale walipolala 2-1 kwa Bournemouth huku vibonde
wawili – Newcastle wakienda sare ya 1-1 na Aston Villa.

Jumapili hii Watford wanawakaribisha Liverpool na Swansea ni wenyeji
wa West Ham. Jumatatu Arsenal walio nafasi ya pili wanawakaribisha
Emirates Manchester City wanaoshika nafasi ya tatu na atakayeshinda
ndiye atakuwa nafasi ya pili siku ya Krismasi.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Buriani Jimmy Hill, utakumbukwa daima

Tanzania Sports

Guardiola aaga Bayern