*Spurs, Newcastle watolewa
Chelsea wamefanikiwa kufika nusu fainali ya Ligi ya Europa, huku Tottenham Hotspurs na Newcastle wakitupwa nje.
Chelsea walijihakikishia nafasi kwenye nusu fainali licha ya kucheza hovyo kipindi cha pili Alhamisi hii kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Rubin Kazan nchini Urusi.
Waliingia kwa kiburi cha ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya awali, kisha wakapata bao la dakika ya tano la Fernando Torres na kudhani walishavuka.
Hata hivyo, Ivan Marcano alisawazisha kwa kichwa dakika ya 51 kabla ya Victor Moses kutupia la pili dakika nne tu baadaye.
Kazan waliongeza mabao mawili kupitia kwa kiki ya Gokdeniz Karadeniz na penati ya Bebras Natcho dakika ya 62 na 75, ambapo walihitaji bao moja zaidi, ambalo hawakupata hata hivyo.
Spurs kwa upande wao walipoteza mechi kwa mikwaju ya penati, baada ya kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Basel ya Uswisi, matokeo sawa na yalivyokua White Hart Lane mechi iliyopita.
Tom Huddlestone na Emmanuel Adebayor walikosa penati zao wakati Basel wakizifunga kiufundi bila wasiwasi na kuwarejesha nyumbani waendelee kupambana kutafuta nafasi ya nne ili wacheze Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Magoli ya Spurs katika muda wa kawaida yalifungwa na Mmarekani Clint Dempsey, wakati yale ya wenyeji yalifungwa na Mohamed Salah na Aleksander Dragovic.
Spurs walimaliza wakiwa 10, kwani beki wao, Jan Vertonghen alipewa kadi nyekundu kwa mchezo wa rafu.
Wawakilishi wengine wa England, Newcastle walitupwa nje ya michuano hiyo na Benfica ya Ureno, baada ya kushindwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani.
Newcastle walikuwa na deni la 3-1 waliyofungwa mechi ya kwanza, na Alhamisi hii wanaweza kuwalaumu waamuzi, kwani mabao mawili ya Papiss Cisse yalikataliwa, likaja kukubaliwa moja la dakika ya 71.
Wakati wakitafuta bao la pili ili kuweka mambo sare, muda uliwatupa mkono na dakika ya 90 Benfica walifunga kupitia kwa Eduardo Salvio.
Katika mechi nyingine, Lazio walitoka sare ya 1-1 na Fenerbahce. Kwa matokeo ya robo fainali hiyo ya pili, timu zilizovuka ni Basel, Benfica, Chelsea na Fenerbahce.